Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ibenge ni jibu la mwisho katika maswali ya Azam?

IBENGE Pict

SIKU tano kabla ya Uhuru wa Tanzania alizaliwa Mkongomani Florent Ibenge. Sijui atakuja kuwapa uhuru wa maisha Azam. Alizaliwa Desemba 4, 1961 halafu Tanzania ikapata uhuru siku tano baadae. Desemba 9. Ibenge ana kazi ya kufanya kuleta uhuru fulani hivi hapa Tanzania.


Ametangazwa kuwa kocha mpya wa Azam wikiendi iliyopita. Kocha ambaye alitamaniwa sana na Simba na Yanga. Kocha ambaye alionekana kama vile ni mmoja wa makocha wa bei zile ambazo Watanzania hatuziwezi. Bei za kina Pitso Motsimane. Habari za kusikia kocha analipa Sh120 milioni kwa mwezi. Ibenge naye alikuwa katika orodha ya makocha hawa.


Wakati ule akiwa na AS Vita kisha akaenda kwingineko ilionekana kwamba ambacho kilishindikana yeye kuja kwa mapacha wa Kariakoo ni dau lake kubwa la mshahara. Alitajwa kuwa mmoja kati ya makocha bora barani Afrika na ilimaanisha kwamba kumpata yeye lilikuwa suala la pesa ndefu kidogo. Uwekezaji wetu ulikuwa haujafika huko.

Na sasa kuna matajiri wenye pesa ndefu wamemleta nchini. Ana kazi ngumu ya kufanya. Kuna maswali ambayo Azam wameulizwa kila kukicha na majibu yanakosekana.

IBE 01

Mara ya kwanza na mwisho kwa Azam kutwaa taji la Ligi Kuu ya Tanzania ilikuwa miaka 11 iliyopita. Mwaka 2014. Wakati huo wa kina Kipre Tchetche. Nadhani kuna mashabiki wa sasa hawamjui hata Kipre yule. Mashabiki wa Instagram.

Azam imejaribu kujibu kila swali ili iweze kutawala mpira wa Tanzania, lakini imeshindikana. Kule Afrika Kusini kuna timu inaitwa Mamelodi Sundowns.

Kupitia pesa za tajiri Patrice Motsepe wamefanikiwa kupenya katikati ya timu mbili kubwa na maarufu zaidi Afrika Kusini Kaizer Chiefs na Orlando Pirates na wao ni wababe zaidi katika soka la huko.

Kule Misri rafiki zetu Pyramids bado hawajaweza kutwaa ubingwa wa ndani wa nchi, lakini msimu ulioisha wamefanikiwa kutwaa ubingwa wa Afrika. Azam wanaonekana kutokuwa tayari katika mambo yote mawili. Kutawala ndani ya Tanzania au nje ya Tanzania. Bado hawapo tayari.

IBE 02

Unaweza kusema kwamba ndani ya Tanzania wamekuwa wakifanyiwa figisu nyingi, huku wakubwa wa Kariakoo wakipewa upendeleo mwingi, lakini vipi kuhusu michuano ya CAF? Majuzi walitolewa na timu za Ethiopia na Rwanda katika michuano ya kimataifa. Kwa sasa hautazamii kama Simba na Yanga wangekwama kwa timu za Ethiopia na Rwanda katika michuano ya kimataifa.

Hadi kumfikia Ibenge, Azam wamejaribu kila waliloweza kupata mafanikio katika mpira wetu. Wamejaribu kila walivyoweza kusimama juu ya Simba na Yanga, lakini inaonekana imeshindikana. Kitu kizuri kwao ni kwamba pesa ipo. Pesa imejaribu kuongea kwa kila namna lakini mambo magumu.

Imewahi kuvamia kambi ya Yanga na kuwatwaa wachezaji wao bora kama Mrisho Ngassa na Fei Toto katika zama tofauti. Imewahi kuleta wachezaji bora kutoka nje ya mipaka yetu. Bado mambo yanaonekana kuwa magumu kwa upande wao. Bado inakuwa ngumu kwao kusimama juu ya Simba na Yanga.

IBE 03

Huku kwa makocha wamewahi kuwanyakua makocha wengi bora barani Afrika na nje ya Afrika. Ilifikia wakati walikwenda Hispania kuchukua benchi zima la ufundi. Kuanzia kocha mkuu hadi mpishi, lakini mambo hayakwenda sawa kama walivyofikiri. Tunaoifahamu Azam vizuri tunajua kwamba wamejaribu kufanya kila wanachoweza ili kupata mafanikio. Wamefanya kile ambacho pesa inaweza kufanya.

