Prime
Kilichoziangusha Simba, Yanga hiki hapa
WAKATI droo ya hatua ya robo fainali ya michuano ya CAF kwa msimu wa 2025-2026 ikifanyika leo, furaha ya mashabiki wa soka nchini miezi kama minne baada ya Tanzania kuingia timu nne hatua ya makundi ya michuano ya kimataifa, imemalizika kwa huzuni.
Hii ni baada ya timu za Simba, Yanga, Azama FC na Singida Black Stars zilizoiheshima nchi kwa kutinga makundi mwisho mwa Oktoba mwaka jana na kuanza kasi ya kusaka tiketi ya kwenda robo fainali Novemba hadi juzi Jumapili kuchemsha kama utani.
Timu hizo zimekwamia makundi na kutolewa michuanoni zikiwa makundi, tofauti na matarajio ya wadau wengi wa soka nchini kwa msimu huu wa Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika 2025-2026.
Yanga na Simba zilizokuwa zinashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, zimejikuta zote zikishindwa kufuzu hatua ya robo fainali, sambamba na ilivyokuwa kwa Azam FC na Singida bS zilizowakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika .
Kutolewa kwa wawakilishi wote katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, ni pigo kubwa kutokana na matarajio ya wadau wengi wa soka, ingawa zipo sababu zilizochangia kama Mwanaspoti linavyoelezea kwa kina.
YANGA
Licha ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JS Kabylie ya Algeria katika mechi ya mwisho ya Kundi B iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar, ila timu hiyo ilishindwa kusonga mbele ikiwa ni msimu wa pili mfululizo.
Yanga ilikuwa inahitaji ushindi wa zaidi ya mabao 3-0, kama huo ilioupata, ingawa hesabu za kikosi hicho cha kufuzu robo fainali zilififia baada ya AS FAR Rabat ya Morocco kutoka suluhu ugenini dhidi ya Al Ahly ya Misri.
Suluhu hiyo kwa AS FAR, iliifanya ifikishe pointi tisa na kumaliza ya pili ikiungana na Al Ahly iliyoongoza na pointi 10, huku Yanga ikimaliza ya tatu na pointi nane, wakati JS Kabylie imeburuza mkiani na pointi tatu tu.
Kutolewa kwa Yanga ni mwendelezo mbaya kwa timu hiyo kwa msimu wa pili mfululizo katika michuano ya CAF, baada ya msimu wa 2024-2025 kushindwa kufuzu hatua ya robo fainali, ikimaliza ya tatu kundi A na pointi nane kama ilivyo msimu huu.
Msimu uliopita, Yanga ilihitaji ushindi wa aina yoyote katika mechi ya mwisho ya makundi ili ifuzu robo fainali, lakini ikaishia kutoka suluhu na MC Alger ya Algeria na kuishia hapo, huku MC Alger na Al Hilal iliyoongoza kundi na pointi 10 zikisonga mbele. TP Mazembe ya DR Congo ikiburuza mkia na pointi tano ktika kundi hilo.
Msimu huu wa 2025-2026, Yanga ilifeli mapema kuchanga vyema karata zake baada ya sare ya bao 1-1 mbele ya Al Ahly ikiwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar, Januari 31, 2026, kutokana na kushindwa kutumia nafasi nyingi za kufunga.
Moja ya changamoto iliyoigharimu Yanga, ni kukosa umakini wa washambuliaji wa timu hiyo, wakiongozwa na Prince Dube na nyota mpya, Laurindo Dilson Maria 'Depu', aliyefunga mabao mawili na JS Kabylie, ambao hawakutumia vyema nafasi mwanzo.
Mbali na utumiaji wa nafasi kwa washambuliaji, ila eneo la kujilinda ilikuwa ni changamoto nyingine ya timu hiyo, kwani katika mechi sita ilizocheza imeruhusu mabao manne, ikiwa sio dalili nzuri kutokana na malengo makubwa ya kikosi hicho.
