Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HISIA ZANGU: Acheni Mayele atibu moyo wake wenye maumivu

Muktasari:

  • Hii ilikuwa mara ya pili Mayele anautibu moyo wake wenye maumivu. Mara ya kwanza ilikuwa pale alipokutana na mashabiki wa Yanga katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Walipiga naye picha kwa furaha kubwa. Straika wao mahiri wa zamani ambaye aliwapa furaha kwa staili ya kutetema. Walisahau kama kulikuwa na ugomvi hapo kati.

FISTON Mayele yupo Dar es Salaam. Juzi nilimuona akiingia uwanja wa Chamazi akiwa na Rais wa Yanga, Hersi Said. Namna maisha yanavyokwenda kasi. Alishangiliwa na mashabiki wengi wa Yanga waliokuwepo uwanjani. Alikumbuka mambo mengi. Namna alivyokuwa mfalme wao klabuni hapo.

Hii ilikuwa mara ya pili Mayele anautibu moyo wake wenye maumivu. Mara ya kwanza ilikuwa pale alipokutana na mashabiki wa Yanga katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Walipiga naye picha kwa furaha kubwa. Straika wao mahiri wa zamani ambaye aliwapa furaha kwa staili ya kutetema. Walisahau kama kulikuwa na ugomvi hapo kati.

Kivipi anautibu moyo wake? Wakati ule Mayele anashinda mitandaoni akiwa analumbana na mashabiki wa Yanga ni wazi kwamba alikuwa na mkanganyiko wa mawazo wa kuondoka katika nchi ambayo alipendwa na kuabudiwa. Tanzania. Mwili wake ulikuwa Misri, lakini akili yake ilikuwa Tanzania. Alishindwa kuhimili vishindo vya kuondoka Tanzania.

Lakini hapo hapo akajikuta katika msongo mwingine wa mawazo kwa sababu maisha ndani ya uwanja pia yalikuwa magumu. Hakuwa anaziona nyavu kwa urahisi kama ilivyokuwa ‘nyumbani’ kwake Tanzania. Alifikia mahala akaamini kwamba kuna watu wa Yanga walikuwa wanamfanyia mambo ya kishirikina ili asizione nyavu. Maisha yalikuwa tofauti na Tanzania yake nje na ndani ya uwanja.

Tanzania ina raha yake. Kila alipokwenda alishangiliwa, alizungukwa, aliombwa picha na mengineyo. Ghafla akajikuta katika nchi ambayo hatambuliki, hajulikani na wala haabudiwi. Simu yake ndio ilikuwa kitu pekee ambacho kilikuwa kinamliwaza. Zaidi ni kwamba aliamua kulumbana na watu kwa ajili ya kujiweka katika siasa za mitandaoni za Tanzania.

Ni wazi kwamba Mayele anapendwa zaidi Tanzania kuliko kwao DR Congo. Kuondoka Tanzania kulimsumbua. Na sasa amerudi tena walau kupata nafuu ya moyo wake. Kama vile kuingia uwanjani na Hersi ilikuwa ni kutibu moyo wake wenye maumivu ya kuondoka nchini. Anasikia raha kwa mara nyingine kushangiliwa, kuombwa picha na mengineyo.

Tanzania ni nchi tamu. Wachezaji wengi wa kigeni huwa wanapenda kurudi hata kutembea pindi wanapokuwa wameendelea na safari ya kucheza kwingine. Mayele ni mmojawao kama ilivyokuwa kwa kina Emmanuel Okwi na hata sasa hivi kina Bernard Morrison. Tanzania utarudi tu. Chakula kizuri, usalama upo, marafiki wazuri wapo. Ukiondoka utaikumbuka.

Wapo ambao wameoa dada zetu kama vile Tonombe Mukoko. Wapo walioamua kuzaa na dada zetu kama vile kina Bernard Mwalala. Wapo walioamua kutembea na warembo wetu maarufu kiasi kwamba inaaminika walisaini mikataba mipya ili waendelee tu kuwepo nchini. Iliwahi kutajwa hivyo kwa rafiki yetu, Aziz Ki.

