JIWE LA SIKU: Ishu ya Kibu, Mnunka ni yale yale

Muktasari:

  • Suala la Kibu lilivyoanza, alisaini mkataba mpya na Simba, Juni mwaka huu uliokuwa na hekaheka nyingi akitaka mkwanja mrefu. Hata hivyo, baada ya kelele nyingi za wengi kusema anastahili, Simba ikampa na kusaini.

BAADA ya sekeseke la Kiungo mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis na klabu yake kumalizika kwenye tamasha la Simba Day, kuna sinema nyingine imeubuka kwa Wekundu wa Msimbazi, lakini safari hii ni kwenye timu ya wanawake, Simba Queens.

Suala la Kibu lilivyoanza, alisaini mkataba mpya na Simba, Juni mwaka huu uliokuwa na hekaheka nyingi akitaka mkwanja mrefu. Hata hivyo, baada ya kelele nyingi za wengi kusema anastahili, Simba ikampa na kusaini.

Hata hivyo, baada ya kukamatia mkwanja huo, akaenda mapumzikoni Marekani na baada ya bata kuisha alitakiwa kuripoti kambini Misri lakini hakutokea.

Mvutano ukawepo wa pande mbili kati yake na Simba kwa kutoonekana kwenye kambi, huku sababu zikitajwa, mara ameenda Kigooma kumuuguza mama mzazi, mara ametimkia Norway kufanya majaribio kabla ya dili hilo kudaiwa lilishindikana.

Hata hivyo, mwishowe alirejea nchini na juzi alitambulishwa kwenye kilele cha Simba Day baada ya kusamehewa.

Sasa kwa upande wa wanawake, ishu ya Mnunka imeibua sintofahamu baada ya ghafla tu kutoweka klabuni na hata akipigiwa simu haziiti. Kwa kifupi kazima simu.

Hata kwenye usiku wa tuzo za Shirikisho la Soka nchini (TFF) zilizofanyika kwenye Ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam, hakutokea na badala yake tuzo zake zilichukuliwa na nahodha wa timu hiyo, Violeth Nickolaus.

Kwenye usiku huo aliiondoka na tuzo tatu, mchezaji bora wa Ligi (MVP), Mfungaji Bora akiondoka na kiatu na akiingia kwenye kikosi bora cha mwaka.

Inaelezwa Mnunka hajaungana na wachezaji wenzake kambini huku New Heroes Queens klabu inayotajwa itacheza Ligi Kuu ya Wnawake msimu ujao ndiyo inayompa jeuri nyota huyo tishio kwenye eneo la ushambuliaji.

Kilichopo ni bosi wa timu hiyo ameanza na usajili wa mchezaji huyo tishio WPL, huku pia ikihusishwa na nyota wengine kadhaa waliocheza Ligi Kuu wa ndani na nje ya nchi wakiwamo waliotemwa na Simba na Yanga.

Simba Queens ambao ni mabingwa wa Ligi ya Wanawake msimu uliopita imeweka kambi Bunju Dar es Salaam kwa ajili ya michuano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) inayotarajiwa kuanza Agosti 17, mwaka huu, Ethiopia.

Ikiwa ni wiki ya pili sasa inakwenda, Mnunka ambaye bado ana mkataba wa mwaka mmoja na miamba hiyo ya soka la wanawake na mabingwa watetezi wa kombe hilo, hajatokea mazoezini na hata akitafutwa kwenye simu hapatikani.

Inaelezwa pia, sababu kubwa ni bosi huyo wa timu inayomtaka kupania kuuvunja mkataba wa nyota huyo ambaye bado ni mali ya Simba ili akacheze kwenye kikosi chake ingawa kwa upande wa vviongozi wa Simba hawana taarifa za mchezaji huyo na simu yake haipatikani.


MKWANJA MIREFU

Inaelezwa kama dili la Kibu lingetiki Norway, angeuzwa kwa takriban Sh2 bilioni na Simba ingefaidika na mauzo yake.

Kwa Mnunka, inaelezwa tayari imemkabidhi nyumba na gari na kumuahidi mshahara mnono kama atasaini klabuni hapo na bosi wa klabu hiyo yuko tayari kumwaga pesa ndefu ili tu mchezaji huyo mwenye tuzo tatu msimu huu za MVP, Mfungaji Bora na kuingia kwenye kikosi bora amwage wino hapo.


WOTE MUHIMU

Kibu ndiye mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Simba kwa sasa, vivyo hivyo kwa Mnunka ambaye aliisaidia timu hiyo kubeba ubingwa wa ligi kwa mabao 20 aliyofunga msimu uliopita.

Katika eneo la ushambuliaji bila shaka Mnunka ndiye mchezaji muhimu Simba, hivyo kuondoka kwake haraka huenda ikawa pigo kwa mabingwa hao wa nchi na wawakilishi wa kimataifa.