SIMBA
Hesabu za Simba za kufuzu hatua ya robo fainali zilianza kufifia tangu mwanzoni mwa msimu huu, baada ya kikosi hicho cha Msimbazi kushindwa kutumia vyema faida za uwanja wa nyumbani, kuanzia mechi za hatua ya awali hadi zile za makundi pia.
Simba iliumaliza mwendo tangu raundi ya nne ya hatua ya makundi ilipotoka sare ya mabao 2-2, nyumbani mbele ya Esperance ya Tunisia, kisha kujitibulia ilipotoka sare nyingine ya bao 1-1, ugenini dhidi ya Petro Atletico ya Angola, February 7, 2026.
Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Stade Malien ya Mali katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi, ulikuwa ni wa kwanza kwa Simba msimu huu ikicheza nyumbani, jambo linaloonyesha wazi kikosi hicho kilitengeneza mazingira magumu tangu mwanzoni.
Simba iliyofika fainali ya Shirikisho msimu uliopita na kupoteza jumla ya mabao 3-1 mbele ya RS Berkane ya Morocco, ni mwaka 2003 tu, iliishia makundi, ila mara zote ilikuwa ikikwamia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na Shirikisho Afrika t1ngu 2018-2019.
Timu hiyo iliyofundishwa na makocha watano tofauti msimu huu, akianza, Fadlu Davids, Hemed Suleiman 'Morocco', Selemani Matola, Dimitar Pantev na sasa Steven Barker, ni ishara nyingine ya anguko kutokana na mabadiliko ya benchi la ufundi.
AZAM FC
Timu hii ya Azam imeaga michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu, baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Wydad Casablanca ya Morocco, katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mohammed V.
Azam inayoshiriki hatua ya makundi ya michuano ya CAF kwa mara ya kwanza katika historia, ilipoteza hesabu kwenye mechi mbili tu za mwanzoni, baada ya kuchapwa mabao 2-0 na AS UnionManiema ya DR Congo, kisha bao 1-0 ilikabiliana na Wydad Casablanca visiwani Zanzibar.
Kupoteza mechi mbili, kuliweka matumaini finyu ya timu hiyo kusonga hatua ya robo fainali, japo kukosa umakini kwa safu ya ushambuliaji inayoongozwa na Mkongomani Jephte Kitambala, kuliigharimu kutokana na nafasi nyingi zilizotengenezwa.
Licha ya kutolewa, ila imeandika rekodi ya kushiriki hatua ya makundi ya michuano ya CAF kwa mara ya kwanza ikiwa kombe la Shirikisho, huku ikipata pointi nyingi ambazo haijawahi kutokea kwa klabu yoyote ya Tanzania katika ushiriki wake wa kwanza.
Azam imemaliza nafasi ya tatu na pointi tisa, ikiwa ni pointi nyingi zaidi kwa timu ya Tanzania katika ushiriki wake wa kwanza, kwani hata vigogo wa soka nchini Yanga, Simba na Namungo ziliposhiriki kwa mara ya kwanza hazijawahi kuzifikia.
Yanga ikicheza makundi kwa mara ya kwanza mwaka 1998 katika Ligi ya Mabingwa ilimaliza ikiwa na pointi nne, huku Simba ikicheza makundi kwa mara ya kwanza mwaka 2003, katika Ligi ya Mabingwa Afrika kama ilivyo Yanga, ilivuna pointi saba.
Hata kwa Yanga iliyorudi pia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa ni ya kwanza kwa Tanzania mwaka 2016, iliburuza mkiani kundi A na pointi nne, nyuma ya TP Mazembe ya DR Congo, MO Bejaia ya Algeria na Medeama SC ya Ghana.
Msimu wa 2020-2021, Namungo ikishiriki kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, iliweka rekodi ya kutoshinda wala kufunga bao au kupata pointi zozote katika mechi sita, huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara tisa.
