Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HESABU ZA VIDOLE: Kufuzu Afcon kuna makundi hayajajielewa

Muktasari:

  • Hata hivyo, utamu wa michuano hayo umefikia pazuri na tayari mataifa nane yameshafuzu na zinasikilizia mataifa mengine 16 kuungana nayo kuwa 24 zitakazopepetana Morocco kwenye fainali hizo zitakazoanza Desemba 21, 2025.

RAUNDI ya nne ya mechi za hatua ya makundi kufuzu Afcon 2025, Morocco tayari zimepigwa huku Nigeria na Libya zikishindwa kucheza mchezo wao kutokana na mambo yanayoelezwa ni fitna za kisoka walizofanyiana.

Hata hivyo, utamu wa michuano hayo umefikia pazuri na tayari mataifa nane yameshafuzu na zinasikilizia mataifa mengine 16 kuungana nayo kuwa 24 zitakazopepetana Morocco kwenye fainali hizo zitakazoanza Desemba 21, 2025.

Kuna mataifa ambayo yalipewa nafasi kubwa ya kufuzu fainali hizo lakini kwa sasa hali inaonekana kuwa mbaya na ilivyo ni hadi mechi za mwisho kuamua zitakazofuzu.

Hapa tunakuchambulia makundi ya vigogo waliopewa nafasi lakini hazieleweke pamoja na makundi ambayo michezo ya mwisho ndiyo itakayoamua.


KUNDI A

Yoyote inaweza ikafuzu kama tu itachanga vyema karata kwenye mechi mbili zilizobaki. Tunisia inaongoza ikiwa na pointi saba, Comoro inafuata na sita, Gambia tano na Madagascar mbili.

Hata hivyo, kati ya mechi hizo, Tunisia inahitaji ushindi wa mechi moja tu, huku ikiziombea Comoro na Madagascar zitoke sare ili kufuzu.

Hii ni kwa sababu, Comoro na Tunisia zimepishana pointi moja na ndizo zenye nafasi kubwa ya kufuzu ikiwa zitashinda mechi zilizobaki.

Kilichoshangaza kwenye kundi hili ni, licha ya Tunisia kupewa nafasi kubwa ya kufuzu kutokana na ubora wake na ukongwe, ilijikuta ikipoteza nyumbani nyumbani dhidi ya Comoro ikiwa ni mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka 30.

Gambia pia ina nafasi ya kufuzu kama itashinda mechi zote mbili, dhidi ya vinara Tunisia na Comoro.

Madagascar pia ina nafasi ya kufuzu kama itashinda mechi zote mbili na itafikisha pointi nane, huku ikiziombea Tunisia au Comoro mmoja apoteze zote.


KUNDI D

Hapa kuna kasheshe. Nigeria ilisusia mchezo dhidi ya Libya kwa kudai ilifanyiwa figisu kuanzia uwanja wa ndege. Uamuzi bado haujatolewa iwapo mchezo huo utachezwa au kufutwa na Libya kupewa ushindi.

Si kitu kwa Nigeria. Inaonyesha inajiamini ndiyo maana ilikuwa tayari hata kugawa pointi hizo kwa Libya ili isicheze nayo licha ya kudai fitna zimesababisha.

Kwenye kundi hilo, Nigeria ndiyo kinara ikiwa na pointi saba, ikicheza mechi tatu, ikifuatiwa na Benin yenye pointi sita na michezo minne, Rwanda pointi tano baada ya michezo minne na Libya inaburuza ikiwa na pointi moja na michezo mitatu.

Inaonyesha Nigeria hata ikipokwa pointi, inatakiwa kushinda mechi mbili tu kati ya tatu na itafikisha pointi 13 ambazo hazitaweza kufikiwa na yoyote kwenye kundi hilo.

Benin pia itafuzu kama itashinda mechi zote mbili kwani itafikisha pointi 12 na tofauti na Nigeria, nyingine hazitaweza kuifikia.

Hata hivyo, hali ni mbaya kwa Rwanda na Libya ambazo ili zifuzu, lazima zishinde mechi zote zilizobaki zitakapokutana na Nigeria na Benin.


KUNDI F

Hili ni moja kati ya makundi yaliyoshangaza wengi. Hadi sasa Ghana inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama mbili tu baada ya michezo minne.

