Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dieng alivyoanzisha safari ya Yanga kutofuzu robo fainali CAF

HISIA Pict


NA saa chache baadaye Yanga walimfuata Simba kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika. Mechi yao ilichezwa katika uwanja ambao wameupachika jina la Guantanamo Bay. Kwamba ni ngumu kutoka ukiingia anga za Yanga pale Uwanja wa New Amaan.


Ni kweli JS Kabylie hawakutoka salama katika Uwanja wa Amaan. Yanga walifanya kila kitu sahihi. Kila kitu katika kipimo chake. Waarabu walikufa mabao 3-0. Hawakuwa na majibu kwa mashambulizi ya mara kwa mara ya Yanga. Walifungwa kihalali na ilitegemewa wafungwe idadi hiyo ya mabao ili Yanga wabaki na sala tu ya kuona bao lolote la Al Ahly dhidi ya Far Rabat pale Misri.


Mshambuliaji anayeitwa Depu alifunga mabao mawili. Chadrack Boka akicheza kwa pamoja na Mohamed Hussein Tshabalala kwa mara ya kwanza naye akafunga bao lake la kwanza katika jezi ya Yanga. Yanga walifanya kile ambacho walikiahidi kwa mashabiki wao mara nyingi kupitia kwa msemaji wao Ali Kamwe.

Yanga inapofunga mabao mawili mengine katika pambano la kimataifa huku Pacome Zouzoua akiwa nje ya uwanja, ilitoa ishara kwamba walikuwa na jambo lao na ilikuwa lazima walitimize. Tatizo lilikuwa mechi ya Cairo. Basi. Hakukuwa na tatizo jingine la msingi zaidi ya Al Ahly kushindwa kuweka mpira katika nyavu za Far Rabat katika pambano ambalo walilitawala kwa muda mrefu.

Yanga wakaishia kuoga, lakini mjini hawakwenda. Zamani pointi nane zilikuwa kama ndoto kwa timu za Tanzania. Sasa hivi kumbe unaweza kuzifikisha na bado usiende hatua ya robo ya fainali. Ndicho ambacho kimewatokea Yanga. Pointi moja tu imewakosesha nafasi ya kusonga mbele. Kuna jambo ambalo wanapaswa kujifunza.

Mwandishi anayeitwa Ben Mtobwa katika kitabu chake cha ‘Tutarudi na roho zetu?’ Aliwahi kuandika kwamba kila dakika inayokuweka hai jaribu kuinunua kwa kiasi chochote cha pesa. Kuna mahala Yanga watatazama nyuma na kugundua kwamba kuna mechi ambazo walipaswa kukaza zaidi. Watagundua kwamba kila dakika ambayo walikuwa katika michuano walipaswa kuinunua kwa gharama yoyote.

Nje ya pambano hili Yanga walipaswa kushinda pambano dhidi ya Al Ahly. Hauwezi kuwalaumu sana kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Far Rabat. Hapana. Katika mechi ile walizidiwa kwa kila idara. Ambacho Yanga wanapaswa kujutia zaidi ni kuruhusu bao la Aliou Dieng wa Al Ahly walipokutana pale Unguja.

HISI 01

Jina la utani la Guantanamo Bay lingetimia kama Yanga ingeondoka na pointi zote tisa nyumbani. Unapoondoka na pointi zote tisa nyumbani kisha ukatoka sare moja ugenini ina maana tayari una pointi kumi. Ngumu sana kufikisha pointi kumi na usifuzu hatua inayofuata. Yanga ilipaswa kutodondosha alama yoyote nyumbani.

Katika siku ambayo Al Ahly haikuwa katika ubora, Dieng alikuja kusawazisha bao la kipindi cha kwanza la Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na Yanga waliona kawaida tu kwa sababu walidhani wangeambulia pointi kule Rabat. Kama wangekaza zaidi katika kipindi cha pili cha pambano lile hadithi ingeweza kuwa tofauti.

Katika ubora wao TP Mazembe ya kina Mbwana Samatta ilikuwa inafanya hivyo. Na wala hatuhitaji kutoa mifano ya mbali. Katika ubora wao, Mnyama pia alikuwa hafanyi kosa katika uwanja wa nyumbani pale kwa Mkapa. Na ndio maana wenyewe walikuwa wanasema “kwa Mkapa hatoki mtu”. Kunusurika kwa Al Ahly baada ya bao la Dieng kuliiweka Yanga katika mazingira magumu.

