Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

JICHO LA MWEWE: Prince Dube amezungukwa na Sayansi tatu tofauti

Muktasari:

  • Kila mtu alitamani Dube awe mchezaji wake wakati ule alipotua nchini na kuvaa jezi ya Azam. Akili yangu ilikuwa inawapongeza namna Azam walivyofanya kazi nzuri ya ‘kumscout’ Dube na kumleta nchini. Alikuwa analijua lango na wote tukamwita ‘Mtoto wa Mfalme’.

MPIRA wetu mgumu. Una mauzauza mengi. Hauwezi kuamini namna ambavyo mshambuliaji anayeitwa Prince Dube alivyogeuka kuwa kichekesho katika soka leo. Alikuwa ndoto ya kila mtu. Kila mtu? Ndio, kila mtu nchini ni shabiki wa Simba au Yanga.

Kila mtu alitamani Dube awe mchezaji wake wakati ule alipotua nchini na kuvaa jezi ya Azam. Akili yangu ilikuwa inawapongeza namna Azam walivyofanya kazi nzuri ya ‘kumscout’ Dube na kumleta nchini. Alikuwa analijua lango na wote tukamwita ‘Mtoto wa Mfalme’.

Baada ya kila kitu kilichotokea, Yanga walifanya fitina na kuinasa saini yake. Wakati anatua Yanga, Injinia Hersi Said alisikika akidai kwamba lazima Dube angefunga mabao ishirini na kuendelea. Unapofikiria kwamba nyuma ya Dube kuna Aziz Ki, Clatous Chota Chama na Pacome Zouazou unaelewa kwanini Injinia alikuwa na jeuri ile.

Lakini ghafla Dube amegeuka kichekesho. Alianza vema katika mechi za maandalizi ya msimu mpya lakini ghafla amegeuka kuwa kichekesho. Anakosa mabao ya wazi ambao zamani alikuwa hakosi, anashindwa hata kutuliza mpira, anashindwa kufungua njia zake ambazo wote tulimzoea kuona akizifungua kwa urahisi na kufunga mabao.

Katika pambano dhidi ya Al Hilal pale Temeke Dube aligeuka kuwa kichekesho. Mbele ya macho yetu sisi tuliokaa katika televisheni tulishangazwa kumuona akishindwa kuutuliza mpira na kuanguka mwenyewe huku akigaragara ingawa uwanja haukuwa na utelezi.

Kuna sayansi tatu zinaweza kutumika katika kumjadili Dube. Sayansi ya kwanza ni sayansi ya mpira. Kwamba Dube amekwenda katika timu kubwa. Amepata presha kubwa ambayo hajawahi kuipata tangu aanze kucheza soka.

Amecheza katika klabu za Highlanders ya kwao Zimbwabwe, kisha Supersport United na Balck Leopards za Afrika Kusini halafu akarudi kwao kucheza Highlanders tena ambako Azam walienda kumchukulia huko.

Katika klabu zote hizo ukijumlisha na Azam hakuna klabu yenye mashabiki wengi na wanaofurika uwanjani kama Yanga. Labda Dube amepata presha hapo. Unajaribu kujiuliza ni namna gani alikuwa hapati presha akiwa Azam wakati anacheza dhidi ya Simba na Yanga unashangaa kwa sababu alikuwa anawafunga.

Labda ni jezi ya Yanga tu ndio imekuwa nzito kwake kwa sababu ya presha ya mashabiki ambao sasa anachezea timu yao badala ya kuwashambulia kama alivyokuwa Azam. Hili ni jambo la kisaikolojia zaidi.

Kuna Sayansi nyingine ya pili. kuna wachezaji huwa mambo yanawaendea ovyo tu kama wakihama kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Haijalishi kama wanaweza kumudu presha lakini mambo hayaendi sawa na hawaendelei tena kuwa kama walivyokuwa hapo awali.

Imewahi kuwatokea wanasoka wengi hata barani Ulaya. Mfano ni Philippe Coutinho. Mambo hayakwenda sawa alipoamua kuhama Liverpool kwenda Barcelona. Hauwezi kusema kwamba Coutinho alikuwa hawezi kumudu presha kwa sababu tayari alikuwa amecheza chini ya mashabiki wendawazimu wa Anfield na mambo yalikuwa safi tu.

Alishindwaje kucheza chini ya mashabiki wa Camp Nou? Baadaye alienda zake Bayern Munich kwa mkopo lakini mambo yakawa yale yale tu. Unashindwa kucheza katika presha ya mashabiki wa Allianz Arena wakati ulishafanya mambo makubwa na mashabiki wa Anfield wenye presha kubwa zaidi.

Iliwahi kumtokea pia Fernando Torres. Alipohama kutoka Anfield kwenda Stamford Bridge maisha hayakuwa yale yale. Huwa inatokea. Huenda ni kitu ambacho kinaweza hata kumtokea Dube ingawa ni mapema kusema hili kwa sababu ana miezi mitatu tu tangu aanze kuichezea Yanga mechi za kishindani.

Halafu kuna sayansi hii ya tatu ambayo hauwezi. Kuithibitisha hadharani. Sayansi ya ushirikina. Nimeinamisha sikio ardhini kujaribu kusikiliza kinachosemwa kuhusu Dube pale Jangwani nadhani sayansi hii inaaminiwa na watu wengi pale Jangwani.

Kwamba huenda kuna mambo ya kishirikina ambayo Dube amefanyiwa na wenzake pale klabuni au amefanyiwa na watu wa kule alikotoka. Kwamba kule alikoondoka aliondoka kwa jeuri kubwa na wameamua kumkomesha.

Sisi ambao tunakaa katika viti vya mbele kanisani huwa hatuamini haya lakini wenzetu huwa wanaamini. Nasikia kuna jitihada kubwa zinafanywa kumrudisha Dube kupitia katika mambo hayo. Sisi hatujui chochote isipokuwa tunatumia sayansi ya kwanza.

Sayansi ya kwanza ni hii ya presha. Labda anahitaji kutuliza kichwa chake tu. Inawezekana apewe hata penalti afunge kwa ajili ya kurudisha uwezo wake wa kujiamini. Wakati mwingine wachezaji wanahitaji hivi. Kai Havert alianza vibaya Arsenal na ilipotokea penalti wachezaji wenzake wakampa katika pambano dhidi ya Bournemouth ili arudishe uwezo wake wa kujiamini.

Kitu kizuri kwa Dube ni kwamba ana bahati kubwa mashabiki wa Yanga na viongozi walimfahamu katika uwezo wake tangu alipotua nchini. Kama angekuwa ni mchezaji mpya katika soka letu nadhani angeweza kuonyeshwa mlango wa kutokea Januari tu.

Bahati kila mtu anamfahamu Mtoto wa Mfalme na uwezo wake wa kuziona nyavu. Hii ni bahati ambayo itamfanya aendelee kununua muda wake katika jezi za kijani na njano. Anaweza kurekebisha mambo kama ilivyowahi kumtokea Aziz Ki.

Aziz alikuwa ovyo katika msimu wake wa kwanza kabla ya kujipata katika msimu wa pili. Na alivumiliwa kwa sababu tu mashabiki wa Yanga walishauona uwezo wake akiwa na ASEC Mimosas ilipokuja nchini kucheza dhidi ya Simba.

Mpira upo kwake mwenyewe Dube. Itategemea na kile ambacho anakiamini katika sayansi hizi tatu ambazo zimemzunguka. Sisi kazi yetu ni kuendelea kukitazama kinachotokea uwanjani. Mengineyo atajuana na kina Injinia Hersi.