Huyu hapa mtu anayemfanya Carrick kutisha Man United
Muktasari:
- Kwa mtazamo wa nje, inaonekana Holland tayari ana athari chanya kubwa kwa vigogo hawa walioporomoka wa soka la England. Kazi inaweza kuwa ngumu na mahitaji yanaweza kuwa makubwa, lakini ni haki kusema kwamba mzaliwa huyo wa Stockport, ambaye ni mlevi wa soka, ndiye silaha muhimu ya Carrick.
LONDON, ENGLAND: WAULIZE watu wanaomfahamu vizuri Steve Holland watakueleza vyema juu ya mtu huyo aliyekuwa kocha wa Chelsea na England kwa namna alivyokuwa fundi.
“Mpira wa miguu ni maisha yake,” chanzo kimoja kiliiambia BBC Sport.
“Iwe ni Ligi ya Mabingwa Ulaya, mawazo kuhusu wachezaji au jambo lolote lile, ana akili kubwa sana linapokuja suala la undani wa soka.”
Hilo linathibitishwa kwa hili. Badala ya kupumzika na kufurahia ushindi wa Manchester United wa mabao 3-2 dhidi ya Arsenal, Holland alitumia safari ya kurejea Kaskazini Magharibi mwa England akipitia video za mechi hiyo pamoja na kocha mkuu Michael Carrick na benchi zima la ufundi, ili kuandaa mpango wa mchezo wa nyumbani wa Jumapili dhidi ya Fulham.
Siku ya Jumatatu, wakati wachezaji walipopewa mapumziko ya siku moja, Holland na wenzake walikuwa uwanjani Carrington, wakikamilisha mazoezi wanayotumaini yatazaa ushindi wa tatu mfululizo kwenye Ligi Kuu ya England. Na ikafanikiwa. Man United ilishinda tena 3-2 dhidi ya Fulham.
Umakini ni sifa ya Holland, jambo alilolitegemea tangu alipojiunga na Crewe 1992, baada ya kuhitimisha kwamba angepiga hatua zaidi kama kocha kuliko alivyofanya kama mchezaji iwapo angejitolea mapema kwenye taaluma hiyo.
Holland, mwenye umri wa miaka 55, anaamini kuwa aliyekuwa kocha wa England, Graham Taylor pekee aliyekuwa mdogo kuliko yeye alipata leseni ya ukocha ya Uefa A (kama inavyojulikana sasa), alipokuwa na umri wa miaka 21.
Kwa makocha wengine wa benchi jipya la Man United, Carrick alikuwa hata hajaanza shule ya sekondari wakati Holland alianza safari ya ukocha.
Jonathan Woodgate ana umri mkubwa kidogo kuliko Carrick, huku Jonny Evans na Travis Binnion wakiwa wadogo. Ndiyo maana uwepo wa Holland na kupitia uzoefu wake na timu ya England, uwezo wake wa kukabiliana na shinikizo kubwa ni muhimu sana kwa Carrick na benchi lake la ufundi.
Ndiyo pia sababu anapewa sifa nyingi kwa mwanzo mzuri wa kazi ambao tayari umezaa ushindi dhidi ya Man City, Arsenal na Fulham na hivyo kuipaisha timu hiyo hadi katika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu England.
“Hatasumbuliwa na shinikizo na macho ya watu Manchester United,” anasema aliyekuwa mhariri wa Radio Stoke, Graham McGarry, aliyemfahamu Holland vizuri wakati wa miaka yake 16 huko Crewe.
“Atachukua yote kwa utulivu na kufanya kazi yake tu. Mazoezi yake ni bora sana. Unaweza kuona wazi wachezaji wa Man United wanaitikia vizuri.”
Si kwamba Holland anatarajiwa kuzungumza sana kuhusu hilo hadharani. Sifa ya pili inayotajwa mara kwa mara ni kwamba yeye ni mtu wa maneno machache na ni vigumu kumsoma. “Huwezi kujua kama alikuwa ameridhika kimya kimya au amekasirika kwa ndani,” alisema mtu aliyefanya naye kazi.
Lakini uso huo usioonyesha hisia unaweza kusaidia katika utoaji wa ujumbe. Kadri mtu anavyoongea kidogo, ndivyo watu wanavyosikiliza zaidi anapozungumza.
Ni mapema sana kutathmini kazi ya Holland. Ni zaidi ya wiki mbili tu tangu benchi la ufundi lijitambulishe kwa wachezaji wa Man United kama kundi, lakini vyanzo vilivyo karibu vinasisitiza makocha hufanya kazi kwa ushirikiano.
Pia haipaswi kusahaulika kwamba ingawa Darren Fletcher hakushinda michezo yake miwili kama kocha wa muda, aliweka upya mfumo wa uchezaji baada ya kufukuzwa kwa Ruben Amorim, Januari 5, mwaka huu.
Mskochi huyo alianza kuinua morali. Pia alimrejesha Kobbie Mainoo. Hilo liliwafanya wachezaji muhimu Bryan Mbeumo na Amad Diallo warejee kutoka Kombe la Mataifa ya Afrika katika mazingira tulivu, jambo lililompa Carrick nafasi nzuri zaidi ya kufanikiwa.
