Prime
Hili hapa deni jipya la Okello Yanga
JANUARI 12, 2026 ndiyo siku iliyoandikwa kwa herufi kubwa katika historia Yanga wakati mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara ilipotangaza rasmi utambulisho wa kiungo mshambuliaji Allan Okello, kutoka Uganda Cranes.
Ujio huo, uliowavutia mashabiki wa timu hiyo katika ukanda huu wote, ulijiri baada ya Okello kukamilisha dili kubwa la usajili kutoka Vipers SC, hatua inayochukuliwa kama mojawapo ya uhamisho wenye hadhi ya juu zaidi kwa mchezaji wa Uganda kuelekea ligi ya Tanzania.
Okello, mwenye umri wa miaka 25 na sifa ya kuwa mchezaji mwenye ufundi katika eneo la kiungo mshambuliaji, alijiweka kwenye ramani ya soka la Afrika Mashariki kutokana na msimu aliokuwa nao Vipers SC.
Katika msimu wa 2024-25, akiwa na timu yake hiyo ya zamani alifanya vizuri akiingia kambani mara 19 na kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Uganda, aliisaidia timu hiyo kushinda kombe la ligi na kombe la Uganda Cup.
Kiungo huyo katika mechi za ligi kwa kipindi chake nchini Uganda Okello kwenye mechi 58 alizocheza amefunga mabao 24 na pasi 13 za mwisho takwimu zilizothibitisha uwezo wake wa kuchangia kwa ubunifu na kwa matarajio akiwa kwenye eneo la kiungo. (Takwimu za mechi na pasi hazijathibitishwa wazi kwenye vyanzo).
Usajili huo wa Okello pia umeibua rekodi nyingine ya kifedha akiwa mchezaji wa pili ghali zaidi kutoka Vipers SC hadi kufikia kiasi cha Dola 300,000 (kama ripoti mbalimbali zilivyodai), akifuatiwa tu na usajili wa Farouk Miya 2016 kwenda Standard Liege.
Ujio wa Okello ndani ya Yanga umeifanya iwe na orodha ndefu ya wachezaji kutoka Uganda waliowahi kucheza kwenye kikosi hicho. Mwanaspoti linakuletea nyota hao na rekodi walizoacha.
Swali ni je, Okello ataweza kutengeneza rekodi yake mwenyewe ndani ya Yanga kama alivyofanya nje ya timu hiyo, na hata kuvunja au kupanua mafanikio ya wachezaji waliomtangulia kama Hamis Kiiza aliyejulikana kwa rekodi njema ya mabao na ushawishi mkubwa ndani ya klabu?
HAMIS KIIZA
Ni mshambuliaji ambaye ubora wake ulimfanya azitumikie Simba na Yanga. 2011-2015 ndio kipindi chake cha kwanza kucheza Tanzania akijiunga na Yanga na kuichezea mechi 80 za mashindano akiifungia mabao 56.
Hakuishia kuifungia mabao hayo tu ambayo ni rekodi bora kuwekwa na mchezaji wa Uganda, mshambuliaji huyo pia alipata bahati ya kutwaa mataji mbalimbali kabla ya kutua Simba kwa msimu mmoja (2015-2016) na kucheza mechi 30 akifunga mabao 24 yakiwamo 19 ya Ligi Kuu na matano ya Kombe la Shirikisho.
Mshambuliaji huyo ambaye pia alipata nafasi ya kucheza Kagera Sugar, akiwa Yanga alikuwa akivaa jezi namba 20 ambayo amekabidhiwa pia Okello, na ada ya kujiunga na Yanga mapema dirisha dogo la usajili lililofunguliwa mwezi huu.
EMMANUEL OKWI
Ni miongoni mwa washambuliaji bora walioweka rekodi Ligi Kuu Bara kutokana na ubora wa kufumania nyavu aliokuwa nao akianza kuitumikia Simba kabla ya Yanga kuvutiwa na ubora wake na kumshawishi atue Jangwani.
