HISIA ZANGU: Yanga ‘walivyoiteka’ Kigali kwa saa 24 kwa ruhusa ya Kagame

NA ndoto nzuri ni ile iliyoishia pazuri. Ndio, namna ambavyo watu wanaojiita Wananchi walivyoivamia Kigali kwa ruhusa ya Rais Paul Kagame, kisha wakaiteka, halafu wakaanzisha mashambulizi na mwisho wakaondoka wababe. Haitasahaulika kiurahisi.

Magari aina ya Toyota Coaster zaidi ya 70 yaliwasili Kigali kutoka katika maeneo mbalimbali ya Tanzania ikiwa ni kwa mshangao wa wakazi wa Kigali. Mji mzima ulichanua kwa rangi za njano na kijani. Ilishangaza kiasi hiki cha mapenzi ya soka kwa Watanzania.

Rais Kagame alilazimika kumtuma Waziri wa Michezo, Dada mrembo, Munyegaju Aurore Mimosa kwenda katika hoteli ya Yanga, Park Inn Radisson iliyopo maeneo ya Kiyovu kwa ajili ya kuzungumza na wachezaji wa Yanga na kuwatia moyo kuelekea pambano hilo. Sijui kama mrembo huyu aliyekuwa akiendesha gari mwenyewe kama alikwenda katika kambi ya Al Merrikh. Sijui.

Na simulizi hii iliishia pazuri pale ambapo ndani ya uwanja wachezaji walifanya kile ambacho kilipaswa kufanywa na wao ikiwa ni deni kwa maili ambazo mashabiki walikuwa wamesafiri kuiona timu yao huku wakijaza uwanja mpya wa Pele ambao ulifunguliwa majuzi tu wakati FIFA walipofanya mkutano wao wa kisela Kigali.

Yanga walikuwa bora kuliko Al Merrikh. Walikuwa bora kwa dakika 90. Walicheza kwa majivuno na kuonyesha pengo lililopo kati yao dhidi ya Wasudan hawa. Ni pengo kubwa lililosababisha Wasudan wakimbize vivuli vya wachezaji wa Yanga na kujikuta wakicheza rafu zaidi kuliko mpira.

Hakukuwa na matatizo yoyote kwa kipa Djigui Diarra ambaye hapana shaka alikuwa likizo kwa muda mrefu huku akilindwa na Dickson Job, Ibrahim Bacca, Joyce Lomalisa na Yao Yao. Mbele yao alisimama Khalid Aucho ambaye ameanza kutengeneza upacha na Mudathir Yahaya. Wanatazamana kwa haraka wanapokuwa na mpira kwa ajili ya kuupeleka katika eneo la mbele yao.

Ni hapa eneo la mbele yao ndipo tatizo la Al Merrikh lilipoanzia. walikumbana na viungo watatu wa Yanga, Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua na Aziz Ki ambao muda mwingi walikuwa bora kwa kuunganisha timu na kupeleka mashambulizi yenye akili mbele.

Ama kwa kumsaka Clement Mzize aliyekuwa mbele peke yake au kwa wao wenyewe kujaribu kuisaka safu ya ulinzi ya Al Merrikh ukweli ni kwamba eneo hilo Yanga wanaonekana kuwa bora zaidi. Ilidhaniwa kuondoka kwa Fei Toto kungedhoofisha mambo lakini kina Maxi wameongeza ubora zaidi.

Huyu Pacome ni mmoja wa viungo wanaovutia uwanjani. Aliingia Yanga kimya kimya kama kivuli na kelele zikaenda Maxi Nzengeli pamoja na Mahlatse ‘Skudu’ Makudubela ambaye nilikuwa nimekaa naye jukwaani, lakini sasa Pacome anadhihirisha ni kwanini alikuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Ivory Coast msimu uliopita.

Ananyumbulika kiurahisi, anachukua uamuzi kwa haraka akiwa na mpira, anapiga pasi zinazorahisisha mechi, pia anajua kupiga zinazoweza kuifungua safu ya ulinzi ya wapinzani. Anacheza kwa swaga. Anajua kwamba anajua na anataka mashabiki wajue kwamba anajua.

