HISIA ZANGU: Mwananchi alipomaliza kazi kishujaa kwa Mkapa

MARA ya mwisho Yanga kutinga robo fainali michuano inayoandaliwa na CAF, Clement Mzize alikuwa hajazaliwa. Kelvin John alikuwa hajazaliwa. Ilikuwa mwaka 1998. Yanga walistahili furaha waliyoipata juzi. Ndiyo, walistahili. Safari wamekwenda robo fainali yenye heshima zaidi.

Mwaka ule wakati kina Ken Mkapa wakienda robo fainali ilikuwa ni Ligi ya Mabingwa wa Afrika lakini ilikuwa ukitinga hatua ya makundi tu basi tayari upo robo fainali. Safari hii katika michuano ya Shirikisho ilihitajika wavuke makundi ndio waende robo fainali. Wamefanya hivyo. Kama ilivyo kwa watani wao Simba, Yanga wameenda robo fainali huku wakiwa na mechi moja mkononi.

Baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa watasafiri zao kwenda Lubumbashi kwa ajili ya kutalii kama ambavyo Simba watakwenda Casablanca kutalii. Haitokei mara nyingi katika maisha yetu ya soka. Zamani katika mechi kama hizi timu zetu zilikuwa zinakwenda kutalii kwa maana ya kwamba kukamilisha ratiba baada ya kushindwa kufuzu. Safari hii ni tofauti.

Ndani ya uwanja Yanga walijua kazi ambayo ilikuwa inawakabili na wakaifanya vema. Nilijua maisha yangekuwa magumu kwa Monastir pale Temeke tangu nilipowaona katika pambano la kwanza dhidi ya Yanga pale Tunis. Nilikuwepo uwanjani. Monastir walikifanya kile ambacho huwa wanaweza kukifanya kwa ubora.

Walifunga mabao mawili ndani ya dakika 16 wakitumia vema uhodari wao katika mipira ya kutengwa. Baada ya hapo wakatoweka uwanjani. Yanga wakaikamata mechi yote huku wakitengeneza nafasi kadhaa ambazo kina Fiston Mayele walishindwa kuzitumia vema. Hii ndio staili yao kubwa Monastir na hata majuzi walipocheza na TP Mazembe pale Tunis maisha yalikuwa yale yale.

Waliifunga Mazembe katika dakika ya nne tu kwa mpira wa kutengwa na baada ya hapo mechi nzima ikachezwa na Mazembe ambao walipoteza nafasi kadhaa. Sikushangaa kuona kocha wa Yanga, Nasireddine Nabi akimuanzisha mlinzi, Ibrahim Bacca. Sababu ilikuwa rahisi tu, Bacca ana uwezo mkubwa wa kuruka hewani. Alimuanzisha kwa ajili ya kudhibiti mipira ya hewani ya Monastir.

Hilo lilipowezekana Yanga wakaweka mpira chini. Walicheza katika kiwango kile kile ambacho walicheza kule Tunis lakini wakaongeza gia ya kasi zaidi ambayo iliwamaliza Waarabu. Kenneth Musonda anaonekana kuwa mtu hatari kwa mipira ya kichwa kama ilivyo kwa Mbwana Samatta. Zaidi ni kwamba kila siku anaonekana kuwa hatari uwanjani.

Bahati nzuri kwa Yanga ni kwamba wanapata bahati ya Musonda na Mayele kucheza pamoja. Musonda anadanganya anatokea upande wa kushoto lakini kumbe anampisha Joyce Lomalisa ashambulie kupitia upande huo na yeye anaingia kwa ndani. Matokeo yake Yanga imejikuta na wafungaji wawili hatari kwa pamoja uwanjani huku Mzize akiwa benchi.

Bao la Mayele lilikuja kama mwendelezo wa mabao yake ambayo amekuwa akifunga katika soka letu. Anauburuza mpira kwa chini katika ‘angle’ ambayo kipa hawezi kufika hata akitanua kwapa. Alifanya hivyo mara nyingi kuanzia kwa Beno Kakolanya katika pambano la Ngao ya Jamii.

