Ibrahim Abraham, kinda anayekuja kwa kasi Ligi Kuu

DUNIA imeshuhudia wachezaji kama akina Diego Maradona alivyokuwa akiabudiwa Argentina pamoja na vurugu zake zote lakini kisa ni kimoja tu, guu lake la kushoto lilitosha kuifanya Dunia imtambue kuwa yeye ni nani.

Ryan Giggs, guu lake la kushoto bado linafanya kazi pale Old Trafford ,Ozil leo ananogesha soka pale England akiwa Arsenal na wengineo wengi wanavyotisha duniani kwa kutumia miguu ya kushoto.

Mwanaspoti limepata bahati ya kuzungumza na kinda wa Tanzania Prisons, Ibrahim Abraham ambaye amezungumzia mambo mbalimbali kuhusu maisha yake ya soka na kufafanua namna alivyopata nafasi ya kucheza Tanzania Prisons.


MGUU WA KUSHOTO ULIVYOMPA ULAJI
Mpira wa miguu umekuwa ajira kwa vijana wengi miaka ya hivi karibuni hasa soka la Tanzania ambalo limekuwa lilikikua siku hadi siku na viongozi kuamua kuwekeza huko kwa kumwaga fedha kwenye usajili na mishahara kwa wachezaji.
Beki huyo anasema kutua ndani ya Prisons hakukumpa mawazo kutokana na uwezo alionao ikiwa ni pamoja na kuwa na kitu cha tofauti.

"Natumia mguu wa kushoto na nacheza beki ya kulia hivyo hiyo ni siri kubwa iliyonipa namba ya kudumu kwenye timu ingawa nilitoka timu ya vijana;
"Niliyemkuta anatumia mguu wa kulia hivyo baada ya kupandishwa na kocha kuniona mazoezini kwa mara ya kwanza aliniita na kuniambia nikitumia vizuri mguu wangu nitambadilisha mawazo ya nani ampange hilo limetimia hadi sasa nacheza kikosi cha kwanza." anasema Abraham.


KUNA TSHABALALA MMOJA TU
Abraham amecheza msimu mmoja tangu amepandishwa kutoka timu ya vijana pamoja na kukutana na mabeki wengi wa timu pinzani amemtaja Mohammed Huissein 'Tshabalala' wa Simba kuwa ndiye beki wake bora.
Anasema licha ya kiwango alichoonesha, bado hajioni kufikia uwezo anaotamani kuwa nao huku akikiri kuwa anahitaji muda zaidi wa kuwa bora.

"Natamani kufikia uwezo wa Tshabalala kwani nimekuwa nikivutiwa na namna anavyocheza na kuwa miongoni mwa mabeki wenye mafanikio kwenye soka letu;

“Nimeaminiwa lazima nioneshe uwezo wangu kwenye kazi yangu, napambania namba kuhakikisha kocha anaendelea kunipanga, bado sijafikia kiwango nachotaka kama alivyo Tshabalala,” anasema kinda huyo ambaye amecheza mechi 22 hadi sasa tangu amepandishwa kutoka timu ya vijana.


CHETI KILIMNYIMA AJIRA PRISONS
Tanzania Prisons ni timu ya Magereza imekuwa na wachezaji wengi walio na ajira na wengine ni raia wa kawaida na Abraham ni miongoni mwao ambaye alichukuliwa mtaani na sasa yupo kikosini huko akiwa mchezaji tegemezi.

"Mimi ni raia sio askari Magereza nacheza hapa kama mchezaji wa kulipwa na sio muajiriwa hii ni kutokana na kukosa cheti cha kidato cha nne kwasababu sikumaliza masomo baada ya kuamua kuchagua soka;

"Ofa ya ajira ilikuwepo lakini sina cheti cha kidato cha nne hivyo nitaendelea kuwa mchezaji wa soka la kulipwa siwezi kusema ni wapi nitacheza msimu ujao kwasasa kwani mkataba wangu na waajili wangu unamalizika mwishoni mwa msimu huu nikiwa nimebakiza mechi mbili tu." anasema beki huyo ambaye amekiri kuwa shule haikuwa kipaumbele kwake kutokana na kupenda zaidi mpira.