Kwa mujibu wa vyanzo, mabadiliko yamefanyika katika ratiba ya mazoezi. Sasa siku ni fupi lakini zenye ukali zaidi. Kuna nishati tofauti katika mazoezi na msisitizo zaidi katika kazi binafsi kwa wachezaji mahususi. Ratiba ya siku ya mechi za nyumbani pia imebadilishwa, na sasa wachezaji wanafika Old Trafford karibu zaidi na muda wa kuanza kwa mechi.
Carrick alipewa kazi hiyo mbele ya Ole Gunnar Solskjaer, kwa sehemu kutokana na kazi yake nzuri uwanjani. Lakini, Holland ndiye aliyekuwa akiendesha mazoezi na timu ya England, huku Gareth Southgate akitoa muhtasari wa jumla.
Kwa ushauri wa Southgate, Holland alihitimisha kuwa mfumo wa England ulikuwa mzito sana wakati wa kufuzu kwa Kombe la Dunia 2018, jambo lililosababisha mabadiliko ya kucheza na mabeki watatu.
“Uwezo wa Harry Maguire kucheza na mpira ulikuwa msingi,” Holland alieleza katika uchambuzi wa kina wa dakika 30 kuhusu kazi yake kupitia podikasti ya Coaches Voice mwaka 2021.
Akizungumza na Sky Sports kabla ya mchezo dhidi ya Man City, Maguire alikumbuka uzoefu wake binafsi na Holland.
“Alikuwa bora sana kwa England,” alisema na kuongeza. “Kila mmoja alijua anachopaswa kufanya. Ninakumbuka muda mwingi nikifanya kazi na Steve, na huwa anasisitiza sana mbinu za ulinzi na jinsi ya kuzuia mabao. Ni misingi ya kawaida lakini yenye nidhamu kubwa. Ninaamini atakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha rekodi yetu ya ulinzi.”
Tangu aondoke England baada ya Euro 2022, Holland amekuwa na kipindi kifupi kisichofanikiwa Japan, na pia alifanya kazi fulani kwa Chama cha Mameneja wa Ligi (LMA). Jambo ambalo hakulifanya ni kutafuta umaarufu wa vyombo vya habari.
Mazungumzo yake na Coaches Voice na mahojiano machache na Shirikisho la Soka England (FA) ni nadra sana. “Naibu mkamilifu,” kama anavyoelezewa mara nyingi. Maarifa machache yaliyopo ni ya kuvutia.
“Katika kila zoezi, kadri wachezaji wanavyofurahia kazi yao, ndivyo utakavyopata zaidi kutoka kwao,” alieleza katika mahojiano yaliyochapishwa na FA.
“Ni muhimu kutafuta njia bunifu za kuwasilisha mazoezi yanayojirudia ili kuwachochea wachezaji. Jambo muhimu katika mazoezi ni uhamishaji wake kwenda kwenye mchezo halisi. Ni lazima kujaribu kuongeza uwezekano wa hilo kwa kutokutoka mbali sana na uhalisia wa mchezo.”
Huenda ni mgeni Man United, lakini kukabiliana na madhara ya kuondoka kwa kocha ni jambo ambalo Holland analifahamu vyema.
Ilikuwa ni meneja wa Chelsea wakati huo, Andre Villas-Boas, aliyempandisha kutoka timu za vijana hadi kikosi cha wakubwa.
“Nilikuwa likizo Hispania,” Holland alikumbuka. “Nilipokea simu siku ya pili na nikarudi nyumbani siku ya tatu. Mke wangu hunikumbusha hilo mara kwa mara.”
Villas-Boas alifukuzwa baada ya miezi tisa mwaka 2012. Mrithi wake, Roberto Di Matteo, alishinda Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini naye aliondolewa baada ya miezi minane.
Huku nyuma ya pazia, Holland alikuwa akivutia. Alinusurika vipindi vya Rafael Benitez, Jose Mourinho na Guus Hiddink kabla ya kuondoka ili kujikita kikamilifu na England baada ya Chelsea kushinda Ligi Kuu England katika msimu wa kwanza wa Antonio Conte.
“Katika klabu kubwa, kila siku ni kasheshe,” Holland aliambia Coaches Voice. “Haiko vibaya kama inavyoonekana, lakini uwezo wako wa kukabiliana na nyakati hizo ndio unaoamua. Uzoefu wangu Chelsea umenifundisha kuwa ni kuhusu kushinda. Akili ya ushindi haijumuishi kujionea huruma au kutoa visingizio. Inamaanisha kuchambua na kusukuma kuboresha wakati ujao.”
Maneno hayo yanaonekana kuwa ya busara, hasa ukizingatia kelele na presha kubwa zinazoizunguka Man United, ambao watajaribu kuimarisha madai kwamba ufufuo wao chini ya Carrick na benchi lake si wa muda mfupi, watakapowakaribisha Tottenham Hotspur uwanjani Old Trafford, Jumamosi.
Kwa mtazamo wa nje, inaonekana Holland tayari ana athari chanya kubwa kwa vigogo hawa walioporomoka wa soka la England. Kazi inaweza kuwa ngumu na mahitaji yanaweza kuwa makubwa, lakini ni haki kusema kwamba mzaliwa huyo wa Stockport, ambaye ni mlevi wa soka, ndiye silaha muhimu ya Carrick.