Angola tayari imefuzu ikiwa na pointi 12 na imesaliwa na michezo miwili. Pointi hizo haziwezi kufikiwa na Niger na Ghana, labda Sudan ambayo itafikisha pointi 13 na kama Angola itapoteza mechi zake mbili zilizobaki.

Sudan inapewa nafasi kubwa ya kuifuata Angola kwa sababu ina pointi saba na ikishinda mechi moja tu kati ya mbili ilizobakiwa nazo itakuwa imefuzu moja kwa moja.

Ghana inaweza ikafuzu lakini kama tu itashinda mechi zote na kufikisha pointi nane, huku ikiombea Sudan ipoteze mechi zote itakapokutana na Niger na Angola.

Sudan imeonekana kuwa timu iliyoshangaza zaidi katika kundi hili baada ya kuichapa Ghana mabao 2-0 katika mchezo wa marudiano baada ya ule wa kwanza uliopigwa Ghana kumalizika kwa suluhu.


KUNDI H

Hapa DR Congo tayari imeshafuzu. Ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Tanzania uliifanya ifikishe pointi 12, huku msala wa nafasi ya pili ukiachwa kwa Tanzania, Guinea na Ethiopia.

Hata hivyo, vita kubwa inaonekana ni kwa Tanzania na Guinea ambazo zinakaribiana pointi na Guinea ina sita na Stars nne na zote zimebakisha mechi mbili na moja ikizikutanisha zenyewe.

Ikiwa Tanzania itashinda dhidi ya Guinea na Ethiopia itakuwa imefuzu moja kwa moja sawa na ilivyo kwa Guinea kama itashinda zote. Guinea ikishinda zote itakuwa na pointi 12 wakati Tanzania itakuwa na 10.

Kwa asilimia kubwa timu itakayoungana na DRC huenda ikajulikana katika mechi ya mwisho kati ya Guinea na Tanzania. Kwa upande wa Ethiopia yenye pointi moja, itahitaji kushinda mechi zote mbili zilizobakia ili ifikishe pointi saba kisha kuiombea Guinea isishinde hata mechi moja itakapokutana na Tanzania na Congo. Hata hivyo, hesabu zinaonekana kuwa ngumu, kwani mechi mbili ambazo Ethiopia itamaliza nazo ni dhidi ya Congo ugenini na Tanzania nyumbani.


KUNDI G

Hapa kinara Ivory Coast yenye pointi tisa inahitaji kushinda mechi moja tu ili kufuzu na shughuli ibaki kwa Zambia na Sierra Leone zinazogombania nafasi ya pili.

Zambia ina pointi saba wakati Sierra Leone ambayo mechi yao ya mwisho ilichapa Ivory Coast ina nne.

Ikiwa Sierra Leone itashinda mechi zake mbili zilizobakia itafikisha pointi 10 wakati Zambia itafikisha 13.

Hata hivyo, uwezekano wa Sierra Leone na Zambia kushinda mechi zao mbili zilizobakia ni mgumu kwani mechi ya kwanza kwa Sierra Leone itakuwa ni dhidi ya Chad ambayo hapo awali ilitoka nao sare wakati Zambia ikikutana na Ivory Coast.

Ikiwa wababe hawa watashinda mechi zao zijazo huenda kundi likaamuliwa katika mechi za mwisho na zitakutana zenyewe.


KUNDI I

Hadi sasa hakuna timu iliyofuzu katika kundi hili ingawa Msumbiji na Mali ndizo zinapewa nafasi kubwa kwa kuwa zinaongoza kundi.

Timu hizi zote zina pointi nane kila moja, huku Msumbiji ikiongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa  ikifuatiwa na Mali.

Timu ya kwanza kufuzu huenda ikapatikana baada ya wababe hawa kukutana kwenye mechi ijayo na zitakutana huku Msumbiji ikiwa nyumbani.

Mmoja kati yao akishinda itakuwa imefikisha pointi 11 ambazo zitamwezesha kufuzu ingawa kuna hatihati ya mmoja wao kuangukia pua na kushindwa kwenda Morocco.

Hatihati hiyo inatokana na Guinea Bissau ambayo ina pointi nne na kama itashinda mechi zote itafikisha 10, hivyo timu itakayopoteza kati ya Mali na Msumbiji kisha ikatoa sare ama kufungwa katika mechi ya mwisho itakuwa imeipa nafasi Guinea Bissau kufuzu kwa pointi 10.