Alifanya hivyo kwa kipa wa Real Bamako pale ugenini. Lakini juzi pia amefanya hivyo. Ni mabao magumu yanayohitaji nguvu kubwa ya upigaji lakini hilo ndilo ambalo linamtofautisha Fiston na washambuliaji wengine. Si ajabu ndio maana ameitwa katika timu ya taifa ya DR Congo licha ya timu hiyo kusheheni mastaa wengine kina Cedric Bukambu na wengineo.

Juzi Yanga walifanya kila kitu sahihi uwanjani. Silaha yao kubwa ni umiliki wa mpira. Lakini silaha yao nyingine ni uwezo wao wa kukaba na kutomruhusu adui kujitawala uwanjani. Hiki ndicho ambacho kinamuweka nje Aziz Ki kwa sasa kwa sababu hana uwezo mkubwa wa kukaba. Ana uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira lakini kitimu huwa hakabi vema.

Hata kama wasingefanya bado walikuwa wana uwezo wa kufika robo fainali kwa sababu Mazembe alikuwa anafungwa na Real Bamako ugenini. Ni kitu ambacho nilikitabiri. Mazembe hawa wametabirika na wameshuka kwa kiasi kikubwa. Kama Yanga isingefuzu katika kundi hili wangejilaumu wenyewe tu.

Kwa kiasi kikubwa kupita kwa Yanga kumechangiwa na kushuka na TP Mazembe pia. Lakini pia wangeweza kupita kama Mazembe wangekuwa wazuri kiasi cha kuwasaidia kazi katika mechi mbili dhidi ya Monastir. Matokeo yake walipoteza mechi zote dhidi ya Monastir na kuwaacha Yanga kuwa timu pekee ya kupambana na Mwarabu.

Nini kinafuata? Yanga wanakwenda sehemu ngumu zaidi. Wanahitajika kuwa bora katika timu ambazo wanaweza kucheza nazo mbele ya safari. Mpaka sasa kuna kina Pyramids, Rivers, ASEC, Marumo Gallants na wengineo. Hawa wamejichuja na kuwa bora zaidi kuliko wengine katika makundi yao.

Kama ilivyo kwa Simba, Yanga wanahitajika kucheza kiume zaidi katika hatua inayofuata. Ukweli ni kwamba hauwezi kucheza fainali bila ya kucheza dhidi ya timu ngumu katika hatua ya robo au nusu. Unaweza kukutana na timu dhaifu katika makundi lakini hauwezi kukutana na timu dhaifu katika robo fainali.

Yanga wana wachezaji wa hadhi hiyo kwa sasa. Simba pia wana wachezaji wa hadhi hiyo. Jana asubuhi tumeona picha za mastaa Simba na Yanga wakiwa uwanja wa ndege kwa ajili ya kwenda kujiunga na timu zao za taifa. Kama wachezaji wanacheza katika timu za taifa za Congo, Zambia, Uganda, Senegal, Mali basi ni wazi kwamba wana hadhi ya kucheza robo fainali na kudaiwa ushindi.

Wakati nikiamini kitu kizuri kwa Simba ni kuikwepa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, binafsi naamini kitu kizuri kwa Yanga ni kuikwepa timu ya Pyramids ya Misri. Ni kweli hawa hawapo katika hadhi ya Zamalek wala Al Ahly lakini bado wanabakia kuwa timu ngumu na inayocheza katika ligi ngumu na yenye ushindani.

Hawa wengine weusi wenzetu tuna tamaduni zetu. Tunawezana nao. Kuna ambao hatuwawezi kama Mamelodi lakini hawa wengine tunawezana nao. Hawa kina ASEC tunaweza kucheza nao hata ugenini lakini ni ngumu kucheza na Mwarabu kwake. Yanga akimuepuka Pyramids anaweza kwenda mbele zaidi.