HISIA ZANGU: Simba mpya, sura mpya, bora hasara kuliko fedheha

Muktasari:

  • Sikuona kitu kama hicho. Alikuwa kiungo wa kawaida tu. Anayepokea mpira na kutoa pasi. Basi. Hakukuwa na maajabu mengine. Kwamba labda ni bingwa wa kukaba. Au ni bingwa wa pasi za mwisho. Au ni mtaalamu wa hali ya juu wa umiliki wa mpira.

NILIMTAZAMA tena na tena Babacar Sarr. Nikavua miwani halafu nikavaa tena. Nikamtazama tena na tena. Labda nilikuwa naona mpira katika macho tofauti. Ni mchezaji aliyekuwa ameletwa kufanya mabadiliko makubwa kikosini na kukomesha utawala wa Yanga?

Sikuona kitu kama hicho. Alikuwa kiungo wa kawaida tu. Anayepokea mpira na kutoa pasi. Basi. Hakukuwa na maajabu mengine. Kwamba labda ni bingwa wa kukaba. Au ni bingwa wa pasi za mwisho. Au ni mtaalamu wa hali ya juu wa umiliki wa mpira.

Jana Simba wamemtangaza Yusuf Kagoma kuwa mchezaji wao mpya. nikimtazama Kagoma nikamlinganisha na Sarr naona wazi kwamba Kagoma ni mchezaji bora kwa mbali zaidi kulinganisha na Sarr. Kagoma ni fundi. Labda tu tatizo la wachezaji wetu wazawa ni kukosa ujeuri wa kupambana.

Nilimtazama tena na tena Pa Omar Jobe. Nikajaribu kujiridhisha zaidi na zaidi. Hata hivyo mwishowe nilikata tamaa na kugundua kwamba Samson Mbangula wa Prisons alikuwa hatari kuliko yeye licha ya kuwa na umri mkubwa kwa sasa.

Naam, haishangazi kuona Simba imejaribu kufumua benchi lake la watu ambao wanasajili wachezaji. Kuna watu hawakuifanya kazi yao ipasavyo kwa muda mrefu sasa pale klabuni. Hasara imekuwa kubwa. Sio kwa Sarr tu. wachezaji wengi waliochukuliwa kwa takribani madirisha sita ya uhamisho wamekuwa wa kawaida tu.

Mchezaji kama Leandre Willy Essomba Onana anaweza kuwa mzuri ndani ya wenzake lakini hawezi kuwa tishio kwingineko. Kuna kiwango Simba walikiweka miaka michache iliyopita na Onana asingeweza kupata nafasi katika kikosi kile. Ni vile hadhi ilishuka na ndio maana akaonekana kuwa tishio.

Na sasa Simba imetangaza wachezaji wapya 11 kikosini. Hao ni mpaka sasa nadhani wengine wanakuja mbele. Steven Mukwala kutoka Asante Kotoko, Debora Fernandes kutoka Mutondo, Jean Charles Ahoua kutoka Stella, Valentine Nouma kutoka Lupopo, Karaboue Chamou kutoka Club Abidjan.

Wengine ni Joshua Mutale kutoka Power Dynamos, Augustine Okejepha kutoka Rivers United, Valentino Mashaka kutoka Geita, Abdulrazak Hamza kutoka Supersport United, Omary Omary kutoka Mashujaa na jana ametangazwa Kagoma.

Haishangazi sana. Kwa ambao tunafahamu soka ukweli ni kwamba Simba ilipaswa kuwa na kazi kubwa ya kupangua kikosi chake na kukisuka upya. Tatizo kubwa la mashabiki na viongozi wetu ni kupenda kusikia wanachotaka kuambiwa.

Kuanzia kupoteza mataji kila siku, mpaka kuambulia kichapo kikubwa walichopata kutoka kwa mtani hao, halafu wakashindwa pia kuingia katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, Simba walikuwa wanashuka kila siku.

