JICHO LA MWEWE: NILICHOKIONA SIMBA VS AS VITA KWA MKAPA

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

PASAKA njema kwa mashabiki wa Simba. Maisha yanataka nini zaidi? Saa chache kabla Yesu hajafufuka unakwenda Uwanja wa Mkapa au unakaa mbele ya timu yako ukiwa ni shabiki wa Simba na unashuhudia wakimchakaza Vita na kutinga robo fainali.

PASAKA njema kwa mashabiki wa Simba. Maisha yanataka nini zaidi? Saa chache kabla Yesu hajafufuka unakwenda Uwanja wa Mkapa au unakaa mbele ya timu yako ukiwa ni shabiki wa Simba na unashuhudia wakimchakaza Vita na kutinga robo fainali.

Simba wameibuka viongozi wa kundi lao la A. Hakuna ambaye alitazamia hapo kabla. Ilidhaniwa kwamba Al Ahly angeongoza kundi halafu wengine wangewania nafasi ya pili. Na kama ungebashiri kwa haraka haraka basi nafasi hiyo ungeipeleka kwa AS Vita kutokana na historia yake.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Juzi nimeona mengi Uwanja wa Mkapa. Kitu cha kwanza kikubwa ni namna ambavyo Simba wanacheza huku wanaringa. Wamarekani wangesema Simba inacheza kwa swagga. Wachezaji wake wanaringa. Wanajua kwamba wanakwenda kushinda.

Kwa miaka mingi sijawahi kuona timu ya Tanzania inayocheza kwa maringo katika michuano ya kimataifa kama Simba hii. Sijawahi kuona Taifa Stars, Yanga au Simba wakicheza kama Simba wa juzi. Hata hao Simba wa zamani akina Nicodemus Njohole hawakucheza kwa maringo kwa ya namna hii.

Nadhani kushinda mechi zote za nyumbani katika hatua ya makundi michuano yao ya mwisho kumewatia kiburi. Lakini pia kuwachapa Al Ahly mara mbili mfululizo katika Uwanja wa Mkapa kumewatia kiburi. Simba wanacheza kwa maringo sana.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Mpango wao wa mechi ulikuwa mwepesi tu. Kuwapa Vita mpira na kisha kuwasubiri kwa ajili ya mashambulizi ya kushtukiza. Hili lilifanyika kwa ufasaha katika kipindi cha pili. Kipindi cha kwanza wachezaji walikuwa wanaonyesha uwezo wao binafsi katika rundo la wachezaji wa Vita langoni mwao.

Simba ina Clatous Chama, ina Bernand Morrison, ina Luis Miquisssone. Achana na Larry ‘Soft Touch’ Bwalya ambaye aliingia kipindi cha pili na kuwateketeza kabisa Vita. Hawa watu wa Simba wote wanajua kukaa na mpira. Wanaujua kumsaka adui na kumpiga chenga kabla ya kuleta madhara makubwa.

Mara nyingi zamani tuliambiwa kwamba timu nzuri huwa zinasukwa kuanzia nyuma lakini Simba hii imesukwa zaidi kuanzia eneo la kiungo kwenda mbele. Mpaka leo sina uhakika kama Simba wana safu nzuri ya ulinzi. Ambacho nina uhakika ni kwamba tishio lao la kwenda mbele ni kubwa kuliko tishio la adui kuja kwao.

Hapo katikati Jonas Mkude na Thadeo Lwanga walicheza vema zaidi lakini kikubwa ni pale Simba wanapokwenda na mpira mbele. Na inapotokea Chama anakuwa katika ubora wake kama juzi basi adui anapata wakati mgumu zaidi.

Nilichokiona juzi tatizo kubwa la Simba linabakia katika mshambuliaji wa kati. Chris Mugalu sijui amerogwa? Mabao yote ya Simba yalifungwa na viungo na si kwa sababu mshambuliaji wao wa mbele hakupata nafasi. Mugalu alipata nafasi nzuri lakini akaishia kuwa ovyo tu.

Kwa Mugalu niliyemuona katika mechi za kwanza wakati anatua Simba hakuwa hivi. Kwa Mugalu niliyekuwa nasikia sifa zake wakati akiwa Zambia hakuwa hivi. Sijui ni kitu gani kinamtokea lakini sisi tunaomtazama kwa sasa tunaamini kwamba Simba inahitaji mshambuliaji mkali zaidi yake. Kuna mechi ambazo viungo hawatafunga na watahitaji mshambuliaji wao kutumia nafasi moja tu aliyopata. Ni kama nafasi ambazo zilimuangukia Mugalu juzi. Sijui kitu gani kinamtokea hasa wakati huu ambao amekuwa mshambuliaji namba moja wa Simba.

Meddie Kagere naye alipoingia hadithi ilikuwa ile ile tu. Hakuna kitu cha maana alichofanya. Labda tuseme kwamba uwezo wake wa kujiamini umekwenda chini kwa sababu amekuwa akipewa dakika chache uwanjani siku za karibuni.

Tuhamie upande wa pili kwa rafiki zetu Vita. Kimewakumba kitu gani? Wamekuwa timu ya kawaida sana. Sio kwa sababu wamefungwa na Simba, hapana, kwa jinsi ninavyowatazama kila siku wamekuwa wakitiririka kwenda chini.

Kitu ambacho nimekiona juzi na kimenichekesha ni ukweli kwamba Tuisila Kisinda na Tonombe Mukoko bado wana nafasi ya kung’ara katika kikosi chao. Wakati wanawaruhusu kwenda Yanga tukadhani kwamba labda mastaa hawa wangekuwa magarasa kwa wakali ambao wangeletwa Vita.

Ukweli ni kwamba Vita niliyoiona bado Tuisila na Mukoko wangeweza kucheza na kuwa mastaa wakubwa Vita. Nilikuwa nadhani kwamba Vita ilikuwa imeimarika zaidi baada ya kuachana na nyota hawa kumbe wamekwenda kuwaimarisha Yanga kuliko walivyojiimarisha wenyewe.

Kichekesho zaidi ni kwamba walimchukua mchezaji ambaye aliachwa na Yanga, Papy Tshishimbi ambaye anashindwa hata kuanza kikosi cha kwanza katika timu. Kitu hiki kinadhihirisha namna gani Simba imeruhusiwa kwenda juu zaidi na wababe wengine wa Afrika.

Kitu kingine ambacho ni kichekesho zaidi ni ukweli kwamba soko la kocha wa Vita, Florent Ibenge huenda likawa limeanza kwenda chini kwa sasa. Alikuwa anatamaniwa sana na matajiri wa Simba na Yanga lakini baada ya vichapo hivi viwili mfululizo kutoka kwa Simba sidhani kama matajiri wa Simba na Yanga watamtaka tena. Vita inacheza kawaida tu.