Kibwana Shomari asimulia alivyoiacha solemba Simba

Beki Yanga asimulia alivyoiacha Simba kwenye mataa

Muktasari:

  • Ubora wa Shomari Kapombe ndio unamsukuma Kibwana kujituma na kucheza kwa bidii ili aweze kufikia kiwango cha beki huyo wa Simba na pia aweze kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

WAKATI Yanga ikiachana na beki Juma Abdul, mashabiki wengi wa timu hiyo walikuwa wakijiuliza nani ataweza kuziba pengo la beki huyo maarufu kwa krosi maridadi za mabao.

Hata baada ya klabu hiyo kutangaza kumsajili Kibwana Shomari kutoka Mtibwa Sugar bado mashabiki wengi hawakuwa na imani naye sana.

Hata hivyo, Kibwana ameshawadhihirishia mashabiki kuwa yeye ni mmoja wa mabeki bora wa kulia hapa nchini licha ya umri wake kuwa mdogo.

Ubora wa Shomari Kapombe ndio unamsukuma Kibwana kujituma na kucheza kwa bidii ili aweze kufikia kiwango cha beki huyo wa Simba na pia aweze kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.


Kujiunga Yanga

Kibwana anasema alitumia siku tatu tu kukamilisha dili la kutoka Mtibwa na kujiunga na Yanga alikosaini mkataba wa miaka miwili.

“Kwanza ndoto yangu ilikuwa kucheza nje ya nchi lakini bahati nzuri ndio dili ya kuja Yanga ikaja hivyo nikasajili nikiamini kuwa ni hatua mojawapo ya kunipelekea kule ninapopataka.

“Nakumbuka Simba ndio walianza kunihitaji tangu msimu uliopita lakini nafikiri walishindwa kuvunja mkataba wangu kwani nilikuwa bado nina mkataba wa miaka mitatu na Mtibwa. Kisha Yanga nao wakanihitaji na kuongea na meneja wangu na nafikiri waliafikiana dau na mimi niliambiwa ndani ya siku tatu tu nikapewa mkataba nikasaini,” anasema.

Kibwana anasema anafurahia kuwa Yanga licha ya kwamba maisha ndani ya klabu hiyo ni tofauti na Mtibwa Sugar.

“Kuna tofauti kubwa sana timu hii na ile niliyotoka kwani Mtibwa hakuna presha kama Yanga.Kule hata mkishindwa kupata matokeo mazuri ni kawaida tu lakini hapa ni tofauti kwani ni lazima mfikie malengo ya timu, pia ukichanganya na presha ya mashabiki ndio kabisa inakufanya upambane sana,” anasema Kibwana.

Anaongeza: ”Pia hapa nafurahi kwani nimekutana na wachezaji wengi wa kigeni ambao wananipa changamoto ya kuzidi kujituma na kupambana zaidi ili na mimi siku moja nitoke niende kucheza nchi nyingine.”


Nafasi ndani ya Yanga

Kibwana anasema licha ya kwamba amejiunga na timu hiyo na moja kwa moja kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza, sio kwamba ni bora zaidi ya wengine akiwemo Paul Godfrey ila ni kutokana na uamuzi ya makocha wake, Zlatko Krmpotic (ameshaondoka) na huyu wa sasa Cedric Kaze.

“Nafurahi kuona nimejiunga na timu hii na moja kwa moja nikaingia kikosi cha kwanza ingawa mimi sio kwamba ni bora sana kuliko Paul ila kocha ndio ana uamuzi wa mwisho kuona nani acheze

“Mimi na Paul ni marafiki na tunaishi poa tu tena tunaelekezana vitu vingi kwa sababu wote ni vijana na tunatafuta maisha hivyo hakuna haja ya kuchukiana eti kwasababu mwenzako anacheza na wewe hupati nafasi”, anasema Kibwana.

Kibwana anasema anamudu kucheza nafasi zote za beki za pembeni na hata wingi zote huku pia akiwa vizuri hata katika beki ya kati.

“Beki zote mimi nacheza kwani zamani wakati nipo katika timu ya vijana ya Moro Kids nilikuwa nacheza beki ya kati lakini kocha wangu, Hussein Mau, akaniambia kutokana na kimo changu nikicheza beki ya kulia itapendeza zaidi ndio akanihamisha namba na nikacheza vizuri ndio mpaka sasa nacheza nafasi hii na naifurahia,” anasema Kibwana.


Ubingwa Yanga tu

Kibwana anasema licha ya kwamba msimu huu ushindani wa ligi ni mkubwa kutoka kwa wapinzani wao Simba na Azam lakini ana matumaini ubingwa utatua Yanga kutokana na kuwa na kikosi bora.

