Hisia zangu kwa Khalid Aucho na Himid Mao

Wednesday October 06 2021
hisia pic
By Edo Kumwembe

NATAKA kuwaungumzia wachezaji hawa watatu kwa haraka haraka. Wa kwanza ni huyu kiungo mpya wa Yanga, Khalid Aucho. Anatoka Uganda. Ni fundi kwelikweli. Ghafla ameibadili Yanga katika namna ambavyo ilikuwa inacheza. Na sasa inavunia zaidi katika eneo la kiungo.

Tangu kuondoka kwa Thaban Scara Kamusoko hakujawahi kutokea kiungo aliyeitua Yanga zaidi ya huyu Aucho. Anajua kutuliza mpira. Umiliki wake wa mpira (ball control) ni wa kiwango cha juu. Anachonifurahisha ni maamuzi yake kabla ya hajapokea mpira.

Kabla hajapokea mpira Aucho anajua ataupokeaje halafu ataupeleka wapi. Viungo wetu wengi wana tabia ya kuupokea mpira kwanza na kisha kuanza kufikiria wapi kwa kuupeleka. Aucho sio mchezaji wa namna hii. Anailainisha timu kwa sababu anafikiria kabla ya kupokea mpira.

Maono yake katika eneo hilo ni makubwa. Lakini pia ana matumizi makubwa ya nguvu huku akikebwa na umbile lake. Viungo wengi wa Tanzania inabidi wabadilike na kuiga tabia za viungo wanaokuja nchini. Katika eneo la kiungo wa chini kuna huyu Aucho.

Hawa viungo wa chini wana tabia mbili - kwanza kuna wale walinzi (defensive midfielders) halafu kuna wale ambao ni watulizaji wa mipira (holding midfielders).

Hawa defensive kazi yao kubwa ni kukaba na kuharibu. Lakini hawa holding ni kama kina Aucho. Wanatuliza timu.

Advertisement

Hawa Holding kwa sasa wanang’ara zaidi katika timu mbalimbali. Ni kama Sergio Busquet na Barcelona yake au Rodri na Manchester City yake. Wale defensive ni kama vile alivyokuwa anacheza Claude Makelele akiwa na Chelsea au Javier Mascherano.

Pale Yanga katika miaka ya karibuni wamepita viungo wawili wa nje.

Papy Tshishimbi aliyekuja na kuondoka huku nafasi yake ikichukuliwa na Tonombe Mukoko. Wote hawa ni wachezaji tofauti kulinganisha na Aucho kwa sababu walionekana kuwa walinzi zaidi na hawakuwa na uwezo mkubwa wa kuituliza timu.

Pale Simba kuna Jonas Mkude. Huyu ni aina ya Aucho kwa sababu ana uwezo mkubwa wa kuituliza timu ingawa kwa ukabaji sio mzuri. Kumbuka jinsi alivyocheza rafu isiyo na akili katika pambano ya Yanga ambao iliruhusu bao maridadi la Bernard Morrison.

Lakini palepale Simba kuna Thadeo Lwanga. Huyu ni kiungo mkabaji zaidi na hana ubora mwingi akiwa na mpira tofauti na Mkude au Aucho. Lwanga anaingia katika kundi la kina Tshishimbi. Unapopata kiungo wa aina ya Aucho na Mkude inakuwa bora zaidi katika umiliki wa mpira.

Makocha wengi wa kisasa wanapenda ‘holding midfielders’ kwa sababu wanasaidia kutuliza timu na kujenga mashambulizi kuanzia nyuma. Hawa kina Pep Guardiola wanapenda zaidi viungo wamiliki kuliko viungo wakabaji. Haishangazi kuona hautakuta timu ya Pep ikiwa na kiungo hodari mkabaji. Pep anataka kila mtu acheze.

Ni muhimu kuanza kuwakumbusha vijana wetu kutulia na mpira katika eneo hilo. Labda tunahitaji viwanja vizuri na makocha wazuri lakini hawa kina Gift Mauya wanahitaji zaidi kujua namna ya uchezaji huu. Inawezekana ni kipaji zaidi lakini viungo wengi wana mambo mengi.


Himid Mao alivyowakamata Mafarao

KIUNGO wa zamani wa Azam, Himid Mao anaonekana amewakamata Mafarao wa Misri kwelikweli. Himid amesaini katika timu yake ya tatu tangu afike Misri. Amesaini mkataba wa miaka miwili katika klabu ya Ghazi Mahalla inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri.

Awali, aliwasili Misri kwa ajili ya kukipiga katika klabu ya Petrojet ambayo ilishuka daraja. Baadaye akasaini katika klabu ya Enppi ambayo nayo ilishuka. Na sasa amesajili katika klabu ya tatu nchini Misri.

Hii ina maana gani? Inaonekana Himid na Waarabu wanapendana. Kuna mambo mengi hapa nyuma. Inakuwaje mchezaji ambaye ameshusha daraja timu mbili akaendelea kubakia Ligi Kuu? Inaonekana Himid ana ubora ambao timu zake zinakuwa hazina.

Inawezekana anastahili kucheza katika timu za juu zaidi. Lakini hapohapo ni rahisi tu kufikiria kwamba Himid anakuwa mchezaji bora zaidi katika vikosi vyake kulinganisha na wachezaji wengine. Wote tunajua ni namna gani ambavyo Himid huwa anajituma.

Lakini pia kuna uwezekano Himid ana wakala mzuri ambaye ana uhusiano mzuri na klabu mbalimbali za Misri. Wakati mwingine hii ndio faida ya kuwa na wakala mjanja ambaye anajua namna ya kumuuza mteja wake. Haishangazi kuona hapati wakati mgumu kutoka klabu nyingine kwenda nyingine licha ya Misri kuwa na nafasi chache za wachezaji wa kigeni.

Hapohapo jaribu kufikiria ambavyo mastaa wengine wa ndani kutoka Afrika Magharibi wanavyoitamani nchi hii ambayo wote tunafahamu inalipa vizuri mishahara yake kutokana na utajiri uliopo katika klabu mbalimbali nchini humo. Wakala lazima anafanya kazi yake vizuri.

Lakini kuna kitu kingine ambacho kinamsaidia Himid kuendelea kupata timu. Ni kama kile ambacho kimemsaidia Mbwana Samatta kurudi tena nchini Ubelgiji na kutamba. Ni kitu kilekile ambacho sasa hivi kimemrudisha nchini Amiss Tambwe hata kama anacheza Championship. Kuna wakati unaizowea ligi na ligi pia inakuzowea. Ni kitu bora zaidi katika soka hasa kama kuna ubora umeuonyesha na kuna alama umeiacha. Kuna wachezaji wa mataifa ya nje wanaweza kucheza mahala fulani kwa miaka zaidi ya 10 wakihama kutoka hapa kwenda pale kama tu wanakuwa wameaminika. Inaonekana Waarabu wameamua kumuamini Himid kitu ambacho ni kizuri kwake na klabu zenyewe.


Advertisement