Kaburu autaja ufalme wa Chama Simba SC

UKIKUTANA na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ atakufunza jambo litakalokupa ujasiri wa kutoogopa changamoto za maisha ambazo zinachangiwa na mwanadamu kutoijua kesho yake.

Anakutana na waandishi wa Mwanaspoti, anawachangamkia huku akitoa tabasamu la mtu aliyepata kitu kikubwa maishani mwake.

Wakati waandishi hao wanampa pole ya changamoto ya kukaa rumande kwa kipindi kirefu kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi, anajibu kwa ujasiri na kusema alipata muda mwingi wa utulivu na kufikiri vitu kwa kina.

Oktoba, 2021 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haikumkuta na hatia Kaburu huku aliyekuwa Mwenyekiti wake Evans Aveva akikutwa na hatia hivyo kuhukumiwa kifungo cha nje cha miezi sita.

Kaburu anaanza kwa kicheko kisha anasema; “Maisha yana safari ndefu sana, lakini kukaa kwangu ndani hakujanifanya niwe mnyonge, nilipata muda wa utulivu na kuyatafakari mengi yaliyonifunza na kuniingizia vitu vipya kichwani mwangu.

“Sikuwahi kuvichukulia vitu kwa upande mbaya zaidi ya kujifunza, ndio maana nina uhuru wa kuendelea kushabikia soka na timu yangu ya Simba, kiufupi nina ujasiri mkubwa wa kuzikabili changamoto mbalimbali katika maisha yangu.”

Katika mahojiano yake na Mwanaspoti anafunguka mambo mbalimbali ikiwamo na kufurahishwa na hatua ambayo Simba imepiga akiwa anapitia changamoto.


MABADILIKO SIMBA

Anakiri Simba kwa sasa ina mabadiliko makubwa, lakini walianza kuyafanya na aliyekuwa mwenyekiti wa timu hiyo Aveva, yeye akiwa makamu, hivyo anafurahishwa na mwendelezo huo.

“Waliokuja nyuma yetu wameendelea na mchakato wa mabadiliko, lakini yalianza chini yetu, soka kwa sasa linaendeshwa kisasa, hivyo hakuna namna yoyote ya kukwepa hilo, lazima tuendane na ulimwengu unavyokwenda.

“Wakati wa uongozi wetu lengo ilikuwa ni kuchukua ubingwa wa Afrika na tulijaribu kufika kwenye hatua fulani Ligi ya Mabingwa, nimeliona hilo ndani ya miaka minne ambayo Simba ilikuwa inachukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

“Hilo kwa sasa linapaswa kuwekewa mikakati kabisa, ili Simba iwe timu ya kwanza kutwaa taji hilo, inawezekana kutokana na uwekezaji mzuri utakaofanya wasajiliwe wachezaji wazuri na sina maana kwamba waliopo ni wabaya.”


NGUVU SIMBA B

Anasema ipo haja kwa viongozi wa Simba kuelekeza nguvu kutengeneza timu za vijana zitakazowafanya wawe na hazina ya wachezaji wenye moyo wa uzalendo na Simba.

“Ni kweli kipindi cha miaka minne naona uongozi uliwekeza nguvu zaidi timu kubwa na wanawake (Simba Queens), ndio maana zilikuwa na mafanikio ya hali ya juu.

“Ila kwa hawa viongozi ambao wataingia madarakani watatakiwa kuwekeza nguvu kwa timu za vijana za Simba kwa maana ya U-15, U-17 na U-20 naamini kuna faida wataipata kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo tulipata mastaa wengi kama kina Jonas Mkude, Ibrahim Ajibu na wengine wengi,” anasema.

Anasema kuzalisha vipaji ni biashara kubwa ambapo wanaofanya vizuri wanaweza wakawa wanauzwa ndani na nje, jambo ambalo litakuwa faida kwa Simba.


CHAMA STAA WA TIMU

Kwake halina ubishi kuona mpishi wa mabao Clatous Chama (asisti 11) ni staa wa timu, kutokana na kazi kubwa anayoifanya ndani ya timu hiyo.

