Prime
Kilichoinyima Simba ubingwa Ligi Kuu hiki hapa! Mangungu afunguka
Muktasari:
- Kwa sehemu kubwa ya msimu, Wekundu wa Msimbazi waliendelea kuwa ndani ya mbio za ubingwa wa Ligi kuu ya NBC na kufikisha ushindani huo hadi mechi za mwisho.
SIMBA SC iliingia msimu wa 2025-2026 ikiwa na dhamira ya kushinda taji kubwa la mashindano ya ndani baada ya kufanya maandalizi makubwa na kuwekeza kwenye kikosi chenye mchanganyiko wa uzoefu na vipaji vya vijana.
Kwa sehemu kubwa ya msimu, Wekundu wa Msimbazi waliendelea kuwa ndani ya mbio za ubingwa wa Ligi kuu ya NBC na kufikisha ushindani huo hadi mechi za mwisho.
Hata hivyo, walishindwa kuvuka mstari wa mwisho mbele ya watani wao wa jadi, Yanga SC.
Ingawa mara nyingi lawama huangukia kwenye mechi moja au mbili, ukweli ni kwamba ubingwa wa Simba haukupotea katika dakika 90 za mchezo mmoja. Ulipotea taratibu kupitia mfululizo wa sare zisizotarajiwa, kupoteza alama dhidi ya wapinzani wa moja kwa moja, kushindwa kuzifunga timu zilizokuwa chini ya kiwango chao, pamoja na mabadiliko ya mara kwa mara kwa benchi la ufundi.
Tofauti kati ya Simba na Yanga haikuwa kubwa kiuchezaji, bali ilikuwa kwenye uwezo wa kutumia kila nafasi ya kukusanya pointi. Wakati Yanga ilionyesha uthabiti wa kushinda hata inapocheza chini ya kiwango chake, Simba mara kadhaa ilishindwa kugeuza ubora wake kuwa ushindi. Mwisho wa msimu, tofauti hiyo ndogo ndiyo iliyotengeneza bingwa kwa Yanga ikiuchukua mara ya tano mfululizo.
Tofauti ya pointi mbili ilizitenganisha timu hizo, Yanga ilikusanya pointi 75, Simba ikaishia 72 baada ya kila moja kucheza mechi 30.
Kukosa kwao taji la ligi, Simba ikajifuta machozi ikitwaa Kombe la Shirikisho la CRDB ikiichapa Azam, kabla ya hapo ilishinda Kombe la Muungano kwa kuifunga Yanga.
Hapa kuna uchambuzi wa mambo kadhaa yaliyoiyumbisha Simba kiasi cha kushindwa kufikia malengo makubwa ya kubeba taji la ligi ambalo limechukuliwa tena na Yanga kwa msimu wa tano mfululizo.
DABI YA KARIAKOO
Hakuna mechi yenye uzito mkubwa katika Ligi Kuu ya NBC kama Dabi ya Kariakoo. Simba ilijua wazi kuwa ushindi dhidi ya Yanga ungekuwa na faida ya alama na kuongeza morali kwenye mbio za ubingwa.
Katika mchezo wa kwanza, mechi ilimalizika kwa matokeo ya 0-0, Yanga ikiwa mwenyeji. Matokeo hayo yalikuwa ya kawaida kwa timu mbili zilizocheza kwa tahadhari kubwa, lakini yalipunguza nafasi ya Simba kupata faida dhidi ya mpinzani wake mkuu.
Mchezo wa marudiano ndiyo ulioumiza zaidi. Simba ilianza kwa kasi na kuonyesha ubora mkubwa, ikiongoza kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Libasse Gueye na Clatous Chama. Katika mazingira ya kawaida, huo ulikuwa ushindi ambao ungeipa Simba alama tatu muhimu na kuipa nguvu kubwa kwenye mbio za ubingwa.
Badala yake, Yanga ilionyesha uimara wa kisaikolojia na kurejea mchezoni kupitia mabao ya Prince Dube na Bakari Mwamnyeto, na kufanya mchezo kumalizika kwa sare ya 2-2.
Kwa jumla, Simba ilikusanya alama mbili pekee kati ya sita dhidi ya Yanga. Ingawa Yanga nayo haikupata ushindi, uwezo wake wa kurejea kwenye mchezo uliifanya ibaki na faida kubwa ya kisaikolojia na kudhibiti mbio za ubingwa.
AZAM MWIBA MCHUNGU
Mbali na Yanga, Azam ndiyo timu iliyoigharimu Simba pointi nyingi zaidi.
