Zidane aanza kukusanya benchi lake la ufundi
Muktasari:
- Nyota na kocha huyo wa zamani wa Real Madrid amehusishwa kwa kiasi kikubwa na kuchukua mikoba ya kuinoa timu ya taifa mwishoni mwa Kombe la Dunia 2026.
PARIS, UFARANSA: ZINEDINE ZIDANE anaripotiwa kuanza kuunda timu yake ya benchi la ufundi kuelekea uwezekano wa kuwa kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa.
Nyota na kocha huyo wa zamani wa Real Madrid amehusishwa kwa kiasi kikubwa na kuchukua mikoba ya kuinoa timu ya taifa mwishoni mwa Kombe la Dunia 2026.
Shirikisho la Soka la Ufaransa (FFF) halijatangaza rasmi nia yake, lakini inaaminika mazungumzo tayari yamefanyika.
Kwa mujibu wa gazeti la L’Equipe, baadhi ya mazungumzo hayo yamegusa suala la nani ataungana na Zidane kwenye benchi la ufundi endapo atapewa nafasi hiyo. Msaidizi wake wa zamani Real Madrid, David Bettoni, anaweza kuwa miongoni mwa watakaojiunga naye.
Kuteuliwa kwa Zidane kuwa kocha wa Ufaransa kunaweza kuwa mojawapo ya uteuzi mkubwa wa makocha watakaoonekana majira haya ya joto.
Manchester United wanatarajiwa kumteua kocha wa kudumu, huku Michael Carrick akiwa kocha wa muda baada ya kufukuzwa kwa Ruben Amorim mwezi huu.
Ni nafasi ambayo Zidane aliwahi kuhusishwa nayo hapo awali, huku Thomas Tuchel, Luis Enrique na Gareth Southgate wote wakitajwa kuwa katika kinyang’anyiro cha kuinoa klabu hiyo ya Old Trafford.
Oliver Glasner ni mgombea mwingine baada ya kuthibitisha ataondoka Crystal Palace mwishoni mwa msimu. Xabi Alonso pia yupo huru sokoni kufuatia kufukuzwa kazi na Real Madrid. Alvaro Arbeloa amechukua nafasi Bernabeu, lakini vigogo hao wa Hispania huenda wakataka kocha mwenye uzoefu na jina kubwa zaidi majira ya joto.
Hata Manchester City wanaweza kuingia sokoni kutafuta kocha, baada ya Pep Guardiola mwezi uliopita kuonya kuwa klabu “lazima iwe tayari” kupanga maisha bila yeye, alisema: “Nina furaha hapa, nataka kubaki hapa. Nisemaje? Mwisho wa siku, matokeo ndiyo huamua.
“Inapofika mwisho wa sura, klabu itachagua aliye bora zaidi kuendeleza kipindi hiki cha ajabu ndani ya Man City.
“Kumekuwa na uvumi mara nyingi kwa miaka ya hivi karibuni, lakini nataka kubaki hapa. Mwishoni mwa msimu, tutaona.”