Prime
JICHO LA MWEWE: Mbona ‘tumemmisi’ Mbwana Samatta mapema hivi?

Muktasari:
- Heshima ni kitu kikubwa katika soka. Nimeamua kukitumia wakati nashuhudia mchezaji akicheza. Watanzania ni watu wa ajabu kidogo. Huwa wanaweka heshima zaidi mchezaji akimaliza muda wake. wakati fulani nilikuwa natamani Mbwana Samatta amalize soka lake ili apate heshima yake.
MCHEZAJI ninayemkubali zaidi kati ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, ni Lionel Messi. Maajabu ya mguu wa kushoto kutoka Argentina. Kwa kila kitu haiondoi heshima yangu kwa Ronaldo. Wakati mwingine najiambia ‘Nilikuwa hai kuwaona hawa jamaa wakicheza soka’.
Heshima ni kitu kikubwa katika soka. Nimeamua kukitumia wakati nashuhudia mchezaji akicheza. Watanzania ni watu wa ajabu kidogo. Huwa wanaweka heshima zaidi mchezaji akimaliza muda wake. wakati fulani nilikuwa natamani Mbwana Samatta amalize soka lake ili apate heshima yake.
Samatta hajawahi kuheshimiwa na Watanzania kama inavyotakiwa. Wakati ule akiwa na Genk, huku aking’ara bado kulikuwa na minong’ono mingi kuhusu yeye pindi anapovaa jezi ya Taifa Stars. Kwamba hajitumi. Kwamba kule anafunga sana kuliko Stars.
Watanzania waliamua kufumbia macho ukweli Ulaya anacheza na watu wanaojua zaidi na huku anacheza na watu wa kawaida. Mbona George Weah hakuwahi kuipeleka Liberia katika michuano ya Kombe la Dunia licha ya ukweli alikuwa mmoja kati ya wanasoka bora duniani?

Katika miaka ya karibuni wakati Mbwana akiwa katika mteremko wake wa maisha ya soka alizidi kuandamwa na mashabiki. Ilikuwa kama vile anajipanga katika kikosi cha timu ya Taifa. Ilikuwa kama vile anajiita kikosini. Maneno ya kejeli yalikuwa mengi.
Kwa wenzetu mchezaji kama Samatta ni lulu. Ni dhahabu. Alitufanya tuamini. Ametufanya tuamini. Amewafanya wengi waamini inawezekana. Inachosha kurudiarudia historia yake ya kutoka Mbagala hadi kucheza Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Inachosha kwa kweli.
Kifupi tu. Ni Mtanzania wa kwanza kuwa mfungaji bora Ligi ya mabingwa wa Afrika. Ni Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya Ubelgiji. Ni Mtanzania wa kwanza kuwa mfungaji bora huko. Ni Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na ni Mtanzania wa kwanza kufunga bao Ligi ya mabingwa Ulaya.

Ni Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi kuu England. Ni Mtanzania wa kwanza kuzifunga Liverpool na Manchester City. Ni Mtanzania wa kwanza kufunga bao Wembley na ni Mtanzania wa kwanza kufanya karibu kila kitu katika soka.
Wenzetu wanaheshimu watu waliofungua njia. Sawa, soka ni mchezo wa ukosoaji lakini wenzetu wanakosoa na kubakiza heshima kwa mtu kama Samatta. Niliona wazi kila siku Samatta anapoteza heshima yake. nilitamani astaafu.
Mara nyingi huwa tunawaheshimu wachezaji wakubwa wakistaafu. Wakati mwingine hata mchezaji kama sio mkubwa lakini akistaafu huwa anaheshimika vilivyo. Zamani tulikuwa na wachezaji wa kawaida tu lakini waliheshimika walipostaafu. Na tulikuwa na wachezaji wazuri ambao nao walikejeliwa wakati ule lakini wakaheshimika maradufu walipostaafu.

Hata hivyo, haijamchukua Samatta hadi astaafu ndipo aheshimike. Juzi juzi tu tumecheza na Ethiopia na tayari umma wa Watanzania umemkumbuka. Mechi mbovu ya kawaida huku wachezaji wengi wa eneo la mbele wakishindwa kuonyesha makali yao, tayari Watanzania wamemkumbuka Samatta.
Huu ndio unafiki wa Watanzania katika ubora wake. Ukweli ni kwamba Samatta bado hayupo katika ubora wake lakini bado ana nafasi ya kuonyesha uzoefu wake uwanjani. Kama sio kwa mechi nzima basi ni kwa dakika kadhaa.
Kuwepo kwake uwanjani tu kunawafanya baadhi ya wachezaji wa timu pinzani kuwa na hofu naye. Hapo ndipo kina Simon Msuva wanafunga mabao na bado tunatoa kejeli kwa Samatta hajitumi uwanjani isipokuwa Msuva ndiye anayejituma zaidi.

Hata mwamuzi akimwona Samatta anaweka heshima zaidi kwake kwa sababu anajua wasifu wake. Ni kitu cha kawaida ndiyo maana imeletwa staili ya kumpa unahodha mchezaji ambaye ni staa zaidi katika taifa. Messi kwa Argentina, Ronaldo kwa Ureno, Neymar kwa Brazil, Mbappe kwa Ufaransa. Mifano ni mingi.
Sasa tunamtaka uwanjani. Wanafiki wote ambao walikuwa wanaongea kwa kejeli nyingi wakati ule ndio wale wale ambao sasa hivi wanahojiwa uwanja wa taifa na kudai pengo la Samatta ni kubwa na limeonekana.
Nadhani akimaliza maisha yake ya soka ndipo tutagundua dhahabu ambayo Watanzania tuliishikilia. Wakenya hawakuwa na mshambuliaji kama yeye japo walikuwa na mchezaji staa anayecheza nafasi ya kiungo, Victor Wanyama.

Waganda hawakuwahi kuwa na mchezaji kama yeye. Mchezaji ambaye amecheza kiwango cha juu hadi Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu England. Hata hivyo sisi tulitumia muda mwingi kumkejeli Samatta hasa wakati akianza kushuka.
Kwa kadri ninavyofahamu soka letu linavyopoteza vipaji kila kukicha nadhani Samatta atakumbukwa zaidi siku za usoni pengine kuliko mchezaji yeyote katika historia ya Tanzania. Kuna Baba zetu kina Sunday Manara walicheza soka katika kiwango cha juu lakini asilimia kubwa ya Watanzania hawakuweza kuwaona ‘live’ uwanjani.
Samatta wamemuona ‘live’ uwanjani akicheza lakini wamemwona pia akipambana na wazungu. Nadhani watamsimulia zaidi kuliko mchezaji yeyote wa Kitanzania. Idadi kubwa ya Watanzania wamemshuhudia Samatta kuliko Manara.
Bila ya kujali kama akirudi kuichezea Stars atafanya makubwa au hapana lakini walau heshima yake imeanza kurudi mapema zaidi. inatoa mwanga tu wa namna gani tutamkumbuka licha ya dunia hii ya mitandao ya kijamii kujaa watu wenye uwezo wa kuandika chochote ili mradi wameshika simu.
Pamoja na kila kitu naamini bado huu ni wakati wa kina Clement Mzize. Kina Samatta wanahitajika katika kuwaonyesha njia kina Mzize na kuwapa uzoefu. Pande zote mbili hazipaswi kukosewa heshima. Wale wanaokaribia kuondoka kina Samatta na hawa wanaokaribia kupewa kijiti kina Mzize. Kila mmoja anapaswa kutiwa moyo.