Mbele alibaki kinda wetu, Clement Mzize. Nitaandika zaidi kuhusu yeye kesho, lakini kwa kifupi tu ni kwamba Mzize inabidi awe makini kutumia nafasi chache anazopata. Kama mshambuliaji ana sifa zote ambazo washambuliaji wengi hawana. Anajua kuuficha mpira, anajua kuwapeleka mchakamchaka mabeki, anakokota mpira na kupiga mashuti kwa miguu yake yote. Anahitaji kukamilika kwa kuweza kufunga mabao kwa kutumia nafasi chache anazopata.

Na baada ya ubora wa mchezaji mmoja mmoja, Kocha Miguel Gamondi anaonekana amefanya kazi nzuri pamoja na benchi lake la ufundi. Yanga hawa wana pumzi nzuri ambayo inasababisha wacheze soka la haraka haraka pengine kuliko wakati wa Professa Nabi. Wanapasiana kwa haraka zaidi na kitu kizuri zaidi ni pale wanapokuwa hawana mpira. Wanakaba kwa haraka haraka na kwa wingi kwa ajili ya kuurudisha mpira katika himaya yao.

Ni rahisi kwenda nao jino kwa jino katika kipindi cha kwanza ukiwa bado una pumzi lakini kipindi cha pili inakuwa ngumu kwa wapinzani. Mabao mengi ambayo Yanga imefunga msimu huu imefunga zaidi katika kipindi cha pili. Hata Al Merrikh walionekana kuishiwa pumzi za kucheza na Yanga katika kipindi cha pili.

Ghafla aliingia Kennedy Musonda na kwenda kumuonyesha Mzize namna mpira unavyowekwa katika wavu. Bahati nzuri kwa Mzize ni kwamba kocha hakumtoa wakati Musonda anaingia. Hii ilimaanisha kwamba Yanga walikuwa wanacheza na washambuliaji wawili, uwanjani huku nyuma yao wakicheza Pacome na Aziz Ki.

Baadaye Aziz akampa pasi murua ya kisigino Mzize aliyekwenda kufunga bao la pili. Hii ilikuwa inamaanisha kazi ilikuwa imefanyika kwa ufasaha. Viungo wawili washambuliaji Pacome na Aziz Ki wakawa wametengeneza mabao mawili kwa washambuliaji wao Musonda na Mzize.

Kuanzia hapo nafasi zikazidi zaidi kuanguka kwa Yanga ambapo hawakuzitumia kiufasaha. Wangeweza kuondoka uwanjani na ushindi mnono zaidi lakini kama ilivyo desturi ya soka kwamba kadri unavyotengeneza nafasi zaidi ndivyo unavyozichezea zaidi. Ni Waarabu wa Afrika Kaskazini tu ndio huwa wana nidhamu ya kutumia nafasi.

Wakati mwamuzi akipuliza kipyenga chake kuashiria kumalizika kwa pambano hilo ilikuwa wazi kwamba mashabiki walikuwa wametosheka na kile walichokiona uwanjani. Uchovu wa safari yao ulifidiwa vema na kiwango ambacho kilionyeshwa na wachezaji wao.

Wakati kocha Gamondi akiwakusanya wachezaji wake kwenda kushangilia na mashabiki ilikuwa wazi kwamba Kigali ilikuwa imetekwa na alama ilikuwa imewekwa. Haitawatoka akilini kwa urahisi wote waliokuwapo Kigali kushangilia Yanga. Lakini zaidi ni kwamba matokeo ya mechi hii yatakuwa yameirahisishia Yanga mipango yake katika mechi ya marudiano pale Dar es Aalaam.

Yanga wachukue tahadhari zote wakati huu wakisaka nafasi ya kucheza hatua ya makundi kwa mara ya kwanza tangu walipofanya hivyo kwa mara ya mwisho mwaka 1998. Ni miaka mingi sasa na Yanga wanapaswa kuchukua tahadhari ya kweli kuelekea katika pambano hili la marudiano. Sio kwamba wameifunga timu mbovu, hapana, wameifunga timu bora ila wao walikuwa bora zaidi.

Umakini unahitajika kumaliza kazi Dar es Aalaam kwa sababu mchezo wa soka una maajabu yake. Yanga wanaweza kushangazwa kama wakilegeza mishipa yao ya fahamu. Wana kila sababu ya kwenda katika makundi lakini wawe na nidhamu iliyopitiliza dhidi ya wapinzani wao licha ya kuwa na timu nzuri.

Hadi wakati mwingine lakini kwa wikiendi hii Kigali ilikuwa njano na kijani. Wakati mwingine inatamanisha hata pambano moja la Simba na Yanga lichezwe hapa. Italeta picha ya kuvutia.