Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Inyeshe mvua, liwake jua...Simba baba lao

Inyeshe mvua, liwake jua ...Simba baba lao

JUZI katika Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, Simba ilithibitisha kuwa hakuna cha kuwazuia pale wanapokuwa na jambo lao iwe mvua au jua, baada ya kuichapa Red Arrows bao 3-0 kwenye mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika uwanja uliojaa maji na baadhi ya maeneo huku mvua ikiendelea kunyeesha, wachezaji wa Simba walionesha umwamba wao mbele ya Arrows inayodhaminiwa na kikosi cha jeshi la anga nchini Zambia.

Mabao ya Benard Morrison aliyefunga mawili dakika ya 16 na 77 na Meddie Kagere dakika ya 19 yalitosha kuipa Simba akiba ya mabao matatu nyumbani kabla ya mchezo wa marudiano utakaopigwa Desemba 5 jijini Lusaka, Zambia.

Gazeti hili linakuletea uchambuzi wa mechi nzima ilivyokuwa pale kwa Mkapa juzi.


MVUA

Mvua kubwa iliyonyesha jijini Dar es Salaam siku ya juzi ilisababisha eneo la uwanja la kuchezea kuwa na maji ambayo yalipoteza radha kadhaa za mchezo huo.

Dakika 90 zote za mechi ile zilihitaji nguvu zaidi kuliko ufundi wa wachezaji kutokana na kucheza wakati mvua ikiendelea kunyesha huku uwanja ukiwa unmejaa maji.

Baadhi ya pasi za chini zilishindwa kufika kwa wahusika kutokana na maji na kukwama huku wachezaji wakiteleza na kuanguka mara kwa mara jambo lililopoteza ufundi na mbinu za timu zote mbili.


PABLO ASAPRAIZI

Kocha mkuu wa Simba Pablo Franco aliwashangaza wadau na mashabiki wa timu hiyo baada ya kutoa kikosi kitakachoanza na kukosekana kwa beki mahili wa kulia Shomari Kapombe ambaye hata benchi hakuwepo.

Katika eneo hilo alimuanziasha Israel Mwenda ambaye alicheza kwa ufasaha huku mapungufu yake yakiwa machache kama kurudisha mpira nyuma mara kwa mara.

Wengine walioanza walikuwa ni Aishi Manula, Mohamed Hussein, Joash Onyango, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Rally Bwalya, Sadio Kanoute, Morrison na Kagere huku Mzamiru Yassin, Henoc Inonga, Ibrahim Ajibu na Peter Banda wakiingia kipindi cha pili.


KAZI KAZI

Pamoja na uongozi, mashabiki na benchi la ufundi kufanya jitihada kubwa ili timu ipate ushindi lakini pongezi za pekee ziende kwa wachezaji wa Simba kwa kujitoa kupambana.

Ilifika muda mbinu za kocha zikawa hazifanyi kazi kutokana na uwanja kujaa maji na pasi kushindwa kwenda lakini wachezaji walijitoa na kucheza kwa nguvu zao zote huku wakipigwa na mvua.

Wachezaji wa Arrows walikuwa na nguvu na vimo vikubwa ambapo walicheza sana mipira ya juu iliyokuwa ikipigwa na Simba lakini wachezaji wa Simba hawakuchoka kufanya hivyo kwani ndio njia pekee iliyokuwa imebaki baada ya pasi za chini kukwama.

Inyeshe mvua, liwake jua ...Simba baba lao

MORRISON, MKUDE WAMOTO

Kila mchezaji alitimiza vyema majukumu yake katika hali ile ngumu ya uwanja kuwa na maji.

Simba baada ya kugundua kuwa njia pekee ya kupata ushindi ni kucheza pasi ndefu kwa kuhamisha uwanja, ndipo wachezaji Morrison na Mkude wakaonekana kuwa usukani wa timu.

Mkude aliyekuwa akicheza eneo la kiungo mkabaji, alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kupokonya mipira kwa wapinzani, kuichezesha timu na kwenda na presha ya mchezo huku akipiga kwa ufasaha pasi nyingi.