Katika mzunguko wa kwanza, Simba ilifungwa mabao 2-0 dhidi ya Azam, matokeo ambayo yalionyesha udhaifu wa timu dhidi ya wapinzani wenye uwezo wa kushambulia kwa kasi. Mchezo wa marudiano uliomalizika kwa sare ya 0-0 uliendeleza rekodi mbaya ya Simba dhidi ya Azam ambayo nayo inaingia kwenye timu shindani za kuwania ubingwa.
Matokeo hayo yaliifanya Simba kupata alama moja tu kati ya sita zilizokuwa zinapatikana.
Katika mbio za ubingwa, kupoteza pointi tano dhidi ya mpinzani wa juu ni tatizo kubwa. Huku Simba ikikwama mbele ya Azam, Yanga iliendelea kutumia nafasi hizo kujijengea pengo la alama ambalo baadaye lilikuwa gumu kufutwa. Kumbuka Yanga ilikusanya pointi nne dhidi ya Azam, ikianza na matokeo ya 0-0, kisha ushindi wa 3-0.
KUPOTEZA UMAKINI
Licha ya matokeo dhidi ya Yanga na Azam, ukweli ni kwamba ubingwa ulipotea zaidi kwenye mechi dhidi ya timu zilizokuwa katikati na chini ya msimamo.
Simba ilitoka sare dhidi ya Dodoma Jiji, Pamba Jiji na TRA United. Hizi zilikuwa mechi ambazo kwa hesabu za ubingwa zilipaswa kuleta alama zote tatu.
Tofauti ya mabingwa na washindani mara nyingi huonekana kwenye uwezo wa kushinda mechi kama hizi. Mfano sare dhidi ya Pamba Jiji, Simba ilipoteza umakini na kujikuta wapinzani wao wakitoka nyuma na kusawazisha.
Yanga ilifanya hivyo. Iliwafunga wapinzani waliokuwa chini yake na kukusanya pointi bila kuyumba. Simba ilipoacha alama, Yanga ilizichukua. Hapo ndipo pengo la alama lilipoanza kujengeka na baadaye kuwa gumu kufikiwa.
Kwa mtazamo wa takwimu, pointi zilizopotea dhidi ya Dodoma Jiji, Pamba Jiji na TRA United zilikuwa na thamani kubwa kuliko hata sare za Dabi ya Kariakoo.
Hata hivyo, Yanga nayo haikuchukua pointi zote kwa Dodoma Jiji ikiambulia tatu kutokana na mechi moja kufungwa, nyingine kushinda, huku dhidi ya TRA United, ikiambulia pointi nne, ilishinda moja, nyingine sare. Kwa Pamba Jiji, ndipo ilikusanya pointi zote sita jambo ambalo Simba ilishindwa kutokana na kuambulia nne.
UKAME WA MABAO
Tatizo lingine lililojitokeza mara kwa mara lilikuwa ukosefu wa umaliziaji mzuri.
Katika michezo mingi Simba ilitengeneza nafasi nyingi lakini ikashindwa kuzitumia. Sare za 0-0 dhidi ya Yanga, Azam na Dodoma Jiji zilidhihirisha changamoto hiyo.
Safu ya ushambuliaji ilikosa mshambuliaji mwenye uwezo wa kutumia nafasi chache na kubadili matokeo ya mchezo. Katika baadhi ya mechi, Simba ilitawala umiliki wa mpira na kutengeneza nafasi nyingi kuliko wapinzani wake, lakini ilikosa bao ambalo lingebadilisha mchezo.
Hilo limejidhihirisha katika takwimu ambapo Simba imemaliza na mabao 54, wakati Yanga ikifunga 71.
MABADILIKO BENCHI LA UFUNDI
Msimu ulianza bila utulivu wa kutosha kwenye benchi la ufundi la Simba, hata Yanga hali ilikuwa hivyo, lakini kidogo kulikuwa na utofauti.
Msimu ulianza na kocha Fadlu Davids, ghafla akaondoka, msala ukabaki kwa kocha msaidizi Seleman Matola, akaletwa Hemed Suleiman Morocco kwa muda, kisha akaajiriwa Dimitar Pantev, alipoondoka, Steve Barker akashika usukani hadi mwisho wa msimu.
Mabadiliko hayo ya makocha watano ambao walikaa kwenye benchi la ufundi la Simba, kwa kiasi fulani yaliwachanganya wachezaji kimbinu ndani ya uwanja.
Steve Barker alipowasili Desemba 19, 2025, alikuta timu tayari imepoteza alama muhimu.
