HISIA ZANGU: Unapopangwa na Dube usiwasahau hawa hapa


Muktasari:

JINSI mpira ulivyomgonga mgongoni Abdalla Shaibu ‘Ninja’. Jinsi ambavyo Prince Dube aliupitia na kugeuka. Jinsi ambavyo alipiga lile shuti kali. Jinsi ambavyo mpira ulimpita kizembe kipa wa Yanga, Faroukh Shikalo, bado isingeondoa kwamba lilikuwa bao zuri.

JINSI mpira ulivyomgonga mgongoni Abdalla Shaibu ‘Ninja’. Jinsi ambavyo Prince Dube aliupitia na kugeuka. Jinsi ambavyo alipiga lile shuti kali. Jinsi ambavyo mpira ulimpita kizembe kipa wa Yanga, Faroukh Shikalo, bado isingeondoa kwamba lilikuwa bao zuri.

Siku hizi ni wachezaji wa kigeni zaidi wanaoweza kufanya mambo yale. Ni wachezaji wachache wa ndani ambao wanaweza kufanya vile. Haishangazi kuona kila kukicha tunafukuzana zaidi na wachezaji wa kigeni katika suala la uhamisho wa wachezaji kuliko wachezaji wa ndani.

Juzi usiku mitandao yote ilikuwa imejaa picha ya Dube. Wengine walikuwa wakilirudia mara kwa mara. Bonge la bao, hasa kwa mechi kama ile. Wachezaji wakubwa huwa wanatamba katika mechi kama hizi na Dube ni mmojawao.

Lakini tujiulize, Dube anatoka wapi? Zimbabwe. Tangu lini Zimbabwe iliwahi kutuletea wachezaji wabovu? Hakuna. Karibu wote walikuwa katika vikosi vya kwanza na walikuwa wachezaji maridadi. Hakuna garasa kutoka Zimbabwe.

Tuanze na nani? Thaban Scara Kamusoko. Mmoja kati ya viungo bora wanaojua kuurahisisha mpira ambao wamepita Tanzania. Alitoka Zimbabwe na kuibadili kabisa Yanga. Niliandika hapa jana, huyu ndiye aliyekuwa mwasisi wa staili ya ‘kampa kampa tena’.

Huyu ndiye ambaye aliwabadili Yanga kwa kiasi kikubwa na kujikuta wakicheza mpira ambao kwa miaka mingi ulikuwa unachezwa na watani wao, Simba. Alishirikiana vizuri na Mnyarwanda Haruna Niyonzima katika kazi hii.

Tangu ameondoka mpaka leo Yanga haijaweza kucheza tena kama timu. Wanahaha kubadilisha wachezaji na makocha, lakini hawajawahi kucheza tena kama timu. Unaweza kujua ni kwa namna gani Kamusoko aliwabadili Yanga. Huenda wakatulia siku watakapopata mchezaji wa aina yake. Alikuwa fundi ambaye macho yako yangependa kumuona kila siku akicheza. Baadaye akawaachia ufalme hawa kina Clotus Chama.

Nani mwingine? Alikuja na Donald Ngoma. Yule ngoma alipokuja alikuwa akidharauliwa sana. Alipozoea akageuka kuwa mmoja kati ya washambuliaji bora kuwahi kucheza nchini akitokea nchi za watu. Mpira wake wote aliuacha Yanga. Alipokwenda Azam ndipo hadithi ilibadilika.

Aliwahi kuja hapa Justice Majabvi. Rafiki yangu mmoja kutoka Zimbabwe, aliwahi kuniambia kuwa Majabvi kule Zimbabwe alikuwa akifahamika kama jaji mkuu. Yaani chief justice kutokana na jina lake la kwanza, lakini pia jinsi alivyokuwa analitendea haki eneo la kiungo.

Wamekuja Wazimbabwe wengi. Pale Azam kwa sasa wapo Bruce Kangwa na Never Tigere ambao ni panga pangua kikosini huku pia wakicheza katika timu ya taifa ya Zimbabwe. Huyu Dube ni ongezeko la Wazimbabwe wengine waliopo kikosini ambao ni tumaini la timu.