Na huyu rafiki yetu Aziz nilijua tu kwamba ingekuwa ngumu kwake kuondoka nchini. Namna anavyopendwa na mashabiki wa Yanga na wanavyofanya ajisikie, klabu nyingine zilihitaji dau kubwa kumng’oa nchini. Labda kama kuhama angeenda Simba au Azam ilimradi tu aendelee kuzurura mitaa ya Masaki na Oysterbay.

Ni vile tu mpira wetu hauna pesa nyingi kama ilivyo kwa Morocco, Tunisia, Algeria, Misri na Afrika Kusini vinginevyo hakuna mchezaji wa kigeni ambaye angependa kuondoka katika soka letu na kuiacha ardhi ya Tanzania. Hata kina Clatous Chama, Luis Miquissone na wengineo walijua chaguo namba mbili baada ya kuondoka nchini lingekuwa kurudi tena hapa.

Sisi tupo kama Afrika Kusini. Mazingira ya maisha yetu ni mazuri. Kule Bondeni nako kuna raha zetu. Mchezaji wa kigeni akienda anaweza asiondoke ile nchi hata kwa miaka 20. Kawaulize kina Dennis Onyango. Hata kijana wetu, Abdi Banda ameishia kuzurura katika klabu za kule kwa sababu ya mazingira.

Bahati nzuri kwa Mayele ni kwamba alichagua vita mbaya katika namna ya kuimisi Tanzania. Vita ya kugombana na Yanga. Hauwezi kushinda kirahisi vita hii. Nadhani baadaye alikuja kugundua kwamba ulikuwa ni ujinga. Ni kama ambavyo imetokea kwa Fei Toto.

Fei alijiingiza katika vita kubwa na Yanga na hasa rais wao Hersi, lakini mbele ya safari nadhani amejua kwamba asingeshinda vita hii kwa urahisi. Majuzi amerekebisha kauli zake na ameonyesha kuwa karibu tena na rais wa Yanga pamoja na mashabiki wao.

Kwa Mayele bahati mbaya nyingine ambayo inamkabili ni ukweli kwamba simuoni akirudi katika nchi yake hii anayoipenda hivi karibuni. Mabao yake mengi aliyofunga akiwa na Pyramids yamemchongea. Dau lake kwa sasa halitapungua Dola 2 milioni. Wanaoweza kumchukua ni wakubwa wengine wenye pesa kama Zamalek, Al Ahly, Waydad Casablanca na wengineo.

Hakuna timu ya Tanzania inayoweza kumudu dau la Mayele kwa sasa. Kiwango chake kikipungua ataweza kurudi nchini, lakini kama Waarabu wenyewe wataamua kuuchana mkataba. Vinginevyo haitakuwa rahisi. Kwetu Sh4 bilioni hatuwezi kuiweka kwa mchezaji mmoja. Ni bajeti ya kuendesha klabu walau kwa nusu msimu.

Zaidi ya kila kitu ni mshahara wake. Nani anaweza kuumudu? Ni wazi kwamba Waarabu watakuwa wanamlipa Sh50 milioni na zaidi kwa mwezi. Bado hatujafika katika mishahara hiyo. Tunajaribu kupambana, lakini hatujafikia viwango hivyo. Kuna baadhi ya timu hiyo pesa ni mshahara wa wachezaji wote kwa mwezi.

Nafahamu kwamba ndani ya ugomvi wake na Yanga, klabu za Simba na Azam zilipambana kumrudisha nchini, lakini mazingira ya kipesa yalikuwa magumu. Wasingemudu vyote viwili. Mshahara wake pamoja na dau la mauzo ambalo Pyramids waliweka kumruhusu aondoke kwa mujibu wa mkataba.

Mayele anakaribishwa kututembelea. Hakuna ubaya. Mmoja kati ya washambuliaji bora wa kigeni kuwahi kucheza katika viwanja vyetu. Amani aliyoitafuta na watu wa Yanga ni kitu bora zaidi kuliko kudai kwamba walikuwa wamemtupia majini asifunge mabao.