“Kila timu ina staa wake, Simba naona ni Chama na sio mimi ndiye niliyemchagua bali ni mashabiki kwa namna wanavyomuongelea. Wakati mwingine akikosekana kunaonekana kama kunakuwa na presha kubwa.

“Kwa ukubwa wa majukumu yake, Chama anapaswa kupewa heshima yake inavyotakiwa na hilo halimaanishi kama wengine hawafai ila wakilitazama kwa jicho la faida litaongeza ushindani ili kila mmoja awe kwenye thamani ya juu ambayo itawafaidisha wenyewe kwa kupata pesa nyingi,” anasema.

Anatolea mfano enzi za Emmanuel Okwi alivyokuwa anatajwa kila sehemu kulingana na kuwafurahisha mashabiki kwa kazi yake ya uwanjani, kwamba sasa ni zamu ya Chama.

“Kilichokuwa kinawafanya mashabiki lisiwakauke midomoni mwao jina la Okwi ni ufundi na nidhamu yake ya kazi, ndio maana aliishi muda mrefu kwenye fikra za watu, Chama akifanya hivyo atakuwa kipenzi cha mashabiki kwa muda mrefu,” anasema.

Akiwa Simba Chama amewahi kuuzwa mara moja mwaka 2012 kwa timu ya RS Berkane ya Morocco, ingawa hakudumu sana kutokana na kukosa nafasi ya kucheza na kuamua kurejea Simba dirisha dogo la msimu uliopita. Berkane ilimnunua Chama kwa dola 600,000.


OKWI ALIIFAIDISHA SIMBA

“Ukiachana na Luis Miquissone na Chama mwenyewe, Okwi ndiye mchezaji aliyeongoza kwa kuipa Simba pesa nyingi baada ya kuuzwa mara kadhaa, ni kati za sajili ninazojivunia kwani nilimsajili mimi mwenyewe akiwa na umri wa miaka 19.

“Kuna faida ya kupata wachezaji wenye viwango vya juu ambao wanapopata timu za nje Simba inafaidika nao, soka kwa sasa ni biashara kubwa.”

Okwi amerudi kuichezea Simba mara tatu tofauti huku akiuzwa mara mbili, aliuzwa mwaka 2013 Etoile du Sahel kwa dola 300,000 na mwaka 2015 kwa timu ya SonderjyskE alikocheza nusu msimu na kurudi Simba, sababu ni ushindani wa namba.


YANGA uDHAIFU TU

“Nikitaka burudani ya mechi basi naipata timu yangu ya Simba inapocheza, kuhusu Yanga huwa sina muda wa kuifuatilia inafanya kitu gani zaidi ya kukagua udhaifu wa wachezaji wao, kisha kuufanyia kazi.

“Ninachokiamini Simba ina kikosi kizuri ingawa kuna udhaifu mchache sana nadhani viongozi wameufanyia kazi kupitia usajili wa dirisha dogo kuongeza watu wa kazi ambao watasaidiana na waliopo.

“Licha ya kwamba Yanga inaongoza Ligi Kuu sidhani kama inaweza ikasimama kifua mbele ione imeshamaliza kazi na kutangaza ubingwa, vivyo hivyo kwa Simba, haiwezi kujihakikishia hilo ama kukata tamaa kwani zipo mechi nyingi na lolote linaweza likatokea,” anasema.

Anachoshauri kwa mastaa wa Simba ni kujitoa na kuweka akili zao kwenye kazi na wajuane namna ya kucheza kwa kombinesheni itakayofanya wawe tishio kwenye mechi zilizosalia.


SERA ZA WAGOMBEA

“Japokuwa nilienguliwa kwenye mchakato wa awali nilipokuwa miongoni wa wagombea nafasi ya uenyekiti, hilo haliwezi kunizuia kuhudhuria kampeni za wagombea wengine, kwani nataka kujua sera zao ili nijue nani wa kumuunga mkono,” anasema Kaburu huku akisisitiza suala la kuja kugombea tena siku za usoni litategemea uzima na mipango ya Mungu.