Prime
O Hexa ni ndoto inayowatesa Brazil kama la Decima ilivyowatesa Real Madrid
Muktasari:
- Sayansi haikamiliki kama hakuna maneno ya kilatini na kigiriki...hata neno lenyewe sayansi ni la kilatin, scientia. Lakini kabla ya kuitwa kilatini, sayansi iliitwa kigiriki, Philosophiæ Naturalis.
Sisi waswahili tunaamini Kiingereza ndiyo lugha ya kisomi na ustaarabu. Lakini waingereza wenyewe na wazungu wenzao wanaamini tofauti, au angalau katika sehemu ya maisha yao kuna wakati waliamini tofauti...kwamba lugha za kisomi na ustaarabu ni kilatini au kigiriki.
Unaweza kushangaa lakini huo ndiyo ukweli.
Sayansi haikamiliki kama hakuna maneno ya kilatini na kigiriki...hata neno lenyewe sayansi ni la kilatin, scientia. Lakini kabla ya kuitwa kilatini, sayansi iliitwa kigiriki, Philosophiæ Naturalis.
Kitabu cha Sir Isaac Newton, ambacho ndicho msingi wa sayansi, kinaitwa Philosophiæ Naturalis Principia Mathematica.
Japo yeye alikuwa muingereza lakini hakutumia kiingereza kwenye kazi zake kwa sababu hakuamini kama kiingereza kinatosha kuwa lugha ya sayansi.
Sheria haikamiliki bila kuwa maneno au misemo ya kilatini na kigiriki.
Waliosoma sheria wanajua misemo kama Actus reus (sheria ya hatia), Mens rea (akili za kihalifu) na kadhalika.
Na hii ni kwenye kila kitu...hadi majina ya nchi na miji mingi. Kwa mfano Uingereza inaitwa Britain, hili ni jina lenye asili ya kilatini la Britannia.
Hata miji yake mingi kama London, ni Londinium au Londonia, kilatini. Na hii haiishi hapo...hata kwenye timu za mpira za Uingereza kuna ulatini mwingi sana.
Kwa mfano, kaulimbiu za baadhi ya klabu za England zimeandikwa kwa kilatini.
Manchester City ni “Superbianin prelio” yaani fahari katika mapambano (pride in battles). Everton ni Nil Satis Nisi Optimum, yaani Hakuna zaidi ya kilicho bora na uzuri wake wa kujitosheleza.
Hata Arsenal, kwa miaka yote huko nyuma kaulimbiu yao ilikuwa ya kilatini, Victoria Concordia Crescit, yenye maana ya ushindi huja kutoka kwenye utulivu. Waliacha kuitumia msimu wa 2001/02.
Kwa kifupi, kilatini ndio lugha iliyozaa lugha nyingi za Ulaya, aidha moja kwa moja au kwa kukopa maneno mengi.
Kiitaliano, Kihispaniola, Kireno na hata kifaransa, ni lugha za muendelezo wa moja kwa moja wa kilatini.
Hata namba wanazotumia ni aidha za kilatini au kigiriki...na hapa ndipo kwenye mada yetu ya leo.
Mwaka 2002 Real Madrid ilishinda ubingwa wa tisa wa Ulaya, kwa kuwafunga 2-1 Bayer Leverkusen ya Ujerumani. Ubingwa huu wakauita LA NOVENA...yaani wa tisa.
Novena ni namba tisa, kwa kilatini na lugha zake zote zitokanazo.
Kutoka Novena inakuja Decima...yaani kumi.
Novena ndio iliyozaa Novemba...na Decima ndio iliyozaa Disemba.
Kiasili Novemba sio mwezi wa kumi na moja kama ilivyo sasa...ni wa mwezi wa tisa.
Na Disemba sio mwezi wa kumi na mbili, ni mwezi wa kumi.
Hii ni kwa mujibu wa kalenda ya zamani ya walatin (warumi).
Kalenda hiyo ilikuwa na miezi 10 tu...mwaka ulianzia mwezi Machi na uliishia mwezi Disemba.
Baadaye kalenda hii ikabadilishwa na kuja kalenda mpya yenye miezi 12...ndipo mwezi Januari na Februari ikaongezwa..
Hapo ndipo Novemba na Disemba zikaangukia kuwa ya miezi ya 11 na 12 mtawalia.
Samahani kwa kutoka nje ya mada kidogo...lakini nadhani umepata kitu angalau.
Turudi kwenye mada yetu, kwa hiyo Real Madrid wakaanza kuitafuta La Decima, yaani ubingwa wa 10.
Kwa hiyo Real Madrid baada ya ubingwa wa tisa, safari mpya ya kuutafuta ubingwa wa kumi ikaanza.
Yaani baada ya La Novena, wakaanza kuitafuta La Decima.
Mashabiki wakaimba La Decima, vyombo vya habari vikaitikia La Decima...wimbo ukawa ni La Decima kila mahala.
Kuanzia mwaka 2002, ndoto ya La Decima iliwatesa na kuwaumiza sana.
Rais wao, Florentino Perez,.akatimiza mabilioni ya pesa kununua wachezaji nyota ili kuigeuza ndoto ya La Decima kuwa kitu halisi...lakini haikuwa.
Waliendelea kuteseka hadi 2014 ndipo wakafanikiwa...na baada ya hapo mambo yakawa rahisi...rahisi sana!
Yale mateso waliyopitia Real Madrid ndiyo wanayopita Brazil kwa sasa.
Wamechukua ubingwa wa dunia mara tano...wanaongoza.
Katika lugha ya kigiriki, tano pénte...utakumbuka Pentagon, lile umbo la pembetano...wakati wa somo la Hisabati.
Kutoka Pente ni Hexa...yaani SITA. Pia utakumbuka Hexagon, lile umbo la pembesita.
Kwa hiyo Brazil baada ya kushinda ubingwa wa tano (e penta) mwaka 2002, waaka kuota ubingwa wa sita, O Hexa.
Hii ni ndoto iliyoishi kwenye vichwa vyao tangu 2002...na bado inawatesa.
2026 wako Marekani, ardhi waliyoshindia ubingwa wao wa nne mwaka 1994.
Watu wote wanataka kuwa mabingwa wa dunia...lakini ndoto ya O Hexa inawatesa sana Brazil.
Walipoandaa mashindano mwaka 2014, walitarajia wangeifikia ndoto yao, lakini badala yake wakaruka kutoka O Hexa yaani SITA, hadi O Eptá, yaani SABA, kile kipigo cha 7-1 kutoka Ujerumani.
Yaani walifika saba kabla kuifikia ndoto yao ya SITA.
Tusubiri kuona 2026...ndoto itatimia au wataendelea kuteseka?