Katika msimu huo, Namungo ilimaliza mkiani mwa kundi D, bila pointi zozote, nyuma ya vinara, Raja Casablanca ya Morocco iliyokuwa na 18, ikifuatiwa na Pyramids ya Misri yenye 12, huku Nkana ya Zambia ikimaliza ya tatu na pointi zake sita.
SINGIDA BLACK STARS
Singida inayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo, imehitimisha hatua ya makundi ikiwa mkiani na pointi tano kundi C, ambazo ni sawa na za Stellenbosch ya Afrika Kusini, iliyomaliza ya tatu.
CR Belouizdad ya Algeria inayonolewa na aliyekuwa Kocha wa Yanga, Sead Ramovic, imeongoza kundi C ikiwa na pointi 15, ikifuatiwa na AS Otoho D'Oyo ya Congo Brazzaville yenye pointi tisa, ambazo timu zote tayari zimeshafuzu robo fainali.
Hesabu za Singida hazitofautiani sana na wawakilishi wengine wa Tanzania, kwani baada ya kuchapwa mechi ya kwanza mabao 2-0, dhidi ya CR Belouizdad, ilitakiwa itumie vyema uwanja wa nyumbani, jambo ambalo hata hivyo, ilishindwa kulitumia.
Mechi ya pili ikicheza nyumbani, Singida ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Stellenbosch ya Afrika Kusini, ingawa kichapo kingine cha bao 1-0, mbele ya CR Belouizdad, kilitibua hesabu kabisa za timu hiyo kusonga hatua ya robo fainali.
Kwa Singida kupata pointi nne kati ya tisa ilizotakiwa kuzipata ikiwa kwenye uwanja wa nyumbani, ilikuwa ni hesabu ngumu kwa timu hiyo, hasa kutokana na kutokuwa pia na mwenendo mzuri hasa inapocheza mechi za ugenini katika mashindano hayo.
Azam na Singida ambazo zimefika hatua hii kwa mara ya kwanza katika historia, zina kitu kikubwa cha kujifunza ambacho msimu ujao zinaweza kufika mbali zaidi, ingawa kwa Yanga na Simba haina ubishi miamba hiyo ya soka hapa nchini imefeli.
TIMU ZILIZOFUZU
Kutolewa kwa timu za Tanzania iliyokuwa moja ya nchi nne zilizokuwa zimeingia timu nne sambamba na Misri, Algeria na Morocco, imeziacha jumla ya timu 16 zikitinga hatua hiyo kuopitia michuano y Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho zikisubiri droo leo kujua zitacheza na nani.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika Misri na Morocco zimeingiza timu zote mbili za Al Ahly na Pyramids kwa (Misri), huku Morocco ikiwa na AS FAR Rabat na RS Berkane, ilihali timu nyingine ni Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Al Hilal ya Sudan, Esperance ya Tunisia na Stade Malien ya Mali.
Kwa Kombe la Shirikisho Misri imeingiza pia timu mbili za Al Masri na Zamalek, Morocco nao imeingiza mbili Olmpique de Safi na Wydad Casablanca, ilihali Algeria ina timu mbili za USM Alger na CR Belouizdad.
Nyingine ni Otoho d'Oyo ya Congo Brazzaville na AS Maniema ya DR Congo naa mechi za mkondo wa kwanza kwa hatua hiyo ya Robo zitapigwa kati ya Machi 13-14 na marudiano ikiwa ni Machi 20-21 na washindi wataenda nusu fainali kusaka tiketi za kucheza fainali katikati ya mwaka huu.
1974 Mwaka ambao SImba iliweka rekodi ya kucheza nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika.
08 Kwa misimu minne mfululizo, Yanga inakusanya pointi nane katika haatua ya makundi ya CAF
05 Pointi ilizovuna Simba katika Ligi ya Mabingwa zikiwa ni pointi chache kwa makundi kwao.