KESSY: Miaka 12 na Asha Mwalala ni raha tu

Katika sehemu iliyopita ya makala hii, beki wa kulia wa KMC, Hassan Kessy aliyewahi kukipiga Simba, Yanga, Mtibwa na Nkana Red Devils ya Zambia pamoja na Taifa Stars kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019, alifunguka mengi ikiwamo kufanya mazoezi na Yanga nchini Uturuki huku akiwa bado ni mchezaji wa Simba na jinsi alivyougua kifua kikuu mwaka na nusu. Twende pamoja…
BAADA ya kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu akijiuguza Kessy, alipopona alienda kwa uongozi wa Mtibwa kuomba wamsajili tena sababu mkataba wake ulishaisha, wakampima na walipoona ni mzima wakampa mkataba wa miaka miwili.
Anasema aliposaini dili hilo hakutaka kupoteza nafasi aliyoipata, alionyesha kiwango cha hali ya juu na ndani ya miezi sita tu alishazishawishi klabu nyingine kuhitaji huduma yake.
“Nilicheza mechi 15 za ligi na mbili za Kombe la FA (Shirikisho) uwezo niliounyesha kwenye michezo hiyo ndio ilifungua milango ya mimi kutoka Mtibwa Sugar na kuingia Simba,” anasema na kuongeza;
“Simba walifanya mpango wa kuongea na uongozi na kununua mkataba wangu uliobaki kwa Sh25 milioni na ndio safari yangu ya kucheza Simba ilianzia hapo na kisha ndio nikatua Yanga.”
JUMA ABDUL NOMA
Pamoja na kusajiliwa kwa shangwe na tafrani kutoka kwa watani wao Simba, Kessy anasema haikuwa rahisi kwake kuingia kikosi cha kwanza moja kwa moja kwani alikutana na Juma Abdul ambaye alikuwa imara zaidi na anakubalika na kocha aliyekuwepo.
“Nilikaa benchi nusu msimu nikingalia wenzangu wakicheza huku nikiwa nimetoka kucheza Simba kikosi cha kwanza sikuweza kupata nafasi hadi nilipoomba kupewa muda kwenye Kombe la Mapinduzi,” anasema na kuongeza;
“Nilionyesha uwezo mkubwa Mapinduzi nikitarajia nitapata nafasi tukirudi Ligi Kuu haikuwa hivyo hadi Juma alipoumia. Nakumbuka ulikuwa mchezo dhidi ya Mbao tulicheza CCM Kirumba Mwanza ndio nikaanza kuchezea Yanga kikosi cha kwanza.”
OKWI KIBOKO
Ni mastraika wengi wazuri kutoka nje wamecheza Tanzania kwa mafanikio kuna Amisi Tambwe, Kipre Tchetche, Emmanuel Okwi na wengine wengi Kessy amesema kati ya hao kwake mshambuliaji aliyemsumbua zaidi ni mmoja.
“Okwi ni mshambuliaji bora kuwahi kutokea kwa wachezaji wa kigeni, ulikuwa hutakiwi kumpa nafasi kwa kumpa mgongo hata dakika moja akigeuka tu anakufunga alikuwa ana kasi na akili ya mpira, kwangu ndiye bora,” anasema Kessy ambaye alipotoka yanga alitua Nkana ya Zambia.
UZITO WAMNYIMA NAMBA
Alipoondoka Nkana baada ya mkataba wake wa miaka miwili kumalizika na mazungumzo ya kuongeza mkataba kutokamilika kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo janga la Covid 19, Kessy anasema aliongezeka kilo nyingi.
“Nilinenepa sana kwani kipindi hicho hadi ligi ya Tanzania ilikuwa imesimama kupisha ugonjwa huo hivyo nilinenepa sana nilikuwa na kilo 70 ambazo zilininyima kabisa namba kikosini kutokana na uzito,” anasema na kuongeza;
“Namshukuru Mungu sasa nimepunguza kilo 10 nina 60. Kwa sasa sichezi kwasababu nimekutana na wachezaji wazuri na wameingia kwenye mfumo wa mwalimu, lakini bado naamini nafasi yangu ipo na nitafanya vizuri tofauti na watu wanavyozungumza kuhusu kushuka kiwango, mimi ni bora.”
OLABA AMBADILI NAMBA
“Nakumbuka nilikuwa nacheza winga katika wingi zote mbili lakini msimu wa 2012 chini ya kocha Tom Olaba ndio nilibadilishwa namba kutoka winga hadi beki sababu ilikuwa ni kasi, aliona naweza kupanda kutengeneza mashambulizi na kurudi kukaba,” anasema na kuongeza: N”ilikuwa napenda sana kucheza winga lakini sasa kutokana na uzoefu nafurahia kucheza nafasi ya beki japo naweza kucheza nafasi zote kikubwa ni kuaminiwa tu.”
WALIZALIWA MAPACHA
Rukia, mama mzazi wa mchezaji huyo anafunguka kuwa alimzaa Kessy akiwa pacha na ndugu yake lakini bahati mbaya mwenzie alitangulia mbele za haki.
“Nikiwa na mzee Kessy baada ya mapacha hao nilibahatika kupata mtoto mwingne wa kiume Omary, sasa amehitimu elimu yake ya sekondari kidato cha nne na yeye ameamua kujihusisha na soka anacheza timu ya KMC ya vijana,” anasema mama huyo ambaye alitengana na mzazi mwenzake.
STRESS MBAYA
“Mwanangu akipunguza hasira na mawazo atafika mbali, namuamini na naamini kudra za Mwenyezi Mungu atatoka na kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania kama ndoto zale za mpira zilivyo, namuombea atafikia malengo,” anasema mama Rukia.
MIAKA 12 NA ASHA MWALALA
Kessy anasema mapenzi yake na nyota wa timu ya soka la wanawake ya Yanga Princess, Asha Mwalala yana zaidi ya miaka 12 na wamedumu kwa muda huo kutokana na kuyafanya ya siri na sio ya wazi kama wengine wanavyofanya kutokana na umaarufu wao.
“Mimi nilikuwa sipendi uhusiano wangu uwe wa wazi, nilikuwa nafahamu changamoto ambazo zingeweza kutokea kwani kuna kutenganishwa na marafiki pia kuibiana, si unajua wachezaji buana,” anasema na kuongeza;
“Miaka 10 yalikuwa ni mapenzi ya kuibana, ndoa tumefunga mwaka jana mwezi wa nane baada ya kutoka Nkana FC kwa changamoto ya Corona, niliporudi tulikaa miezi michache na kufanya uamuzi wa kufunga ndoa.”
Kessy anaweka wazi kuwa pamoja na kudumu kwenye uhusiano huo kwa muda mrefu hawajabahatika kupata mtoto huku akisisitiza kuwa ni mipango ya Mungu.