Prime
HISIA ZANGU: Kama wachezaji, marefa ‘wanabeti’ tuondoe Ligi Kuu Bara mikekani

Muktasari:
- Kuanzia kwa wachezaji. Waaamuzi. Na baadhi ya viongozi wengi. Hawana pesa ya kutisha. Wengi wanaogelea katika maisha ya chini. Sioni dalili yoyote ya kuepuka vishawishi kama mzigo ukikaa mezani.
KWAMBA mpira wetu umeingiliwa na watu ‘wanaobeti’ ndani ya uwanja, ni miongoni mwa taarifa mbaya zaidi kuwahi kusikia katika mpira wetu. Nanong’onezwa kwamba kuna wachezaji wanabeti, kuna waamuzi wanabeti, na kuna viongozi wanabeti. Habari mbaya. Kitu cha kwanza. Kuna umaskini mkubwa katika mpira wetu.
Kuanzia kwa wachezaji. Waaamuzi. Na baadhi ya viongozi wengi. Hawana pesa ya kutisha. Wengi wanaogelea katika maisha ya chini. Sioni dalili yoyote ya kuepuka vishawishi kama mzigo ukikaa mezani.
Wachezaji wa Ulaya na Asia wanalipwa pesa nyingi, lakini wanaingia katika kashfa hivi. Lucas Paqueta wa West Ham United yupo katika kashfa hii. Huyu ni mchezaji anayelipwa hadi Pauni 60,000 kwa wiki na klabu yake ya London. Hata hivyo yupo katika biashara hii baada ya kugundulika kuwa amekuwa akijipa kadi za njano za uongo.
Kiungo wa Newcastle United, Sandro Tonali alifungiwa kucheza soka kwa miezi 10 baada ya kugundulika kwamba alikuwa akibeti katika Agosti 12, 2023 hadi Oktoba 12, 2023. Huyu ni miongoni mwa wachezaji wanaolipwa pesa nyingi pale Newcastle. Rudi nchini. Kutakuwa na matatizo zaidi. Wachezaji wana njaa.

Waamuzi wana njaa. Mbaya zaidi hakuna namna ambayo tunaweza kugundua kwa urahisi kama wanafanya hivyo. Kuna watu wana namba za simu nyingi na wanaweza kutumia majina feki kufanya hivyo.
Wanaweza pia kutumia simu za ndugu zao kufanya hivyo. Lakini wanaweza kuwapa michongo ndugu zao na kutengeneza mtandao wa kupata pesa. Mchezaji yupo uwanjani anacheza huku akiwa tayari ametengeneza mtandao mkubwa wa marafiki zake kunufaika. Nadhani itakuwa hivyo.
Mchezaji mmoja wa zamani wa Mtibwa na Simba aliwahi kunipigia simu akilalamika kwamba pesa zake zilikuwa zimezuiwa na kampuni moja ya kamari nchini. Alikuwa ameshinda mkeka wake katika pambano moja la Ligi Daraja la Kwanza. Alibeti kwamba timu tishio ya daraja hilo ingeshindwa kupata bao katika kipindi cha kwanza cha pambano fulani dhidi ya timu ya kawaida ya daraja hilo.

Ni kweli ilitokea hivyo na kampuni ikaamini kwamba matokeo ya pambano hilo yalikuwa yamepangwa. Nadhani huyu mchezaji alishirikiana na wachezaji wa timu husika katika kuhakikisha hawapati bao katika kipindi cha kwanza ili wapige pesa.
Fikiria mwamuzi akiamua kubeti kwa kuweka shilingi milioni moja kwamba kutakuwa na penalti nini kitatokea? Atalazimisha penalti ya ajabu na wote tutashangaa. Kumbe yeye na rafiki zake wanatengeneza pesa nyingi kupitia penalti hiyo.
Mwamuzi anayelipwa shilingi laki tano kwa kuchezesha mechi moja atashindwaje kutengeneza penalti mbili ambazo zitampatia shilingi milioni tatu? Huu ni ukweli ambao hatuwezi kuukwepa. Betting kwa mpira wetu itakuja kutuonyesha mambo ya ajabu.
Kwa miaka mingi tumekuwa tukihangaika na tatizo la upangwaji wa matokeo kwa mwamuzi kununuliwa na timu moja, au wachezaji kununuliwa na timu pinzani. Lakini sasa tunakabiliwa na tatizo kubwa zaidi kuliko lile.

