Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HERE WE GO! Maajabu ya Fabrizio Romano, sikio ardhini

HERE WE GO! Maajabu ya Fabrizio Romano, sikio ardhini

WAZUNGU wana misemo mbalimbali inayovutia. Celine Dion aliwahi kuimba wimbo uliosema ‘Kama kuta zingeongea’‚ Halafu James Hardley Chase, mwandishi mahiri wa vitabu wa zamani aliwahi kuandika kitabu kilichosema ‘Fanya mzoga utembee’. Chase huyo huyo aliwahi kuandika kitu kilichoitwa ‘Weka sikio ardhini usikilize’.

Katika ubora wao, kuna baadhi ya watu wanasababisha kuta ziongee. Wanasababisha mzoga utembee. Lakini ni wachunguzi kiasi kwamba wanawema kutega sikio ardhini kwa utulivu mkubwa kiasi cha kusikia mazungumzo yanayoendelea chini ya ardhi.

Katika uandishi wa habari kuna habari ambayo lazima ipatikane. Ni lazima na hakuna mjadala. Unatumia mbinu zozote za ujasusi kupata habari hizo. Unapata mazungumzo ya watu wakati haukuwapo. Unasikiliza mazungumzo ya watu wakati haukuwapo.

Wakati mwingine yote haya yanatokana na pesa. Msukumo wa pesa unasababisha haya. Fabrizio Romano ana mtandao mkubwa kutoka kwa baadhi ya watu wa makao makuu wa klabu zote kubwa na ndogo barani Ulaya na kwingineko.

Inasemekana wote hawa wapo katika malipo yake. Romano anajua ambacho kinaendelea katika Headquarters za Manchester United pale jijini Manchester. Inawezekana katika mzunguko ule ule wa watu ambao nimewataja jana. Labda mwanasheria, labda mwakilishi wa mazungumzo, labda daktari wa klabu ambaye atahusika kumpima afya mchezaji mtarajiwa.

Fanya hawa watu waongee ukweli wao. Kuna habari ambayo Mendes anaweza kumwambia Romano kuhusu mteja wake, lakini kuna habari ambazo hawezi kujua hasa ile ambayo inahusu fikra za mabosi wa timu husika.

Kwa mfano, inawezekana kabisa Manchester United inamtaka mteja wa Mendes. Lakini inawezekana pia inamtaka mchezaji anayemilikiwa na Mino Raiola. Inawezekana kuna nafasi moja tu baina ya wachezaji hao wawili. Inawezekana United imewasiliana na Raiola pamoja na Mendes ambao wote wamemwambia Romano.

Lakini kati ya hawa hawajui hasa klabu itaamua kwenda kwa mchezaji gani baina ya hao wawili. Hapo ndipo Romano pia analazimika kuwa na watu wa ndani. Utasikia tu Romano anatuambia pale Twitter ‘Manchester United imeamua kuachana na mpango wa kumchukua Frenkie de Jong na sasa itapeleka macho yake kwa Ruben Neves wa Wolves‚‘. Hii itakuwa ni habari ambayo Romano ameipata kutoka kwa watu wa ndani.

Pia wakati mwingine timu inatoswa katika dau lake la kwanza dhidi ya mchezaji fulani. Inapofikiria kurudi tena na dau la pili ni kitu ambacho wakala wa mchezaji huenda asifahamu. Wanaojua kwamba watarudi na dau la pili au wataachana na mpango wenyewe ni viongozi.

Hapo ndipo Romano anaegesha sikio lake kwa umaridadi mkubwa. Utasikia tu, anatuambia ‘Manchester United imekataliwa katika dau lake la kumtaka De Jong na sasa inafikiria kurudi na dau la pili la pauni 67 milioni’.Habari hii inakuwa imevuja klabuni.

Lakini hapa kuna pande tatu. Kuna upande wa wakala, upande wa klabu inayonunua pia upande wa klabu ambayo inauza. Kwa habari kama hii, Romano lazima awe ameegesha sikio lake ndani ya Barcelona. Hapo ni lazima apate maoni ya Barcelona.

Yaani lazima ajue ni dau gani hasa linaweza kuwashawishi Barcelona kumuuza hata kama hawatafika katika dau la awali la pauni 75 milioni ambalo walikuwa wanalitaka. Jambo hili lazima Romano aegeshe sikio lake kutoka kwa watu wa ndani.

Anaweza kwenda mbali zaidi na kujua ni mchezaji gani ambaye Barcelona wanafikiria kumchukua kwa ajili ya kuziba dau la De Jong. Hii ndio tofauti yake na wanahabari wengine. Amewekeza zaidi katika watu wa ndani ya klabu.

Lakini achilia mbali watu wakubwa katika klabu, Romano anaweza kuwa amewekeza katika watu wa kawaida kabisa klabuni. Katibu mukhtasi, mpiga picha wa klabu, mfagizi na wengineo. Hawa ndio wanaoshughulika na shughuli za kila siku za klabu.

Kwa mfano, mpigapicha lazima ataambiwa ajiandae kwa sababu keshokutwa Gabriel Jesus atapigwa picha akiwa na jezi ya klabu baada ya kutoka katika vipimo vya afya. Unahitaji kuwa na mpigapicha kwa ukaribu zaidi.

Katibu mukhtasi ndiye ambaye anapokea faksi zote za klabu na kuwapelekea mabosi. Analazimika kuwa na jicho la mwewe katika kila karatasi kama ameonyeshwa pesa na Romano. Huu ndio ukweli unaohusu mzunguko wa maisha ya klabu.

Wakati alipofika Arsenal mwaka 1996, kocha wa Arsenal, Arsene Wenger aliwaambia wachezaji wake mastaa umuhimu wa kuwaheshimu wafanyakazi wote wa klabu bila ya kujali nafasi zao kwa sababu wanashika siri nyingi za klabu. Ni katika mambo kama haya.

Kwa Romano ni lazima awe na mzunguko huu wa watu pale Arsenal, Chelsea, Liverpool, Tottenham, Wolves, Manchester City na kwingineko. Akijumlisha habari zake kutoka kwa mzazi wa mchezaji, au mchezaji mwenyewe, wakala, mfanyakazi wa ndani wa klabu, inakuwa rahisi kwake kuja na habari ya uhakika.

Romano anaweza asiwe na uhusiano na wakala wa Raphinha, lakini anaweza kuzipata habari za Raphinha kupitia kwa watu wake wa ndani wa Leeds United au Chelsea, Barcelona na Arsenal ambazo zimekuwa zikimuwania staa huyo wa kimataifa wa Brazil.

Endapo atazikosa habari hizo kwa wakala au watu wa ndani wa klabu bado Romano ana mahali pa kuzipata habari hizo. Kesho nitakwambia ni wapi kwingine ambapo Romano anaweza kuzipata habari za ndani za uhamisho wa mchezaji kiasi cha kuja kututambia kwa uhakika kabisa kuhusu uhamisho wa staa fulani akiwa na kauli yake maarufu inayotisha sasa kuhusu uhamuisho ya ‘Here we Go.”

ITAENDELEA KESHO