Msimu wa 2014/15 Yanga walifanikiwa kunasa saini ya Okwi ambaye hata hivyo hakuweza kucheza kwa muda mrefu kwani alitumika kwa nusu msimu, ambapo mshambuliaji huyo alitumika kwenye 18 akifunga mabao tisa.
Baada ya kutoka Yanga alirudi tena Simba timu ambayo ndio ilimtambulisha Ligi Kuu Bara akiichezea kwa mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuipa mataji mbalimbali na kutwaa tuzo za ufungaji bora.
JUMA BALINYA
Alijiunga na Yanga akitokea klabu ya Police ya Uganda ambapo alimaliza msimu wa 2018/19 kwa kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu kwao Uganda jambo lililowavutia Jangwani kuwinda saini yake ili aongeze nguvu eneo la ushambuliaji.
Mara baada ya kumalizana na Yanga kwa kusaini mkataba wa miaka miwili Balinya alitambulishwa na uongozi wa timu hiyo mbele ya wanachama katika hafla ya kuichangia Yanga iliyofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Mshambuliaji huyo licha ya kutoka na rekodi Uganda, lakini ndani ya kikosi cha Yanga hakuwa na namba ya kudumu na kujikita akitumika kwenye mechi 15, akifanikiwa kufunga mabao mawili katika mechi zaidi ya 15. Ni hapo uongozi na mchezaji walipofikia makubaliano ya kuvunja mkataba.
GIFT FRED
Beki huyo wa kati wa kimataifa wa Uganda tofauti na matarajio ya wengi baada ya kuimbwa kwenye usajili alipokuwa anatajwa kutua Yanga mambo yalikuwa magumu upande wake mara tu alipotua kutokana na kushindwa kutoboa mbele ya mabeki watatu ambao tayari wamejijengea ufalme ndani ya kikosi hicho.
Gift akitua Yanga msimu wa 2024-25 Yanga tayari ilikuwa na Bakari Mwamnyeto, Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ watatu hao hawakumpa nafasi ya kutumika nyota huyo wa kigeni ambaye alifanikiwa kucheza mechi 15 tu hadi hapo Yanga walipoamua kukaa naye chini na kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba.
Alisajiliwa akitokea Sports Club Villa ya nchini kwao alikocheza kuanzia 2021 hadi 2023. Alikulia kwenye akademi ya Chuo Kikuu cha Bugema, Uganda na mwaka 2019 alibeba tuzo ya beki bora wa mashindano ya vyuo vikuu.
Baada ya kufanya vizuri kwenye mashindano hayo mwaka 2020 alisajiliwa na Gomba Lions na kutwaa Kombe la Masaza Cup, akichaguliwa kuwa beki bora kabla ya kunaswa na Villa lakini ndani ya Yanga alishindwa kufanya vizuri kutokana na ushindani wa namba aliokutana nao.
KHALID AUCHO
Ameondoka Yanga mwanzoni mwa msimu huu baada ya kuitumikia timu hiyo kwa misimu minne mfululizo akiwa panga pangua kikosi cha kwanza chini ya makocha wote waliopita kwenye timu hiyo ndani ya misimu hiyo.
Aucho ameondoka akiwa ni sehemu muhimu ya mafanikio ya Yanga, akihusika katika ushindi wa mataji mfululizo ya Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya ndani, huku pia akiisaidia timu kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022/23.
Aucho ambaye Yanga ilimtambulisha Agosti 9, 2021 kuwa kiungo mpya akitokea Misr Lel Makkasa ya Misri, amekuwa sehemu kubwa ya mafanikio ya ubingwa kwa misimu minne licha ya kuwa panga pangua akicheza kiungo mkabaji ameifungia Yanga mabao mawili pekee.
Kiungo huyo fundi kwa sasa anaitumikia Singida Black Stars na pengo lake ndani ya Yanga linapambaniwa kuzibwa kwani tangu ameondoka, wakisajiliwa nyota wawili eneo hilo ambao ni Moussa Balla Conte aliyetua mwanzoni mwa msimu na dirisha hili dogo amesajiliwa Mohamed Damaro kutoka Singida Black Stars.