Prime
Kinachombeba Depu Yanga akifanya balaa kwa dakika 442 tu
DAKIKA 442 alizotumia mshambuliaji wa Yanga, Laurindo Dilson Maria Aurelio maarufu Depu kucheza jumla ya mechi sita za mashindano tangu atue kikosini hapo, zimeonyesha kuwashtua wengi.
Hiyo imetokana na nyota huyo raia wa Angola kuwa na wastani mzuri wa kuhusika na mabao ndani ya kikosi hicho jambo ambalo linambeba kwa nafasi yake ya ushambuliaji.
Depu aliyetambulishwa Yanga Januari 15, 2026 katika usajili wa dirisha dogo akitokea Radomiak Radom ya Poland, mapema tu ameonyesha ni mshambuliaji tegemeo kikosini hapo.
Takwimu zinaonyesha Depu amecheza mechi sita za mashindano tofauti akiwa na jezi ya Yanga mgongoni namba 40 na kufanikiwa kuhusika kwenye mabao sita yaliyotokana na kufunga matano na asisti moja.
Huo ni mwanzo mzuri kwa Depu kwani inaonyesha kila mechi amekuwa na uwezo wa kuhusika na bao moja, akiwa na wastani wa kuhusika na bao kila baada ya dakika 63 kitu ambacho ni faida kwa Yanga katika mapambano yake baada ya kushindwa kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikibaki kupambania mataji ya ndani ambayo ni Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na Kombe la Muungano. Kumbuka tayari Yanga msimu huu 2025-2026 imebeba Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi kabla ya ujio wa Depu.
LIGI KUU
Moto wa Depu ulianza kuwashwa katika Ligi Kuu Bara, Januari 19, 2026 wakati Yanga ikiichapa Mashujaa mabao 6-0 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Mechi hiyo Depu aliingia katika dakika ya 55 kuchukua nafasi ya Maxi Nzengeli, ambapo ilipofika dakika ya 81, akatoa pasi kwa Mudathir Yahya aliyefunga bao la tano.
Baada ya hapo, dakika ya 89, Depu akafunga ukurasa wa mabao alipotikisa nyavu akimalizia mpira wa friikiki kutoka kwa Allan Okello uliomshinda kipa Erick Johora. Dakika 35 alizotumia siku hiyo, aliasisti na kufunga, akihusika katika mabao mawili kati ya sita.
Januari 28, 2026 hapohapo KMC Complex, Depu akazifumania nyavu mara mbili wakati Yanga ikishinda 3-1 dhidi ya Dodoma Jiji.
Katika mechi hiyo, Depu alianza kikosi cha kwanza ambapo aliisawazishia Yanga katika dakika ya 45+5 kwa mkwaju wa penalti baada ya mshambuliaji wa Dodoma Jiji, William Edgar kutikisa nyavu za wapinzani katika dakika ya 40.
Kisha dakika ya 60, Depu akaunganisha kwa kichwa krosi ya Duke Abuya na kuiandikia Yanga bao la pili. Baadae Prince Dube akahitimisha ushindi kwa bao la dakika ya 66. Siku hiyo Depu alitumika kwa dakika zote 90, jumla akiwa amecheza mechi mbili kwa dakika 125.
LIGI YA MABINGWA
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ikiwa imepangwa kundi B na kumaliza nafasi ya tatu ikikusanya pointi nane zilizoinyima timu hiyo kufuzu robo fainali, Depu alicheza mechi nne kwa dakika 317. Alikuta tayari Yanga imecheza mechi mbili za hatua hiyo ya makundi.
Mechi hizo nne za CAF kwa Depu akiwa Yanga, amefunga mabao mawili na yote yamepatikana katika mechi ya mwisho hatua ya makundi katika ushindi wa 3-0 dhidi ya JS Kabylie.
Alianza kuonekana Yanga ilipofungwa 2-0 ugenini dhidi ya Al Ahly ambapo alicheza dakika zote tisini, kisha katika sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Mafarao hao kutoka Misri akicheza kwa dakika 73.
Mechi ya tatu alicheza kwa dakika 67, Yanga ilipofungwa bao 1-0 ugenini dhidi ya AS FAR Rabat, kisha mechi ya nne akitumika kwa dakika 87 dhidi ya JS Kabylie, siku ambayo alifunga mabao mawili, la kwanza kwa penalti, kisha kwa kichwa.
Huku kimataifa hakuwa na asisti akiwa amecheza jumla ya dakika 317 katika mechi hizo nne akifunga mabao mawili yanayomfanya jumla kuwa nayo matano katika mechi sita.