Na sasa wametua kwa Ibenge. Kila mwanzo wa msimu, Azam huwa wanang’ata meno kwamba watakwenda kufanya makubwa katika msimu unaofuata. Ni kama ambavyo sasa hivi wamefanikiwa kuinasa saini ya Ibenge ambaye ni wazi anaweza kuwa kocha anayelipwa zaidi nchini.

Je, itatosha kwao kufanya vyema ndani na nje ya nchi? Ni suala la kusubiri na kuona ingawa historia inatusuta.

Ibenge na Azam wana kazi ya kumbakisha Fei Toto ambaye ameziingiza vitani Simba na Yanga. Sijui kwanini Fei anazungumzwa kuondoka wakati ana mkataba na Azam.

Muosha huoshwa? Kama walivyoifanyia Yanga ndivyo wanavyoweza kufanyiwa? Ni swali la kusubiri na kuona, lakini ibenge inabidi aanze kwa kumshawishi Fei Toto kubaki klabuni. Timu inapaswa kutengenezwa ikimzumguka Fei.

IBE 04

Faida ambayo Azam wanakwenda kupata kwa Ibenge ni kuwa watakuwa katika nafasi nzuri ya kupata mastaa wengi wazuri kutoka DR Congo.

Anawafahamu mastaa wengi wazuri kutoka huko na katika siku za karibuni inaonekana soko lake DR Congo huwa linatuletea wachezaji wazuri kuliko kutoka katika mataifa mengine. Labda kwa sasa wanashindana na Ivory Coast.

Faida nyingine ambayo Azam wanakwenda kuipata kwa Ibenge ni kwamba anaufahamu vyema mpira wa Afrika ndani na nje ya uwanja.

Wakati mwingine ni bora kumchukua kocha kama Ibenge kuliko kuleta kocha bora kutoka Ufaransa au Ujerumani ambaye hafahamu vyema misingi ya soka la Afrika. Hawa kina Ibenge, Motsimane, Milutin Sredojevic na wengineo wanafahamu siasa za mpira ndani na nje ya uwanja.

Kwa ligi ya ndani Ibenge ana jukumu la kutengeneza timu kali ambayo sio lazima ishinde mechi za Simba na Yanga tu. Inapaswa kushinda mechi za kawaida kila sehemu. Kuanzia Uwanja wa Sokoine hadi Mkwakwani.

IBE 05

Hapa ndipo ambapo wakati mwingine Azam inakwama. Hauwezi kutwaa ubingwa kwa kuifunga Yanga na kufungwa na Prisons na Coastal Union katika mechi zinazofuata. Sio sawa.

Yanga na Simba huwa wanafanikiwa hapa. Wanaokota pointi nyingi katika timu za kawaida kiasi kwamba pambano baina yao kwa wao haliamui sana bingwa. Imetokea msimu huu tu kwa sababu ya pambano kuahirishwa kwa siasa za mpira wetu.

Mara kibao wamekuwa wakitwaa ubingwa wakiwa na mechi hadi tano mkononi kwa sababu wanashinda sana dhidi ya timu ndogo.

Na sasa tunamsubiri Ibenge kuona namna ambavyo ataitengeneza Azam. Haitakuwa kazi rahisi sana. Kuna sehemu mbili ambazo tunasubiri kwa hamu kuona akiisuka Azam. Kuwa nzuri ndani ya ligi yetu na katika michuano ya kimataifa.

Akitufanyia mambo ya Pyramids tutaamini kweli Azam huwa inakwama katika soka la ndani kwa sababu ya fitina za hapa na pale.

Nisisahau pia kuipongeza familia ya Bakhresa. Namna ambavyo wanaipambania timu yao. Pesa sio kila kitu. Wakati mwingine moyo unahitajika zaidi. Wangekuwa watu wengine Azam ingekuwa imekufa zamani. Wao wanapambana na inafurahisha kuona hata kama hawatwai mataji mara kwa mara, lakini wanaleta ushindani mkubwa.

Ukichungulia ratiba ya mechi za Yanga dhidi ya Azam au Simba dhidi ya Azam unaona wazi kwamba hilo ndilo eneo ambalo wakubwa wa Kariakoo wanaweza kujikwaa katika safari zao za ubingwa. Pengo la Simba na Yanga na wengineo ni kubwa, lakini dhidi ya Azam sio kubwa sana. Lolote huwa linatokea uwanjani.