NI KIRAKA
Ni wachezaji wachache ambao wanaweza kucheza nafasi nyingi uwanjani na kutokuwa na faida kubwa wanapopata nafasi ya kusajiliwa tofauti na wanaocheza nafasi nyingi.
"Pamoja na kocha wangu kuvutiwa zaidi na mimi nikicheza nafasi ya beki mimi ni mchezaji ambaye naweza kucheza nafasi nyingi uwanjani zaidi ya tatu;

"Nacheza winga, kiungo mkabaji na beki ninayoicheza sasa hivyo endapo nikipewa nafasi ya kucheza mbali na hiyo niliyoizoea naweza kufiti maeneo hayo." anasema beki huyo ambaye amejiunga na Tanzania Prisons akitokea Boda United.


AKIKWAZIKA TU MPE MPIRA
Kila binadamu ana ndoto yake na kitu anachokipenda, kuna wanaopenda kuangalia filamu, kusikiliza nyimbo, kuimba na wengine kucheza mpira.
"Mimi ukitaka kunifurahisha nikiwa nimekwazika nionyeshe uwanja na uwe na mpira wa kucheza hasira zangu zote nitazimalizia hapo kwani mpira ndio furaha yangu;
"Nikikwazana na mtu yeyote au nikiwa na hasira basi huwa naenda uwanjani naanza kucheza mpira nitasahau kila kitu kwani nafurahia kucheza mpira na nikiwa uwanjani huwa nasahau kilakitu." anasema Abraham.


EDMUND JOHN NI MTU
Soka la Tanzania limekuwa na limefanikiwa kuwakutanisha wachezaji kutoka mataifa mbalimbali hii yote ni kutokana na namna mpira wetu umekuwa.
"Kuna wachezaji wengi wazuri nimecheza nao kutoka timu pinzani lakini naomba kuthibitisha kuwa winga wa Geita Gold, Edmund John ni bonge la mchezaji anajua sana;
"Ni mchezaji ambaye amekuwa akinipa changamoto uwanjani hasa timu yao inapokutana na timu yetu namuelewa na napenda uchezaji wake pamoja na kunipa changamoto naelewa uchezaji wake."


NABI APEWE MAUA YAKE
Msimu wa Ligi Kuu Bara unatarajiwa kutamalizika Juni 9 mwaka huu lakini kabla ya siku hiyo tayari Yanga wametawazwa kuwa mabingwa wa 29.
Abraham ametaja kikosi chake bora cha msimu huu huku akimtaja kocha Nasreddine Nabi kuwa ndiye kocha bora.
"Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein 'Tshabalala', Nidrin Chona, Henock Inonga, Mzamiru Yassin, Lipre Jr, Feisal Salum 'Fei Toto', Fiston Mayele, Jeremiah Juma na Farid Mussa hiki ndio kikosi changu bora cha msimu." anasema.
Anasema Nabi anastahili kuwa kocha bora kutokana na namna alivyoipa Yanga mafanikio makubwa kwa kutwaa taji la Ligi kuu kutinga hatua ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).


JEZI NAMBA TATU
Wachezaji wanaocheza soka la bongo mbali na jezi zao kuwa na majina ili kuwatambua pia kila mchezaji ana namba ya kuvaa mgongoni ambazo nyingi zimekuwa na maana kwao.
"Navaa jezi namba tatu kwasababu siku ya kwanza nimepandishwa kutoka timu ya vijana na kucheza timu ya wakubwa nilikuta jezi namba tatu ndio imebaki na nikaichukua;
"Mechi yangu ya kwanza kucheza nikiwa na jezi namba hiyo nilifanya vizuri sana na nilipongezwa na kila mmoja ndani ya timu hivyo tangu hapo niliona ni jezi ya bahati kwangu ndio maana naitumia hadi sasa." anasema beki huyo.