Hii Stars inakwenda CHAN kuwakilisha taifa? 

TIMU ya taifa ya soka, Taifa Stars iko kambini kujiandaa kwa fainali za michuano ya ubingwa wa Mataifa ya Afrika, CHAN, inayoshirikisha wachezaji wanaochezea klabu zinazoshiriki ligi za nchi zao. 
Fainali hizo zitafanyika Cameroon kuanzia Januari 16 na kumalizika Februari 7. 
Pamoja na kwamba michuano hiyo ni mikubwa na ambayo ni kipimo halisi cha kiwango chetu cha soka, haionekani kama wahusika wameipa umuhimu huo. Stars imeitwa kama timu ya genge la watu fulani ambayo haiwezi kuwajibika kwa yeyote kama itafanya vizuri au vibaya. 


Kulikuwepo na utamaduni wa kocha wa taifa kuongea na waandishi wa habari wakati anapotangaza timu ili kueleza mikakati yake, sababu za kuteua wachezaji fulani na kuacha wengine ili kuonyesha heshima kwa wananchi wa taifa ambalo amepewa jukumu la kuiongoza timu yao. Lakini haikufanyika hivyo. Timu ilitangazwa mtandaoni na baada ya hapo hakuonekani kama kocha anawajibika kwa aina yoyote kwa Watanzania, ambao wana maswali mengi kuhusu baadhi ya wachezaji walioitwa, hasa baada ya Kocha Etienne Ndayiragije kueleza hadhani misingi anayotumia kuteua timu na kuonekana ameikiuka. 
Taifa limeshikwa na bumbuwazi; inawezekanaje timu ya taifa inayokwenda kushiriki fainali kubwa namna hii iitwe kwa jinsi hiyo na kocha asione umuhimu wowote kuzungumza na wananchi kuhusu mipango yake, mikakati yake, matarajio yao na kutetea kundi aliloliita kuliwakilisha taifa? 
Binafsi ningeweza kuelewa kama angefanya hivyo wakati wa mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi, lakini si wakati anaita wachezaji kwa ajili ya mashindano makubwa ya takriban wiki tatu. Ndio, yeye ndiye atabeba sifa na lawama iwapo timu itafanya vizuri au vibaya, lakini hilo halitakiwi limpe kiburi kiasi cha kutotaka kuzungumza na wananchi kuhusu dhamana aliyopewa. Ni kweli makocha huwa hawataki kuzungumzia wachezaji ambao hawajawaita, lakini ni muhimu kujibu maswali kuhusu wachezaji walioachwa kwa kutumia wale aliowaita. Yaani anaweza kuzungumzia sababu za kutomuacha Tshabalala bila ya kumtaja kwa kuzungumzia sifa za wachezaji aliowaita kwa nafasi hiyo, ingawa najua ni vigumu kutokana na kiwango cha beki huyo wa kushoto wa Simba na uzoefu wa kutosha alionao kulinganisha na walioitwa, hasa ukizingatia kuwa Tshabalala hana udhaifu mkubwa ambao uliwahi kuwa gumzo kiasi cha kocha kueleweka anaposema hamteui. Kuna maswali hata kwa kipa Metacha Mnata kutoitwa licha ya kuwa katika kiwango cha juu kwa sasa, akiwa na uzoefu baada ya kupata nafasi katika fainali za AFCON nchini Misri na michuano mingine ya klabu. 
Kuna wengi wanaweza kutoa mifano ya huko Ulaya ya wachezaji kuacha, lakini hiyo ilitokea kwa mazingira yao. Ni muhimu kocha wetu akaeleza hayo kwa mazingira yetu. 
Cha kuchekesha zaidi ni vyombo vya habari kukaa kimya, kana kwamba ni haki kwao kutohoji uteuzi wa timu ya taifa. Wapo wanaosema wanaheshimu maamuzi ya mtaalamu na wapo wanaosema tusubiri tuone. Ndayiragije alishaheshimiwa kwa kuachiwa uhuru wa kuteua wachezaji, baada ya hapo amefungua mjadala kuhusu uteuzi wake; iwe tunamheshimu au hatumheshimu kwa sababu lazima uamuzi ufanyike kwanza ndipo ufanyike uchambuzi, ndivyo ilivyo duniani kote. Hatuwezi kukaa kimya eti kwa sababu tunaheshimu maamuzi ya kitaalamu. Halafu timu ikifanya vibaya ndio tuanze kutoheshimu maamuzi ya kitaalamu. Haiwezekani. 
Kocha hawezi kujua hisia za Watanzania kama hawatajadili maamuzi yake. Na akijua hisia za Watanzania atafanya bidi ilia pate matokeo yanayolinmgana na hisia zao, la sivyo itakuwa bora-liende kwa kuwa anamudu genge fulani la watu. 
Kutangazwa kwa timu ya taifa mitandaoni, kunaibua hisia nyingi kama zile zilizowahi kutolewa hadi bungeni; kwamba kuna mawakala wa wachezaji ndio wenye nguvu kuliko kocha, kwamba ndio wanaoamua nani aitwe na nani asiitwe kwa kuangalia nani yuko chini ya menejimenti yao. Na kibaya zaidi, hisia zinajengwa kwamba mawakala na mameneja wa wachezaji ndio wale tunaowasikia kila siku wakifanya uchambuzi redioni na katika televisheni ndio maana husikiii wakipiga kelele.