Hii ndio Yanga Princess sasa!

Muktasari:
- Timu hiyo ilianza kushiriki Ligi Kuu ya Wanawake msimu 2018 haijawahi kuchukua ubingwa zaidi ya kushika nafasi ya pili kwenye msimamo tena msimu wa 2021 ikiwa chini ya kocha Edna Lema 'Mourinho'.
KAMA kuna kitu kinasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa Yanga kwenye soka la wanawake ni timu hiyo kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ambayo imekuwa ikiuota kila siku.
Timu hiyo ilianza kushiriki Ligi Kuu ya Wanawake msimu 2018 haijawahi kuchukua ubingwa zaidi ya kushika nafasi ya pili kwenye msimamo tena msimu wa 2021 ikiwa chini ya kocha Edna Lema 'Mourinho'.
Tangu hapo imekuwa ikishuhudia ubingwa ukienda kwa watani wao Simba Queens na JKT Queens, ambao ni washindani wakubwa kwenye ligi hiyo.
Ukiachana na hilo timu hiyo kwa misimu mitatu mfululizo imekuwa ikisajili wachezaji wenye viwango bora lakini wakishindwa kuwatumia vizuri na kuishia kuwauza na wengine kutimkia timu nyingine ambako wamekuwa wakifanya vizuri.

Msimu 2022/23 timu hiyo ilitimua nyota 13 ikaja kufanya hivyo tena msimu uliofuatia kwa idadi hiyo.
Hata hivyo, haikuishia hapo msimu huu pia ikarudia hivyo ikiwapa mkono wa kwaheri wachezaji kama hao na watatu wakaibukia Simba, Precious Christopher, Wincate Kaari na Saiki Atinuke ambao wamekuwa na msaada kwa wanamsimbazi hao wa kike.
Mwanaspoti imekuchambulia usajili uliofanywa na timu hiyo ambao umeonekana kuwalipa na huenda duru hili la pili ikajitutumua mbele ya mabingwa Simba na JKT.
GOLINI
Kama kuna usajili waliofanikiwa kuufanya Yanga Princess basi ni eneo la golini ambalo awali lilionekana kuwa na changamoto.
Msimu uliopita Yanga Princess ilikuwa na makipa watatu, lakini ni mmoja pekee Safiatu Salifu ndiye aliyekuwa akicheza mara kwa mara kutokana na kupishana viwango.
Msimu huu timu hiyo chini ya Edna Lema 'Mourinho' aliyerejea baada ya kuondoka msimu uliopita, iliachana na Safiatu, raia wa Ghana na kuongeza makipa wawili Mnigeria Rita Akarekor na Mtanzania Zubeda Mgunda ambao wanaonekana kuwa na viwango vinavyofanana.

Eneo la golikipa mara nyingi sio linalofanyiwa mabadiliko mara kwa mara lakini inampa urahisi kocha kubadilisha kikosi ili mmoja kumpumzisha.
Hapa Mourinho anapata urahisi kwenye kikosi chake kutokana na kugawa mechi kwa makipa hao kulingana na mipango yake.
Mgunda ambaye alisajiliwa dirisha dogo akitokea Gets Program inayoshiriki Ligi ya Wanawake amecheza mechi moja dhidi ya Bunda Queens kati ya mbili zilizopigwa kwenye duru hili la pili huku Akarekor akicheza tisa.
UKUTA USISEME
Katika maeneo yaliyokuwa na maboresho makubwa msimu huu basi ni eneo la ulinzi ambalo ndani ya nusu msimu imeongeza mabeki saba.