Hakuna ambaye atakuwa salama katika janga hili. Hata timu kubwa hazitakuwa salama sana katika hili. Kwa mifumo ya uchezeshaji kamari wao wanaweza kuwa wahanga zaidi. Ukiathiri timu kubwa isipate matokeo pesa inakuwa nyingi zaidi kuliko ukiathiri timu ndogo.
Mfano wa kawaida ni kama Simba ikicheza na Kagera Sugar. Kama ukiweka kuwa Kagera Sugar itapata bao pesa inakuwa nyingi zaidi kuliko ukiweka kuwa Simba inapata bao. Mwamuzi au mchezaji wa Simba anaweza kuingia katika kishawishi kikubwa kufanya upuuzi wa kuhakikisha Simba inaruhusu walau bao moja.
Hata hivyo kwa sababu bado tupo katika zama za hujuma, mara nyingi kama mlinzi wa Simba au kipa wao, Moussa Camara akiruhusu bao la kizembe akili yetu inakimbilia katika kuamini kwamba amehongwa na watani wao kwa ajili ya hujuma. Hatutaangalia suala la kamari.

Pesa nyingine nyingi huwa inapatikana pale unapoweka kwamba Yanga na JKT Tanzania kila timu itapata bao. Ni rahisi kuamini kwamba Yanga inaweza kupata bao dakika yoyote ya mechi, lakini sio rahisi sana kuamini kwamba JKT Tanzania inaweza kupata bao. Unadhani kama mwamuzi au walinzi wa Yanga wamebeti ni jambo gani linaweza kutokea?
Wataalamu wa masuala haya wameniambia kumekuwa na mabao mengi ya ajabu ajabu. Mabao aliyofungwa kipa wa Nigeria wa Singida Fontain Gate hayaingii akilini. Kuanzia haya aliyofungwa na Yanga hadi yale aliyokuwa anafungwa katika siku za nyuma akiwa na Tabora United hata katika mechi za kawaida tu. Zamani ingekuwa rahisi kuamini amenunuliwa lakini ukifuatilia mwenendo kwa ujumla unaweza kujiaminisha kuna tatizo zaidi ya hilo.
Kwa kuanzia kuna umuhimu wa kusimamisha kwanza mechi za Ligi Kuu Bara katika mpira wetu. Hatupo salama sana kwa sababu hatuna mifumo mizuri ya kuzuia wachezaji na waamuzi wasiweke mikeka yao katika mechi. Bahati mbaya kwetu wao ndio wahusika wakuu wa mchezo wenyewe. Kitu kingine ambacho kinaweza kutokea ni kampuni zenyewe za kamari kujiingiza katika kuathiri matokeo ili ziweze kupata faida. Hii inaangukia zaidi hata timu kubwa. Zinaweza kuwa wahanga zaidi kwa wachezaji wenyewe kulipwa pesa nyingi na kampuni za kamari ili wapate matokeo ya kushangaza katika mechi.

Kwa mfano Simba ikifungwa na Coastal Union ni wazi kwamba kampuni za kamari zitapata pesa nyingi kwa sababu watu wengi wanaweka pesa upande wa Simba kwamba itashinda. Vipi kama ikifungwa au kutoka sare? Kampuni zinapata pesa nyingi kwa sababu walioweka kwamba Coastal itashinda ni asilimia chache.
Ingekuwa idhini yangu nadhani mpira wa Tanzania ungeondolewa katika mfumo wa kamari. Hatuna ubavu wa kuzuia nguvu ya pesa ya kamari. Hata viongozi wetu hawana ubavu huo. Kuna viongozi wengi wa klabu zetu ambao wanaweza kushirikiana na watu wa kamari katika kuathiri matokeo. Kama wanaweza kufanya hivyo hata sasa kwa kupokea pesa kutoka timu zenye uwezo wa kifedha, watapata wapi ubavu wa kukataa kupokea ofa mbalimbali za kuathiri matokeo kutoka kwa watu ambao wapo katika umafia wa kamari?