HISIA ZANGU: Yanga walipoteza pambano ndani na nje ya uwanja kwa Mkapa

Wednesday September 15 2021
edo pic
By Edo Kumwembe

YANGA walivuna walichopanda juzi jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Walifungwa ndani na nje ya uwanja na timu ya Rivers kutoka Nigeria katika kitu ambacho awali mashabiki wao hawakukatazamia.

Baada ya kukosekana katika michuano hii kwa miaka kadhaa sasa, mashabiki wa Yanga walitaka timu yao irudi kwa mkwara mkubwa katika michuano hii. Haikuwezekana. Haikuwa siku njema kwao uwanjani, lakini pia hawakuwa na siku njema nyingi katika miezi ya karibuni.

Tuanzie wapi? Jinsi walivyofungwa nje ya uwanja. Yanga hawakuwa na maandalizi mazuri ya kuelekea msimu mpya (poor pre-season). Ratiba haikuwa rafiki kwao. Walipotoka Kigoma tu kufungwa na watani wao Simba wakajikuta wakirudi Dar es Salaam kushiriki michuano ya Kagame.

Kuna kundi dogo la wachezaji wa kikosi cha kwanza walishiriki michuano hilo lakini bado ratiba haikuwa rafiki kwa wachezaji wengine ambao ghafla walikusanywa kwenda Morocco kuweka kambi. Hapo hapo kulikuwa na wachezaji ambao bado walikuwa hawajakamilisha uhamisho wao kama Khalid Aucho na Yannick Bangala.

Nilikuwepo kambi ya Yanga Morocco. Msafara ulifuatana na wachezaji watatu ambao walikuwa wanaugua Uviko-19. Viongozi hawakujua. Kufika Morocco Uviko-19 ikasambaa kufikia wachezaji 12 na viongozi kadhaa. Walilazimika kuvunja kambi na kurudi Dar es salaam.

Ilikuwa safari ndefu ambayo ililiacha kundi la waliogua kulekule. Hawa wakiongozwa na Djuma Shabani walirudi siku moja kabla ya mechi dhidi ya Zanaco katika shughuli inayoitwa Wiki ya Mwananchi. Sikushangazwa na kiwango chao katika pambano hilo licha ya bao zuri la Heritier Makambo.

Advertisement

Baada ya hapo Yanga ikaanza kujifungia kambini Kigamboni, lakini nimepenyezewa kwamba ndugu zangu Rivers United wamecheza mechi sita za kirafiki kuelekea pambano hili ikiwemo michuano maalumu ya mechi za kirafiki iliyoandaliwa katika nchi moja ya Afrika Magharibi.

Yanga walicheza mechi mbili za kirafiki na timu ndogo pale Kigamboni. Laiti kama wangepata mechi kadhaa ngumu za kirafiki kama lile pambano la Zanaco, basi huenda maisha yao yangekuwa mazuri zaidi kuelekea katika pambano la juzi dhidi ya Rivers.

Kama pambano hili lingekuja baada ya Yanga kucheza walau mechi sita za ligi nadhani wangecheza vyema zaidi kuliko walivyofanya juzi. Labda wangechangamka vizuri zaidi kuelekea katika pambano hili. Ratiba haikuwa rafiki kwao kuwa wachangamfu uwanjani na mechi hii inaonekana ilikuja mapema zaidi.

Ndani ya uwanja, Yanga walionekana kuwa mbali kidogo katika suala la stamina, nguvu na wepesi kulinganisha na wapinzani wao ambao walionekana kuwa fiti zaidi huku wakicheza kitimu.

Ukosefu wa kuwa fiti uliwafanya Yanga kuugawa uwanja katika vipandevipande hasa katika kipindi cha pili ambapo kulikuwa na kundi linashambulia na jingine linajihami. Hii ilikuja hasa baada ya wageni kupata bao la kuongoza kupitia makosa ya walinzi wa Yanga.

Hauwezi kuruhusu wapinzani wapige mpira vichwa mara mbili ndani ya eneo lako la sita katika uso wa lango. Yanga waliruhusu hivyo huku walinzi wake wakikaba kwa macho. Staa mmoja wa Rivers United aliurudisha mpira wa krosi iliyotokana na kona fupi ndani na kisha mwenzake akapasia wavu.

Hapo Yanga waliigawanya timu yao na wangeweza kufungwa zaidi na zaidi. Ukabaji ulipotea na stamina vikaondoka. Lakini kitu ambacho Yanga wanapaswa kukibeba kuelekea mechi ya marudiano ni namna ambavyo kwa muda mwingi wa mchezo walitengeneza nafasi katika pambano hili.

Wangeweza kuondoka na mabao walau mawili au matatu kama Yacouba Sogne na Fei Toto wangekuwa makini. Walipoteza nafasi za wazi ambazo haupaswi kuzipoteza katika mechi kama hii ya kimataifa. Simba walishawaonyesha Yanga katika kipindi ambacho hawapo namna ya kutumia vizuri nafasi kwenye uwanja wa nyumbani.

Ni wazi kwamba Yanga iliwakosa wachezaji wake muhimu ambao leseni zao zimechelewa. Hatujui Aucho angewapa nini Yanga lakini ni wazi kwamba angeongeza uzoefu katika eneo la kiungo. Tunajua ambacho Djuma angewapa.

Djuma ni mtaalamu wa kusogeza mashambulizi mbele na soka lake limeegemea zaidi huko. Anamzidi Shomari Kibwana kwa mambo mengi likiwemo suala la uzoefu, lakini kitu kikubwa zaidi ni kwamba ana utaalamu wa kupiga pasi za kuzalisha mabao, na wakati mwingine kufunga kabisa.

Fiston Mayele ndiye mshambuliaji ambaye amefunga katika mechi mbili mfululizo za kirafiki. Ni wazi kwamba angekuwa katika nafasi nzuri ya kufanya jambo kama angeangukiwa na nafasi kama zile za Fei na Yacouba. Anawazidi kwa uhodari huo.

Yanga wanaweza kupindua meza Nigeria? Inawezekana lakini itakuwa kazi ngumu. Wanaweza kufunga bao, lakini je wataweza kulihami lango lao kwa ufasaha kwa dakika zote 90? Hili ni swali gumu kwao hasa ukizingatia aina ya mabao ambayo wamefungwa dhidi ya Zanaco na juzi dhidi ya Rivers. Wanafanya mambo mengi hasa katika mipira ya kutengwa.

Tumaini pekee lipo eneo la mbele. Kwa sasa wanaonekana wana uhai eneo la mbele ingawa hawakufunga juzi. Wanatengeneza nafasi nyingi za kufunga na tatizo linakuwa katika utumiaji wa nafasi. Wanahitaji kulifanyia kazi tatizo hili.

Vinginevyo kwa ujumla licha ya kufungwa, lakini Yanga wanaonekana kuwa na wachezaji wazuri katika nafasi mbalimbali. Wanachohitaji kwa sasa ni kuendelea kujenga timu.

Advertisement