Kati ya idadi hiyo, wawili ni wageni Igwe Uzoamaka na Angela Chineneri, pacha ya mabeki wa kati ambao wameonyesha kiwango bora wakiingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza.
Waliobaki Wema Maile, Silvia Mwacha (mabeki wa kulia), kutokea Simba Queens, Protasia Mbunda anayemudu kucheza beki zote mbili na hata kiungo, Diana Mnally na Danai Bhobho (kushoto).
Kati ya nyota wote waliosajiliwa, mabeki wa kigeni ndio hadi sasa hawajafanyiwa mabadiliko kwani wamekuwa wakianza kwenye kikosi.
Mwanzoni mwa msimu Wema na Silvia waliotoka Simba walikuwa wakipata nafasi lakini ujio wa Diana na Mbunda unawafanya sasa hivi kuanzia benchini.
Usajili wa Diana, Bhobho na Protasia umeonekana kuwa na manufaa kwa Yanga kutokana na kuwa na uwezo mzuri wa kukaba na kushambulia jambo ambalo wengine walikwama.
Hadi sasa wawili hao wamecheza mechi mbili dhidi ya Bunda Queens, Yanga ikishinda mabao 4-1 na Alliance Girls 0-3 ambapo duru la kwanza wananchi hao walitoka sare zote mbili.
VIUNGO FRESHI
Hili ndio eneo ambalo msimu huu lilikuwa na shida kwa asilimia kubwa kuanzia namba nane na 10.
Maingizo mapya kwenye eneo hilo ni Agnes Pallangyo, Lydia Akoth (Kenya), Aregash Kalsa (Ethiopia) na Adebisi Yemis (Nigeria).
Mwanzoni mwa msimu Yanga ilitambulisha wachezaji wawili Pallangyo ambaye ni kiungo mkabaji na Adebisi, kiungo mshambuliaji.
Pallangyo ni miongoni mwa viungo walioanza vizuri ligi hiyo akitumika kama kiungo mkabaji ambapo mara nyingi alikuwa akishuka chini kusaidia kuokota mipira na kupiga pasi za kwenda kwa washambuliaji.
Katika dirisha dogo Yanga ikaongeza viungo wawili kwenye eneo hilo, Akoth kama kiungo mkabaji na Aregash anayecheza namba 10.
Wawili hao wamecheza mechi moja tu lakini wameonyesha kiwango bora ambacho kimewafanya baadhi ya mashabiki kuanza kutamba juu ya usajili huo.

Aregash ambaye katika mechi yake ya kwanza Yanga ameanza na bao moja kwenye ligi huenda akaziba pengo la Adebisi ambaye hadi sasa hakuwa na mwanzo mzuri akishindwa kuwarahisishia kazi washambuliaji na hadi raundi ya 11 hajafunga bao lolote.
WASHAMBULIAJI
Ile changamoto ya washambuliaji kutofunga au kuwa na muendelezo wa kuchana nyavu sio tu kwa Yanga ya wanaume tu bali hata kwenye timu yao ya wanawake.
Yanga Princess ina washambuliaji watatu Neema Paul ambaye ni msimu wake wa pili kucheza Yanga, Ariet Udong kutokea Ethiopia na Jeaninne Mukandayisenga wa Rayon Sports ya Rwanda.
Udong ambaye yupo nchini tangu mechi za ufunguzi wa ligi akiwateka wananchi kwa kiwango chake licha ya kuwa hakufunga bao lolote lakini umbo lake, nguvu na akili ya kuwatoka mabeki iliwafanya mashabiki kuanza kutaja jina lake.
Mchezaji huyo ni mshambuliaji mwenye sifa za kisasa ambazo kocha yeyote angetamani kuwa naye lakini changamoto ilikuwa kwa viungo wake washambuliaji ambao walikuwa wanashindwa namna ya kumrahisishia kazi ya kufunga.
Hadi sasa ana mabao matatu akiwa ndio kinara wa ufungaji kwa Yanga ingawa ongezeko la wachezaji wapya linaweza kumpa nafuu kama ataendelea alipoishia atakaporejea kutoka kwenye majeraha.
Mukandayisenga ni usajili mwingine uliobamba haraka kwani katika mechi mbili amefunga mabao mawili baada ya kusajiliwa katika dirisha dogo hili.
Nyota huyo huenda akaleta ushindani kwa Udong ambaye ni kama sifa zao zinaendana kutokana na maumbo yao kuwa makubwa, nguvu lakini Udong akiwa na nafasi zaidi ya kutumia akili.

MSIKIE HUYU
Akifichua juu ya usajili huo, mmoja wa viongozi wa Yanga (hakutaka kutajwa jina) alisema sababu ya msimu huu kusajili wachezaji wazawa wengi ni pamoja na kuingiza nyota hao kwenye kikosi cha timu ya taifa 'Twiga Stars'.
"Muda mrefu timu yetu haijapeleka wachezaji timu ya taifa 'Twiga Stars' na kwa matakwa ya kocha Edna Lema alitaka wachezaji hao tukaona pia wanaweza kusaidia timu yetu," alisema kiongozi huyo.