Nini kinafuata? Watani wao wanawacheka. Katikati ya giza zito ambalo limetanda Msimbazi hatimaye mtani amepata njia ya kujifariji kupitia matokeo ya Yanga. Kupitia kwa Yanga kufeli kwenda robo fainali mtani amejikuta akisahau matatizo yake ya kutaka Mohamed Dewji au Murtaza Mangungu mmoja wao aachie timu. Ni jambo la kawaida. Hata kuna nyakati ambazo Yanga alikuwa anajiliwaza kwa vipigo vya Simba mechi za kimataifa. Sio jambo la kushangaza sana.

HISI 02

Kitu cha muhimu baada ya kila kicheko ambacho Yanga wamechemka na mtani ni kwa mtani kujikumbusha kwamba bado kuna pengo kati yake na Yanga. Yanga wametolewa kiume katika michuano na kitu kikubwa kilichowaangusha ni Al Ahly kutopata bao lolote dhidi ya Far Rabat kitu ambacho ni nadra kwa Al Ahly anapokuwa uwanja wa nyumbani. Waarabu hawakuachiana mechi hiyo ya Cairo. Ni vile tu nyavu za Far Rabat ziligoma.

Mtani ajikumbushe kwamba wakati yeye akimalizia pambano la mwisho dhidi ya Stade Mallen ambaye alikuwa na uhakika na nafasi ya kwanza katika kundi, Yanga alikuwa anasaka mabao matatu dhidi ya Waarabu katika pambano la machozi, jasho na damu, na bado alifanikiwa kupata mabao hayo. Wakati mwingine unapaswa kumcheka jirani huku ukijikumbusha utajiri wake.

Mahala pekee ambapo Simba wana haki ya kuwacheka Yanga ni kwamba wao wakiwa katika ubora wao walikuwa na mwendelezo wa ubora katika michuano hii kwa maana ya kufika robo fainali mara kwa mara.

HISI 03

Yanga wana kitu cha kujifunza kutoka kwa mtani kwamba unapotawala soka la ndani bado unapaswa kutawala soka la Afrika walau kwa kufika robo fainali mara kwa mara.

Nini kinafuata? Timu zote za Tanzania hazijaenda robo fainalj ya michuano hii. Bado kuna safari ndefu ya kuwafikia Waarabu wa Misri, Tunisia, Morocco na Algeria. Kuna namna kuna pengo la kiuchezaji limepungua lakini bado hatujaweza kufanya kitu kinachoitwa shifting of power. Bado hatujaweza kufanya kitu ambacho TP Mazembe na Mamelodi Sundowns wamefanya katika miaka 20 iliyopita.

Bado hatujaweza kumtoa bingwa wa Afrika au shirikisho nje ya Afrika Kaskazini. Fikiria namna ambavyo Mazembe na Mamelodi waliwahi kufanya hivyo. Na kwa sasa hata michuano hii inayoendelea kuna dalili kubwa bingwa wa Ligi ya mabingwa na Shirikisho wakatoka kwa Waarabu wa Kaskazini.

Hii ina maana Simba, Yanga, Azam, na Singida wanapaswa kuendelea kutia hela katika mipango yao ya kusaka walau nusu fainali ya ligi ya mabingwa au ubingwa wa Shirikisho.

Naambiwa kwamba michuano ya Shirikisho imefutwa. Walau michuano hii tuliwahi kufika fainali. Wakubwa wetu wanahitajj kuongeza nguvu katika maeneo mengi kuweza kufikia mahala ambapo wenzetu wapo.

HISI 04

Mpaka sasa hatupo pabaya sana. Mfano mzuri ni pointi ambazo Yanga wametolewa nazo. Zamani akina Edibily Jonas Lunyamila na Mohamed Hussein Mmachinga walikuwa hawawezi kuzifikia lakini siku hizi tunazifikia na bahati mbaya timu inashindwa kufuzu. Ni suala la kutia nguvu zaidi na zaidi na kutazama wapi ambapo huwa tumekosea.

Mwisho wa siku nina dokezo tu la kawaida ambalo halina umuhimu sana. Baada ya Yanga na Simba kuchekana sasa wana nafasi nzuri ya kumaliza ubishi pale Unguja. Wana mechi yao ya ligi kuu ambayo kwa kiasi fulani itamaliza ubishi kuhusu wao. Itamaliza ubishi kuhusu nani alitolewa kwa bahati mbaya katika michuano hii

Wakati Yanga wakilaani bahati mbaya ya kutopita katika kundi licha ya kuwa na pointi nane, Simba wanataka kuwaonyesha Yanga kwamba walikuwa na bahati mbaya kutowapata kina Oura mwanzoni mwa msimu huu.

Itakuwa mechi nzuri na ya kusisimua mwanzoni mwa Machi kila mmoja akijaribu kuonyesha kwamba alitolewa katika michuano hii kwa bahati mbaya. Tukutane Unguja.