Pamoja na kuchelewa kuanza kazi, Barker aliweza kubadilisha sura ya Simba. Timu ilianza kucheza kwa kujiamini zaidi, ikawa na nidhamu ya kiuchezaji na kurejesha ushindani wake. Si ajabu alitwaa tuzo za Kocha Bora wa Mwezi Februari, Machi na Mei 2026.
Hata hivyo, mafanikio hayo hayakuweza kufuta makosa yaliyokuwa tayari yamefanyika katika mzunguko wa kwanza.
Yanga yenyewe pia ilifanya mabadiliko ya benchi la ufundi, alianza Romain Folz, akaja Pedro Goncalves, akamaliza Abdihamid Moallin aliyewapa taji la ligi.
USAJILI
Dirisha dogo la usajili lilikuwa hatua muhimu ya Simba kuokoa msimu.
Chini ya ushauri wa Steve Barker, klabu ilisajili wachezaji wanane wapya akiwemo Djibrila Kassali, Ismael Toure, Nickson Kibabage, Libasse Gueye, Anicet Oura, Inno Loemba, Clatous Chama na Baraka Mwangosi.
Usajili huo ulionyesha wazi kuwa uongozi ulikubali kulikuwa na upungufu katika kikosi kilichoundwa mwanzoni mwa msimu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Crescentius Magori, Simba ililazimika kuuza baadhi ya wachezaji wake ili kupata fedha za kufanikisha usajili huo.
Wachezaji wapya waliipa timu nguvu mpya, ushindani na ubora mkubwa, lakini walifika wakati ambao sehemu kubwa ya ligi ilikuwa tayari imechezwa. Walihitaji muda wa kuzoea mazingira, mfumo wa kocha na ligi yenye ushindani mkubwa.
Maboresho hayo yangefanyika kabla ya kuanza kwa msimu, huenda picha ya mbio za ubingwa ingekuwa tofauti.
MSIKIE MANGUNGU
Akizungumzia mwenendo wa Simba katika msimu wa 2025-2026 ambao ulitamatika kwa kushinda Kombe la Shirikisho la CRDB, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu, amesema: "Tunashukuru kwamba tumefika mwisho wa ligi na mashindano mengine yote katika msimu huu pamoja na kwa kuchelewa ukilinganisha na baadhi ya maeneo katika ukanda mwingine wa dunia.
"Lakini kwetu sisi tumeweza kufanikiwa kupata mashindano hayo ambayo tumeweza kufanikiwa kufika mwisho na kuwa sisi ni mabingwa au kuwa sisi ni washindi. Mafanikio siwezi kuyaelezea sana kwa sababu mara nyingi unapima mafanikio kulingana na lile ulilolikusudia.
"Sisi makusudio yetu ilikuwa ni kushiriki mashindano yote na kushinda yote. Yale tuliyofanikiwa tunamshukuru Mungu kwamba tumefanikiwa na yale ambayo hatukufanikiwa basi tutakuwa tayari kufanya marekebisho ili tuweze kuwa washindani zaidi katika mashindano yanayofuata."
Kwa ujumla, Simba haikupoteza ubingwa kwa sababu ya mchezo mmoja, mwamuzi mmoja au bahati mbaya. Ilikuwa ni matokeo ya makosa yaliyokusanyika katika kipindi chote cha msimu.
Sare mbili dhidi ya Yanga, matokeo mabaya dhidi ya Azam FC, kupoteza pointi mbele ya timu zilizokuwa chini kwenye msimamo, ukosefu wa makali ya ushambuliaji, mabadiliko ya benchi la ufundi na marekebisho yaliyochelewa ya kikosi, yote yaliunda mazingira yaliyoipa Yanga nafasi ya kutwaa ubingwa.
Pamoja na maumivu ya kukosa taji, Simba imemaliza msimu ikiwa na msingi mzuri wa kujenga kikosi cha ushindani. Endapo itaendelea na utulivu wa benchi la ufundi, kufanya usajili kwa wakati na kuongeza ufanisi mbele ya lango, inaweza kurejea kwa nguvu zaidi katika mbio za ubingwa msimu ujao.
Kwa msimu wa 2025-2026, somo kubwa kwa Simba ni kwamba ubingwa hauamuliwi kwenye mechi kubwa pekee, bali kwenye uwezo wa kukusanya pointi katika kila mchezo. Hapo ndipo Yanga ilifanya vizuri zaidi, na hapo ndipo Simba ilibaki nyuma.