HISIA ZANGU: Mukoko na uwanja vyote viliharibu mechi Kigoma

HAIKUWA mechi nzuri. Mpira ulikuwa unabutuliwa kwa muda mwingi kutokana na hali ya uwanja. Kama kiungo mkabaji wa Yanga, Zawadi Mauya alivyotuamulia mechi iliyopita, basi ndivyo kiungo mkabaji wa Simba, Thadeo Lwanga alivyotuamulia mechi hii.

Nalizungumzia pambano la juzi katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma kati ya watani wa jadi wa Ilala, Simba na Yanga. Nilikuwepo uwanjani, lakini kama ilivyokuwa kwa mashabiki wengi waliosafiri kutoka mikoa mingine kuja Kigoma wote hatukuona thamani halisi ya nauli zetu.

Labda mashabiki wa Simba walifurahi kwa sababu tu walishinda mechi na kupata kombe, lakini vinginevyo ilikuwa ni mechi iliyojaa butuabutua na wachezaji wa pande zote mbili walishindwa kuweka mpira chini. Makocha wote wawili Mohamed Nabi wa Yanga na Didier Gomes wa Simba walipanga vikosi vyao kwa kuangalia hali ya uwanja.

Gomes alianza na washambuliaji wawili - John Bocco na Chris Mugalu. Alitaka wapigiwe mipira mirefu waangushiane kwa vichwa wafunge. Muda mwingine walinzi wa Simba walikuwa wakipiga mipira mirefu. Bahati nzuri Yanga wana watu wawili wanaopenda kulinda na kuruka. Bakari Mwamunyeto na Dickson Job. Muda wote walipambana.

Upande wa pili kocha Nabi wa Yanga aliwaweka watu watatu wenye kasi. Ditram Nchimbi, Yacouba Sogne na Tuisila Kisinda ambaye sekunde ya tatu tu ya mechi tayari alikuwa amemuacha Mohammed Hussein Tshabalala nyuma huku akijaribu kufunga.

Dhumuni la Nabi lilikuwa kama la Gomes tu. Kwamba watu hawa wapigiwe mipira mirefu wawakimbize walinzi wa Simba. Viungo waliokuwa wanajaribu kucheza kati ni Larry Bwalya na Feisal Salum. Wengine hawakutaka kucheza. Waliamua kubutuabutua.

Halafu ikaja kadi nyekundu ya Mukoko Tonombe. Kadi ya halali na ya kijinga ambayo haiwezi kumuweka mwamuzi, Ahmed Arajiga matatani. Kila shabiki wa Yanga aliikubali. Kwanini Mukoko alifanya vile? Alipaswa kuonyesha ukomavu na kuwa mchezaji wa kulipwa hasa. Aliwagharimu wenzake.

Kuna wanaomtetea kwamba alifanya vile kwa sababu aliudhiwa na rafu ambayo alichezewa na John Bocco katika pambano

lililopita. Bado unakuwa ujinga. Hii ilikuwa mechi nyingine ambayo ilikuwa muhimu kwa timu yake pengine kuliko mechi iliyopita. Hii ilikuwa mechi ya fainali kombe uwanjani na timu yake ilikuwa inahitaji kombe hilo kama dawa.

Hauwezi kufanya vile. Unahitaji kuhimili hasira zako. Wapo wengine wanaodai kwamba hata wachezaji wakubwa kama kina Zinedine Zidane wamewahi kufanya vile. Ni ujinga kwa sababu upuuzi mmoja hauhalalishwi na upuuzi mwingine. Hata Zidane alilaumiwa kwa upuuzi wake.

Ninachokiona hapa ni kwamba watu wa Yanga na Simba wakimpenda mchezaji wao huwa wanamlinda. Kama kile kitendo angefanya Nchimbi au Deus Kaseke leo tungekuwa tunazungumza habari nyingine. Lakini amefanya Mukoko, mmoja kati ya wachezaji wanaopendwa kikosini.

Huwa inatokea katika soka letu. Mpira akiupoteza Clatous Chama mashabiki hawalalamiki. Akiupoteza Mzamiru Yassin kelele zinakuwa nyingi na mashabiki wanataka atolewe uwanjani. Mashabiki wana vipenzi vyao.

Mukoko alipoondolewa uwanjani kwa ugonjwa feki usioeleweka, wachezaji wenzake waliingia kibaruani kufanya kazi mbili katika kipindi cha pili. Waliendelea kulinda lakini hapohapo mstari wa watu watatu wa mbele ukabaki kama ulivyo. Nchimbi, Yacouba na Tuisila.

Walifanya vyema mpaka waliporuhusu bao la Lwanga. Ni kitu rahisi kufunga bao la kichwa kama ukiwa makini. Hata Joash Onyango aliwahi kuwafunga Yanga vile ndani ya mechi tatu zilizopita. Wachezaji wetu huwa hawashambulii mipira ya kona. Wawe waliokuja kutaka kufunga au wanaojilinda. Wengi wanakaba kwa macho.

Yanga walikaba kwa kulinda eneo (zonal marking) na sio kulinda mtu (man marking). Lwanga alitembea hatua mbili akaruka akafunga. Wachezaji wengi wa Yanga walikuwa wamesimama tu. Shughuli ilikuwa imeishia hapo kwa sababu ingekuwa ngumu kwao kusawazisha.

Mabadiliko ya kuwaingiza kina Kaseke, Farid Mussa na Fiston kwa ajili ya kuubadili mstari wa mbele uliokuwa umechoka hayakuwa na msaada wowote ule. Sanasana nimeanza kuona Simba wakiwa na hofu na Yanga. Au labda kwa sababu ya hali ya uwanja. Au labda kwa sababu walihitaji wachukue kombe wakalale.

Nasema hivi kwa sababu sikuona haja sana ya Gomes kuwaingiza Erasto Nyoni na Kennedy Juma. Aliwahofia sana Yanga? Kwanini asitie nguvu zaidi kusaka bao la pili? Yanga walikuwa pungufu na hata kama watu hawa wawili hawajaingia tayari idadi yao ya kushambulia ilikuwa ndogo.

Wakati mwamuzi Arajiga akipiga filimbi tuondoke uwanjani pambano lilikuwa limeamuliwa kwa bao la kiungo mkabaji kwa mara nyingine. Simba wamelipa deni na sasa tunasubiri pambano la tatu katika mfululizo wa mapambano ya karibuni. Pambano la ngao ya hisani.

Afadhali pambano hilo lirudi Dar es Salaam kwa sababu ukweli ni kwamba viwanja vya mikoani vinaonekana kutokuwa rafiki kwa mechi za nusu fainali na fainali. TFF wana lengo zuri la kusambaza mchezo pendwa mikoani lakini kuna ladha inaondoka kutokana na viwanja.

Achilia mbali viwanja lakini hata hoteli zilikuwa tatizo kubwa Kigoma. Sidhani kama wahusika huwa wanafikiria kwamba huenda fainali kama hizi zikawakutanisha Simba na Yanga. Wageni wengi walikosa sehemu za kulala kutokana na uhaba wa hoteli.

Kama tutapeleka mechi hizi mikoani kwa mara nyingine basi maandalizi ya sehemu ya kuchezea yafanyike walau mwaka mmoja kati ya mechi zenyewe. Sherehe ya juzi iliharibiwa na hali ya uwanja.