HERE WE GO: Maajabu ya Fabrizio Romano, sikio ardhini -1
NILIKUWA katika hoteli ya Royal Palm jijini Accra Ghana Februari 2007. Nisikilize vema. Sikuwa nimefikia hotelini hapo kabla. Nilikuwa nakwenda kumtembelea Rais wa wakati huo wa TFF, Leodeger Tenga ambaye alikuwa mmoja kati ya watu wazito CAF. Michuano ya Afcon ilikuwa ikiendelea Ghana.
Katika hoteli hii walikuwa wamefikia watu wazito. Jose Mourinho, ambaye alikuwa amefukuzwa na Chelsea. David Dein, Makamu wa Rais wa Arsenal. Issa Hayatou, aliyekuwa Rais wa CAF. Na vigogo wengine mbalimbali wa soka Afrika na duniani.
Bahati iliyoje, nikiwa nimekaa katika kochi na baadhi ya waandishi wa nchi mbalimbali za Afrika akaingia Abeid Ayew Pele. Sijui alikuja kufanya nini. Nilimtazama kwa jicho la husuda. Abeid, bishoo kama alivyo. Alikuwa ana hereni mbili katika masikio yake. Mwili wake ulikuwa umetakata. Mavazi nadhifu. Hakuonekana kama mstaafu miongoni mwa wastaafu tuliowazoea barani Afrika.
Umri ulikuwa umemtupa lakini alionekana kama baharia. Hakutaka kuzeeka. Nje alikuwa amepaki gari la aina ya Hammer. Kila mtu alimuita kwa jina lake. ‘Peleee’. Mwingine aliita ‘Abeid’. Kuna kilinishangaza zaidi.
Ilikuwa mara yangu ya kwanza kumuona ‘live’ Abeid Pele. Kwanini nisipige naye picha? Kwanini hasa? Nilinyanyuka nikamfuata. Tukapiga picha. Kilichonishangaza ni kwamba nilijikuta ni peke yangu ambaye nilikuwa nimepiga picha na Abeid.
Waandishi wengine walikuwa wanapiga naye soga za kawaida huku wakimtania. Mwandishi mmoja alikuwa akimlalamikia Abeid kwanini hawakuonana jana usiku. Nikagundua kitu. Kitu ambacho kimenifanya nimfikirie Mwandishi maarufu wa habari za uhamisho wa mastaa wa soka wanaotamba duniani kwa sasa, Fabrizio Romano.
Romano mwenye umri wa miaka 29 ana wafuasi 8.3 milioni katika mtandao wa Twitter peke yake. Ana wafuasi 7.8 milioni katika mtandao wa Instagram. Anabakia kuwa Mwandishi anayeaminika zaidi katika katika masuala ya uhamisho wa wachezaji barani Ulaya na duniani kote.
Romano anaonekana kufanya maajabu katika masuala ya habari ya soko la uhamisho duniani. Kila mara yupo. Kila taarifa anayo. Bahati nzuri taarifa zake ni za uhakika. Nitaanza kukupa silaha moja moja ambazo Romano anazitumia kufanikisha mambo yake.
‘Here we go’ ni kauli yake maarufu ambayo haiji bure. Nimekuletea mfano wa mimi na Abeid Pele kujaribu kuanza kukuelewesha namna ambavyo waandishi wenzetu wana mahusiano makubwa na mastaa. Wanaishi nao kila siku na wamewazoea.
Binafsi akili yangu ilinituma kupiga picha na Abeid Pele, lakini waandishi wenzangu wanakutana na Abeid Pele kila kukicha. Wanakutana na Abeid Pele katika michuano mbalimbali ya soka, wanakutana naye katika mikutano ya uchaguzi, wanakutana naye katika makongamano na semina. Wanakutana na Abeid kila mahala na hawana mpango wa kupiga naye picha tena.
Miongoni mwa waandishi wa namna hii yupo Fabrizio Romano. Achilia mbali Abeid Pele yeye atakutana na Fransesco Totti, Ronaldo de Lima, Lionel Messi, Cristiano Ronaldo, Kylian Mbappe na wengineo. Haya ndio maisha yake ya kila siku.
Romano alipoamua kujikita katika masuala ya uhamisho wa mastaa wa soka ni kwamba sababu anafahamiana na wachezaji, mawakala, wazazi wa wachezaji, mabosi watendaji, wafanyakazi wa hoteli na kila mtu. Hapa ndipo kazi yake inapokuwa rahisi.
Kwa mfano, ni rahisi kwa Romano kumuuliza Abeid Pele kuhusu hatma ya Jordan Ayew katika kikosi cha Crystal Palace na akapata habari za ndani. Pele hawezi kufunguka kwangu kwa sababu ndio kwanza ameniona. Hawezi kuniamini. Lakini anaweza kumuamini Romano ambaye amebadilishana namba miaka sita iliyopita na wamekuwa wakichati mara nyingi.
Pele anaweza tu kumwambia Romano kwamba kuna ofa ya Atletico Madrid kwenda kwa mwanae. Akampa maelezo kwamba wameshakubaliana kuhusu mshahara na baadhi ya vipengele vipengele vingine.
Uzuri wake ambao unamjengea imani kutoka kwa watoa taarifa wengine (Sources) ni kwamba Romano haaniki watoa taarifa wake hadharani. Umewahi kuona Romano anataja mahala alipopata hizo taarifa? Hapana!
“Arsenal are confident on Youri Telemans to join the club as the next signing. Official bid will be improved in order to reach full agreement with Leicester City”.
Unajua ni wapi ambapo Romano anaweza kuwa ameipata hii habari? Nimekupa chanzo cha kwanza kabisa. Wazazi au ndugu wa mchezaji mwenyewe. Inawezekana akawa na urafiki wa karibu na mchezaji au ndugu ambaye anamuelezea dili lilipofikia.
Wakati mwingine inakuwa ngumu kwa klabu zote mbili kumueleza Romano habari zozote za maana, lakini leo nimekupa chanzo cha kwanza cha Romano. Ndugu. Ni kama ambavyo nimekupa uhusiano niliouona kati ya Abeid Pele na Waandishi wa Habari. Kuna mtu ambaye anaweza kujua nyendo cha Jordan na Andre Ayew zaidi ya baba yao mzazi? Tofauti ni kwamba wazazi wa mastaa wengi wa soka la Tanzania huwa hawana uhusiano wa karibu na watoto wao. Walau siku hizi kuna Mameneja au mawakala ambao Romano angeweza kufanya nao kazi Tanzania lakini maelfu ya wanasoka walio Tanzania hawana mawakala wala Mameneja.
Ni ngumu kwa Romano kushughulikana na wazazi wa wachezaji kwa sababu wanakuwa hawajui chochote kinachoendelea katika mazungumzo ya watoto wao na klabu zao au klabu wanazotarajiwa kuhamia. Nimekudokeza kidogo kuhusu maajabu ya mtu anaiyeitwa Fabrizio Romano ambaye ameiteka dunia ya soka katika suala la uhamisho wa wachezaji.
Kwenye Mwanaspoti la kesho nitakuletea maajabu mengine ambayo Romano anaweza kuwa anayatumia katika maajabu yake. Usinikose kesho.