Hizi hapa mechi kumi kali za AFCON tangu 1957
Muktasari:
- Wakati Morocco na Comoros zitakapopambana mjini Rabat katika mechi ya ufunguzi, huo utakuwa mchezo wa 786 katika historia ya AFCON, ikiwa ni msimu wa 35 wa mashindano maarufu.
FAINALI za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zinaanza Morocco kesho Jumapili zikiandika ukurasa mwingine katika historia ya mashindano haya yaliyoanza rasmi mwaka 1957 yakijikita mizizi katika utamaduni wa soka barani Afrika.
Wakati Morocco na Comoros zitakapopambana mjini Rabat katika mechi ya ufunguzi, huo utakuwa mchezo wa 786 katika historia ya AFCON, ikiwa ni msimu wa 35 wa mashindano maarufu.
Kati ya michezo 785 iliyochezwa awali:
562 ilimalizika kwa ushindi, huku 223 ilimalizika kwa sare.
Hapa chini ni mechi 10 Bora zaidi katika historia ya michuano hiyo ya AFCON:
1962- Ethiopia 4-2 Misri
Wenyeji Ethiopia waliwakaribisha watetezi Misri katika fainali mjini Addis Ababa.
Ethiopia ilikuwa nyuma kwa muda mrefu hadi Zeleke Ghirma aliposawazisha dakika ya 74.
Misri ilirejea kuongoza haraka, lakini Worku Mengistou akafunga na kupeleka mechi katika muda wa ziada.
Hapo Ethiopia ilitawala, huku Italo Vassalo na Mengistou wakifunga na kuhakikisha ushindi wa nyumbani.
1963- Misri 6-3 Nigeria
Hii ni moja ya mechi za AFCON zilizozalisha mabao mengi zaidi katika historia ya michuano hiyo na ulifanyika Kumasi, Ghana.
Misri illikuwa mbele kwa mabao 4-0 kipindi cha kwanza, Hassan Shazli na Ibrahim Reda wakifunga mara mbili kila mmoja.
Nigeria ilipata mabao ya heshima, lakini Shazli alifunga jumla ya mabao manne katika ushindi huo wa kihistoria.
1970- Ivory Coast 6-1 Ethiopia
Laurent Pokou aliweka rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika mechi moja ya AFCON (mabao 5) mjini Khartoum, Sudan.
Ivory Coast ilimaliza kileleni mwa Kundi B, ingawa baadaye ilimaliza nafasi ya nne katika michuano hiyo.
1980- Nigeria 3-0 Algeria
Nigeria ikiwa wenyeji ilitwaa taji lao la kwanza la AFCON nyumbani Lagos.
Segun Odegbami alifunga mapema dakika ya pili na kuongeza lingine kabla ya mapumziko, huku Muda Lawal akifunga bao la tatu.
1990- Algeria 5-1 Nigeria
Algeria, wakiwa wenyeji, waliifungua AFCON kwa kishindo kwa kuichapa Nigeria mabao 5-1.
Rabah Madjer na Djamel Menad walifunga mawili kila mmoja. Ajabu ni kwamba walikutana tena fainali, Algeria ikishinda tena bao 1-0.
1994- Tunisia 0-2 Mali
Tunisia wakiwa wenyeji walikutana kitu kizito kwa kupigwa butwaa nyumbani mbele ya Mali, iliyokuwa imerejea AFCON baada ya miaka 22.
Fernand Coulibaly na Modibo Sidibe walifunga kipindi cha kwanza na kuwanyamazisha wenyeji.
1998- DR Congo 4-4 Burkina Faso
Burkina Faso ilikuwa mbele kwa mabao 4-1 dakika chache kabla ya mwisho, lakini DR Congo ilifanya comeback ya ajabu kwa kufunga mabao matatu fasta kabla ya kusawazisha.
Baadaye timu hiyo ilishinda kwa penalti na kutwaa nafasi ya tatu.
2010- Angola 4-4 Mali
Mechi nyingine ya kihistoria ya AFCON ambapo Angola iliongoza kwa mabao 4-0 zikiwa zimesalia dakika 15 kabla ya filimbi ya mwisho, lakini Mali ilifanya comeback kubwa zaidi katika historia ya AFCON.
Seydou Keita alifunga mabao mawili, kisha Frederic Kanoute na Mustapha Yatabare waliifanikisha sare hiyo ya kihistoria.
2021- Ghana 2-3 Comoros
Comoros iliishtua Ghana katika AFCON iliyofanyika ya Cameroon baada ya janga la Uviko-19.
Ghana ilimaliza mkiani mwa kundi, huku Comoros ikipata ushindi wa kihistoria.
Ahmed Mogni alifunga bao la ushindi dakika tano kabla ya mwisho.
2023- Ivory Coast 0-4 Guinea ya Ikweta
Guinea ya Ikweta iliandika historia kwa ushindi mkubwa zaidi wa kushtukiza dhidi ya wenyeji wa fainali zilizopita, Ivory Coast.
Mabao mawili ya Emilio Nsue, huku Pablo Gannet na Yannick Buyla wakiongeza mengine mawili na kuwazima wenyeji bila kutarajia.
Ushindi huo uliiwezesha Guinea ya Ikweta kumaliza kileleni mwa Kundi A.