“Tuna timu nzuri na bora sana. Kila mchezaji anajua majukumu yaliyomleta ndani ya timu hii na kila mmoja anapambana sana kuhakikisha tunachukua makombe.

“Ligi ngumu na vita ya ubingwa sio rahisi kwani wapinzani wetu Simba, Azam wako vizuri lakini kwa sababu tumnejiwekea malengo msimu huu kuwa lazima ubingwa utue Jangwani na hilo litatimia,” anasema Kibwana.


Kaze bonge la Kocha

Kocha Mrundi, Cedric Kaze alitua nchini Oktoba 15 mwaka huu na kuanza kibarua cha kuinoa Yanga na sasa ametimiza mwezi tu tangu ajiunge na timu hiyo lakini Kib-wana anakiri jamaa ni bonge moja la kocha.

Kibwana anasema licha ya kwamba kocha huyo amewafundisha kwa muda mfupi lakini ana madini ya maana ambayo ana uhakika kama wachezaji watayatumia vizuri basi hakuna wa kuizuia timu hiyo kutwaa ubingwa msimu huu.

“Ni kocha mzuri sana anajua kuishi na wachezaji na kuwatengeneza ili timu ipate matokeo mazuri.

“Yuko poa sana nje ya uwanja lakini ni mkali kidogo pale mambo yanapokuwa hayaendi jinsi anavyotaka. Ana mbinu na ufundi mwingi wa kufundisha wachezaji utakaoipa Yanga ubingwa kama kila mmoja ataufuata,” anasema Kibwana.

Beki wa kulia katika timu ya Yanga Kibwana Shomari.

Kapombe ni kioo chake

Kibwana anasema mchezaji anayemkubali sana kwenye Ligi Kuu Bara ni Shomari Kapombe wa Simba na amekua akimuangalia kama kioo chake cha kufikia mafanikio.

“Kapombe ni bonge la mchezaji ambaye anaitendea haki nafasi yake uwanjani lakini pia ni mzungu wa roho, hana baya. Wakati tukiwa wadogo yeye alikuwa Moro Kids ya wakubwa na alikuwa akija kutufundisha.

“Nimekuwa namfutilia na nikimuangalia anachofanya na kuiga mazuri yake ambayo yananisaidia na yataendelea kunisaidia kufikia ndoto zangu,” anasema Kibwana ambaye pia anamkubali sana beki wa zamani wa Barcelona, Dani Alves.


DABI YA KARIAKOO

Kibwana anakiri kuwa mechi ya Simba na Yanga ambayo ilikuwa ndio mechi yake ya kwanza kubwa kucheza msimu huu ilimtoa jasho.

“Ujue mechi ya Simba na Yanga ni tofauti na mechi nyingine zote kwa sababu inakuwa na presha sana sio kwa wachezaji tu bali hata kwa mashabiki.

“Ile siku ya mechi nilikuwa naogopa sana, niliwaza sijui itakuwaje na wale mashabiki, yaani bila kocha kunikalisha chini na kunijenga kisaikolojia nahisi ningetoka mchezoni mapema sana.

“Upande wangu kulikuwa na Luis Miquissone ‘Konde Boy’, bwana wee ana balaa yule mtu kwa sababu kwanza ana kasi na hatulii sehemu moja, hivyo nilichoamua ni kumsoma kwanza na kutuliza akili hivyo nilifanikiwa kwa kiasi chake kumdhibiti,” anasema Kibwana mwenye miaka 20 kuhusu winga huyo wa Msumbiji ambaye pamoja na Clatous Chama walikosolewa kwa kupotea mchezo siku hiyo ya Dabi ya Kariakoo.


Wachezaji hawa ndio wanamtoa jasho

Kibwana hakusita kukiri kuwa licha ya kukutana na wachezaji wengi uwanjani katika nafasi yake ya beki ya kulia lakini hakuna wachezaji wanaompa tabu akikutana nao kama Salum Kihimbwa, Haruna Chanongo,Ismail Aidan (wote wa Mtibwa Sugar) na Tuisila Kisinda wa Yanga.

“Kihimbwa anajua kukaa na mpira na ni ngumu kuchukua kirahisi mpira mguuni kwake lakini pia ana kasi, Chanongo yeye ana kasi sana wakati Ismail ni msumbufu, hatulii uwanjani.

“Kwa upande wa Tuisila ambaye huwa tunapambana mazoezini yeye ana kasi sana yule jamaa hivyo lazima umkabe kwa akili, bila hivyo kazi utakuwa nayo,” anasema Kibwana, ambaye bao lake la kusawazisha dhidi ya Yanga kwenye Kombe la Mapinduzi huenda limechangia kupata dili Jangwani.

____________________________________________________________________

Na OLIVER ALBERT