Morrison licha ya kufunga mabao mawili na kutoa pasi ya bao la Kagere pia aliibuka mchezaji bora wa mchezo kwa namna alivyokuwa kwenye kiwango bora.

Ilifika wakati Simba ikipata au ikianzisha mpira kila mchezaji alifikiria kupeleka pasi ya kwanza kwa Morrison aliyekuwa akicheza winga ya kulia kwani alikuwa katika ubora mkubwa kwa kuwapiga chenga na kuwakimbiza alivyotaka mabeki wa Arrows ambao mara nyingi walijikuta wakimchezea faulo.


NINI KIFANYIKE

Baada ya kumalizana na Geita Gold kesho kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara, Simba itasafiri kwenda nchini Zambia kucheza mchezo wa marudiano na Arrows kule inahitaji sare au ushindi ili kusonga mbele pia hata ikipoteza kwa mabao 2-0 bado itaingia makundi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Pamoja na hayo Simba inatakiwa kwenda na tahadhari katika maeneo tofauti uwanjani ili kupata ushindi ugenini na kutinga makundi kwa kishindo.

Eneo la mabeki, Simba inahitaji kuongeza umakini na mabeki wa kati, Onyango, Wawa na hata Inonga kwani mchezo wa juzi, mshambuliaji wa Arrows James Chamanga alikuwa akiwasumbua hivyo wanapaswa kujifua zaidi ili kumchunga ugenini kwani ni hatari zaidi kwenye mipira ya juu na kutumia nafasi vizuri.

Hivyo hivyo kwa beki wa kulia, Pablo anahitajika kuongeza mbinu za kujilinda zaidi kwani mawinga kama Allasane Diarra, Felix Bulaya na George Simbayambaya ni wazuri katika kushambulia wakichagizwa na kasi, nguvu na chenga na kama kuna uwezekano kurejea kwa Kapombe basi anaweza kuisaidia timu zaidi.

Pia Simba inatakiwa kukumbuka ilivyotolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Jwaneng Galaxy kwa kufungwa nyumbani katika mchezo wa marudiano wakati hadi dakika 45 za mechi hiyo Simba ilikuwa ikiongoza kwa jumla ya mabao 3-0. hivyo wanapaswa kulichukua hilo kama somo kwa kwenda kucheza kwa tahadhari zaidi ugenini.

Matumizi sahihi ya nafasi, kukaba kwa kushirikiana ni miongoni mwa vitu ambavyo Simba inahitaji kuvifanyia kazi zaidi kuelekea mchezo wa marudiano ugenini.


WASIKIE WADAU

Kocha wao Pablo baada ya mchezo huo alisema ameridhishwa na upambanaji wa wachezaji wake na sasa anajipanga kwenda kushinda ugenini.

“Kwa hali ilivyokuwa, namna timu ilivyoimarika na namna kila mmoja anavyopambana naweza kusema nimefurahi, lakini sio sana sababu bado tuna mchezo wa ugenini ambao tunahitaji kushinda,î anasema Pablo.

Naye Mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu anaeleza kuwa baada ya ushindi wa juzi, Simba imejiweka sehemu nzuri ya kuingia hatua ya makundi na kama viongozi wanaendelea na taratibu zote za kusafiri kuwafuata Arrows Zambia.

“Wachezaji wetu wamepambana na kupata ushindi uliotuweka sehemu nzuri hivyo tunaenda kupanga taratibu nyingine ni namna gani tutaenda Zambia na kupata matokeo chanya yatakayotupeleka makundi,” anasema.

Mchambuzi wa soka nchini, Oscar Oscar anasema “Ujio wa Pablo ndani ya Simba kuna kitu kimeongezeka, wachezaji wana morali ya juu na wanajituma hivyo upambanaji waliounesha hapa (kwa Mkapa) inatakiwa wakauoneshe Zambia maradufu,”