Ndani ya timu walikuwa wana utofauti mkubwa kuanzia namna ambavyo timu inaendeshwa hadi namna ambavyo walikuwa wanasajili wachezaji. Nje ya timu wangeweza kutoka na kushambulia waandishi wa habari, wachambuzi, GSM na kila mtu.

Inanikumbusha wakati ule Yanga walipokuwa na timu mbovu ya kina Yikpe lakini kila siku walikuwa wanadai Simba inapendelewa na TFF. Mwisho wa siku mpira unachezwa hadharani na kila mmoja anauona. Na sasa Simba wanafumua karibu kikosi kizima.

Nini kinaweza kutokea? Hatufahamu. Ukweli ni kwamba mashabiki na viongozi hawawezi kuwapa muda wachezaji wala benchi la ufundi. Huu ndio ukweli kuhusu soka letu. Mambo ya kusubiri wachezaji wazoeane huku ikienda kushika nafasi ya tatu kwa msimu wa pili mfululizo sio staili yetu. Hatuwezi kuvumilia hilo.

Kitakachojulikana kwa mashabiki ni kwamba wachezaji wanaweza kuzoeana kwa miezi miwili ya kwanza na baada ya hapo timu ikawa bora. Afrika, hasa Tanzania timu huwa hazina programu. Wachambuzi wa siku hizi wanaita project. Hatuna muda huo.

Kupoteza mechi moja tu dhidi ya mtani, hata kama ni Ngao ya Jamii kunaweza kumfukuzisha kocha au kumfanya atazamwe kwa jicho la wasiwasi. Wachezaji wapya wa Simba na benchi la ufundi lazima waelewe jambo hili.

Kocha Fadlu Davids anapaswa kufahamu hilo. Mshambuliaji Mukwala anapaswa kufahamu kwamba yupo klabuni moja kwa moja kuifanya kazi ambayo Jobe ameishindwa. Kuifanya kazi ambayo Onana ameishindwa. Hatuna muda wa kuwapa wachezaji hawa.

Timu inapaswa kuunganika mapema na kushindana. Hivi ndivyo mpira wetu unavyoendeshwa. Wanaosajili wachezaji Simba kwa sasa wanaamini kwamba wanasajili wachezaji waliokamilika ambao wanapaswa kuungana ndani ya siku chache na kufanya mambo makubwa uwanjani.

Kwa mpira wa wenzetu, baada ya kila kilichotokea Simba katika miaka ya hivi karibuni wangeanza kukijenga kikosi taratibu kama Mikel Arteta alivyoisuka Arsenal. Unasubiri walau madirisha manne kuweza kukipangua kikosi kizima. Lakini hapa unatumia dirisha moja tu kukipangua kikosi kizima kwa sababu mashabiki hawana muda wa kusubiri. Hii inaitwa bora hasara kuliko fedheha.  Wanataka matokeo ya papo kwa hapo.

Kuhusu umri wa wachezaji haina uhakika sana. Huku Afrika tunadanganya sana umri. Inategemea tu mchezaji amedanganya kwa kiasi kikubwa. Wakati mwingine unaweza kusema fulani ni mkubwa kuliko fulani kumbe huyo mdogo ndiye mkubwa na mkubwa ndiye mdogo.

Kinachoamualiwa zaidi ni uwezo wa uwanjani na uwezo wa kujitunza nje ya uwanja. Siwezi kumshikia dhamana mchezaji wa Afrika kwamba ana miaka 22 au ana miaka 30.

Tusubiri na msimu uanze. Msimu ambao Simba wataucheza bila ya Clatous Chota Chama. msimu fulani waliwahi kucheza bila ya Chama na badala yake Larry Bwalya akashindwa kuziba pengo lake. Labda tuangalie ni nani ambaye anaweza kuziba pengo la Chama pale Msimbazi. Taarifa zangu za ndani zinaniambia kwamba kiungo, Ahoua ni fundi na anaweza kufanya kazi hiyo.