Simba pia aliwahi kuwepo mzee mmoja kutoka Zimbabwe, Method Mwanjali. Alikuwa katika siku zake za mwisho za maisha yake ya soka, lakini akili yake ya mpira ilikuwa juu kuliko vijana wetu. Waliomuona ujanani wakati akicheza soka Afrika Kusini wanaamini kwamba Simba wasingeweza kumpata wakati huo.

Huyu Chikwende ambaye Simba wamemchukua kutoka Platinum na anaonekana ni mchezaji wa kawaida kwa sasa hapana shaka anaingia taratibu katika kikosi cha kwanza. Umekuwa utaratibu wa Simba katika miaka ya karibuni tangu wawe na mastaa wengi.

Kumbuka hata kina Larry Bwalya walianza kuonekana magarasa katika kikosi, lakini ghafla sasa hivi wameibuka kuwa mastaa wakubwa kikosini. Kuna sababu mbalimbali ambazo zinawafanya wachezaji waingie taratibu kikosini tofauti na papara zetu.

Kuna wachezaji ambao wanazoea moja kwa moja na kuna wachezaji ambao wanaingia taratibu kikosini. Natazamia Chikwende ataibuka kuwa mmoja kati ya wachezaji tishio katika kikosi cha Msimbazi kwa sababu alishatuonyesha ubora wake akiwa na timu yake ya awali.

Kama ningekuwa mmoja kati ya viongozi wa hizi timu nadhani ningejikita zaidi katika kuangalia soko la Zimbabwe. Nadhani wana vitu tofauti ambavyo wachezaji wa ukanda huu hawana. Si ajabu kuona Wazimbabwe wamejaa katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini. Labda kwa sababu ya kijiografia. Zimbabwe imepakana na Afrika Kusini.

Lakini hata hivyo imekuwa kitu cha kawaida kwa viongozi wetu kutojishughulisha. Wale wanaojishughulisha wanakula matunda yao vyema. Mfano mzuri ni huyuhuyu Dube. Niliwahi kunong’onezwa na viongozi wa Azam kwamba walisubiri kwa madirisha mawili zaidi kabla ya kuinasa saini ya Dube.

Kwanza walimjua vyema na baada ya hapo wakamfuatilia vyema. Sawa, usajili ni bahati nasibu, lakini ni wazi kwamba Azam walikuwa wanajua wanachokitafuta kutoka kwa Dube. Haikuwa bahati mbaya sana. Waliwekeza katika kumfanyia uskauti.

Tatizo letu kubwa katika soka linabakia kwenye uskauti wa wachezaji. Hatufanyi uchunguzi wa kutosha na mara nyingi huwa tunawanunua wachezaji wakati ligi zimemalizika. Hatuwanunui wakati ligi zikiwa zinaendelea.

Ni kitu hikihiki ndicho ambacho kinasababisha mara nyingi tuwagombanie wachezaji hawahawa wanapokuwa wameshakuja nchini.

Kwa mfano, ni wazi kabisa kwamba baada ya Azam utakuja kusikia Dube amesajiliwa na timu nyingine hapahapa nchini.

Nawajua wachezaji wa kigeni zaidi ya kumi ambao wamewahi kuzichezea timu mbili kubwa nchini kati ya Simba, Yanga na Azam. Wapo kina Yaw Berko, Ramadhan Waso, Donald Ngoma, Edwin Mukenya, Obrey Chirwa, Bernard Morisson, Pascal Wawa, Obren Curkovic na wengineo wengi. Umekuwa utamaduni wetu.

Haitafika mbali kabla haujasikia Yanga au Simba wanamtaka Dube na kuna vurugu zinaweza kutokea. Wakati hilo likitokea kumbe huu ndio wakati ambapo Yanga au Simba wangepaswa kutega sikio na kusikilizia ni nani ameibuka kuwa Dube mwingine katika soka la Zimbabwe. Ni nchi ambayo imebarikiwa vipaji vya kila aina.