KINACHOMBEBA
Akiwa na urefu wa mita 1.81 ambayo ni sawa na Futi 5.11, Depu ni mzuri kwa mipira ya juu akifanikiwa kufunga mabao mawili kwa kichwa dhidi ya Dodoma Jiji katika Ligi Kuu Bara na dhidi ya JS Kabylie katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mbali na matumizi mazuri ya kichwa chake katika kufunga, pia ameaminiwa katika kupiga penalti na zote mbili ametikisa nyavu tena kwa kuwatesa makipa akiwahamisha upande. Alianza kumtesa Ally Salim wa Dodoma Jiji, kisha Seif Benrabah wa JS Kabylie.
Matumizi mazuri ya kichwa, mikwaju ya penalti na kutumia miguu yote miwili katika uchezaji kutokana na kwamba mabao matatu kati ya matano ameyafunga kwa mguu wa kulia huku mguu wa kushoto akitoa asisti moja, ni vitu vinavyombeba mshambuliaji huyo kuifanya kazi yake vizuri.
WASIKIE WADAU
Kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua, alisema Depu ameanza kwa kuonyesha kiwango kizuri, ana vitu vingi anavyovifanya uwanjani wakati mwingine vinaleta usumbufu kwa mabeki wa timu pinzani.
"Sio mshambuliaji mvivu ndiyo maana analetewa mipira anafunga na anakwenda kuitafuta na kutengenezea wengine wafunge, anafunga kwa kutumia kichwa na miguu, anajiamini kupiga penalti, hivyo uwepo wake Yanga naona unakwenda kuongeza idadi ya mabao," alisema Chambua.
Kwa upande wa mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Singida United, Kipanya Malapa, alisema: "Depu kabadilisha uchezaji kwa sasa anategemewa, akigusa mpira mara ya kwanza ya pili anakufurahisha, tofauti na mwanzo mipira ilikuwa ngumu kuonyesha ni mshambuliaji gani tegemeo wa kumpa mara kwa mara.
"Naamini kwa sasa atakuwa tegemeo katia kikosi cha kwanza, lakini akipona na kuwa fiti kabisa Clement Mzize ataongeza changamoto ya ushindani wa namba dhidi yake."
Staa mwingine wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Mohamed Hussein 'Mmachinga' alisema: "Kwa kiwango alichoonyesha Depu, kimemtafsiri ni mchezaji mwenye uwezo wa juu na usajili wake una mantiki, wachezaji wanaosajiliwa dirisha dogo wanatakiwa wawe tayari kwa kazi na siyo kupewa muda wa kujitafuta."
Winga wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Edibily Lunyamila alisema endapo kama kocha wa Yanga, Pedro Goncalves ataamua kuwachezesha muda mwingi Depu na Prince Dube anaona watazalisha mabao mengi zaidi.
"Dube ana uwezo wa kutokea pembeni na kuwahi kwa haraka kwenda kukaa katika nafasi ya kufunga, lakini Depu ana uwezo wa kutumia vizuri mipira akikaa katika boksi, wakicheza kwa pamoja watatengeneza mabao mengi zaidi, kwa kiwango alichokionyesha Depu anakuwa chaguo la kwanza moja kwa moja," alisema Lunyamila.
Staa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Said Maulidi 'SMG' alisema: "Depu ni mshambuliaji anayesimama katika nafasi yake, ana nguvu na fundi wa vipimo katika kufunga mabao na tayari kaonyesha ana kitu."
MWENYEWE ANASEMAJE?
Depu amewahi kuzungumzia matarajio yake ndani ya Yanga alipozungumza na Mwanaspoti Januari 19, 2026 akisema anatamani kufanya makubwa zaidi akiwa na timu hiyo na mwanzo wake mzuri ni hatua ya kwanza tu ya safari ndefu aliyojipanga kuifanya klabuni hapo.
"Huu ni mwanzo tu, nina malengo makubwa na Yanga, ni timu sahihi kunisaidia kuyafikia.
"Kila siku najifunza kitu kipya, mazingira ni mazuri na hilo linanifanya nijisikie huru," alisema mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26.
Kuhusu matarajio yake binafsi, Depu alisema anataka kuona Yanga inashinda mataji kadiri iwezekanavyo huku akisisitiza: "Mabao na asisti ni kazi yangu, lakini kikubwa ni mafanikio ya timu."
MECHI ZAKE
Yanga 6-0 Mashujaa (dk 35, amefunga bao moja na kuasisti moja)
Yanga 3-1 Dodoma Jiji (dk 90, amefunga mabao mawili, hakuasisti)
Al Ahly 2-0 Yanga (dk 90, hakufunga wala kuasisti)
Yanga 1-1 Al Ahly (dk 73, hakufunga wala kuasisti)
AS FAR Rabat 1-0 Yanga (dk 67, hakufunga wala kuasisti)
Yanga 3-0 JS Kabylie (dk 87, amefunga mabao mawili, hakuasisti)
TAKWIMU ZA DEPU
MECHI: 6 (Ligi Kuu 2, CAF 4)
MABAO: 5 (Ligi Kuu 3, CAF 2)
ASISTI: 1 (Ligi Kuu)
DAKIKA: 442 (Ligi Kuu 125, CAF 317)