Ipo siku mwamuzi atapokonywa kipenga mchezoni

Muktasari:

KUNA usemi wa Kiswahili unaosema ukizoeana na mbwa ipo siku ataingia nawe msikitini. Kuna wakati hujiuliza ni nani alikuwa anatunga misemo ya namna hii ambayo huwa na maana pana za kipekee?

KUNA usemi wa Kiswahili unaosema ukizoeana na mbwa ipo siku ataingia nawe msikitini. Kuna wakati hujiuliza ni nani alikuwa anatunga misemo ya namna hii ambayo huwa na maana pana za kipekee?

Misemo hii huwa na hulka ya kutukumbusha mambo mengi juu ya umakini katika maisha ya kila siku tunayoishi kwamba, kila kitu lazima kiwe na mipaka katika ustaarabu na hata kanuni. Ukifanya makosa ya kuacha makosa yanaweza kukukumba mambo makubwa na kujikuta hulka husika inakusababishia madhara.

Nimelazimika kukumbuka msemo huu nikikumbuka matukio mawili ya hivi karibuni katika michezo ya Ligi Kuu Bara, kati ya Mwadui FC dhidi ya Simba SC na hapa tujikumbushe lile la mchezaji Bernard Morrison alipomvuta kaptula mwamuzi wa pembeni wakati mchezo unaendelea.

Tukio lile lilinishtua sana. Lilikuwa ni tukio lenye sura ya udhalilishaji kwa kitu alichofanya Morrison. Hakuwa na sababu ya kufanya vile hata kama alikuwa na haraka ya kuitafutia bao timu yake.

Morrison asingeweza kupiga mpira ule bila ruhusa ya mwamuzi yule ambaye alilazimika kumsaidia mwamuzi wa kati kuweka usahihi wa wapi pa kusimama kwa mabeki wa Mwadui FC kabla ya mpira kupigwa.

Bahati nzuri mwamuzi wa kati alimpa kadi ya njano Morrison, lakini binafsi naona bado kuna hatua zaidi zinatakiwa kuchukuliwa kwani tukio lile lilimdhalilisha mwamuzi husika na sio kitu ambacho kinatakiwa kupita hivihivi.

Tukio lile lilinikumbusha lile ambalo aliwahi kufanya aliyekuwa beki mkongwe Juma Nyosso kwa aliyekuwa mshambuliaji wa Azam John Bocco. Nyosso alikumbana na kibano kikubwa baada ya tukio lile na halikutokea tena.

Achana na hilo katika ziara hiyo hiyo ya Simba kwenye mechi zake tatu za mikoani lilifuata tukio la pale Misungwi kati ya wenyeji Gwambina dhidi ya Wekundu wa Msimbazi. Hapa alikuwa mwamuzi mwingine tena wa pembeni akilazimishwa kushusha chini kibendera chake na beki Ibrahim Ame wakati mwamuzi husika akijaribu kumjulisha mwamuzi wa kati kwamba kuna kitu hakikuwa sawa wakati beki Joash Onyango akifunga bao kwa kichwa.

Hata hivyo, tukubaliane kwamba bao lile lilikataliwa kimakosa kutokana na marudio ya mikanda ya video kuonyesha kwamba hakukuwa na tatizo lolote wakati kona hiyo inapigwa mpaka bao linafungwa, ingawa maamuzi ya mwamuzi yanabaki kama yalivyo.

Kitu cha kukosa nidhamu ni kile alichofanya Ame akimlazimisha mara mbili mwamuzi husika kushusha kibendera chini kwa kumvuta mkono. Hii ilikuwa ni kukosa nidhamu, naamini mwamuzi ataadhibiwa kwa makosa ya kukataa bao. Sambamba na hilo nataraji tena kuona Ame akichukuliwa adhabu kwa kitendo kile na inawezekana alipofanya vile ndio kilichochea mashabiki kurusha vitu uwanjani na kusababisha vurugu kadhaa na mpira kusimama kwa muda.

Ame angetosha kulalamika kwa mdomo, lakini haikuwa sahihi kuvuta mara mbili mkono wa mwamuzi husika ili akubali bao na katika hali ya kawaida asingeweza kushusha chini kwa ushawishi wa Ame. Lile lilikuwa kosa kubwa.

Matukio ya namna hiyo yakiachwa yatazidi kuongezeka na ndipo napoona kama yataachwa kwa kutochukuliwa hatua na kamati za TFF kuanzia ile ya saa 72, kuna uwezekano mkubwa yatajitanua na kufikia hatua mwamuzi wa kati siku moja kupokonywa filimbi au kadi.

Bahati mbaya tupo katika ulimwengu wa soka ambalo wakati mwingine ni nani amefanya kosa au ni mchezaji wa klabu gani amefanya makosa ili adhabu ya aina gani achukuliwe, ukiwa ni ubabaishaji mkubwa kwa watu wanaoendesha kamati hizi.

Kasumba hii ndio inaturudisha nyuma na sitashangaa pia kama matukio kama yale yatatafutiwa namna ya kufunikwa na kuonekana kama hakuna kibaya kilichofanyika katika michezo ile kwani mifano iko mingi kwa wahusika kushindwa kuyachukulia hatua matukio katika kulindana.