Hawa wanarudi nyumbani

Friday June 11 2021
morinho pic

LONDON, ENGLAND. BAADA ya Mauricio Pochettino kuondoka nyumbani Tottenham kwa muda, sasa taarifa zimefafanua kwamba ana asilimia nyingi za kujiunga tena na Spurs kwani ana hati hati ya kuondoka PSG kwa sababu hana maelewano mazuri na mabosi wa timu hiyo.

Hata hivyo, ikiwa Pochettino atarejea Spurs hatakuwa kocha wa kwanza yeye kufanya hivyo. Kuna makocha wengi wakubwa waliowahi kuondoka kwenye timu na baadaye wakarudi tena. Hawa hapa makocha watano waliorejea tena kwenye timu zao za zamani.


Jose Mourinho

Baada ya kupata jina la Special One kwa kufanya makubwa pale Real Madrid na Inter Milan aliamua kurejea tena Chelsea mwaka 2013.

Aliporejea tena kwenye kikosi hicho aliwawezesha kuchukua tena ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 2014-15, akiwa mafundi kibao kama Eden Hazard, Diego Costa na Cesc Fabregas.

Advertisement

Lakini alifungashiwa virago Desemba mwaka 2015 baada ya timu kuwa kwenye hali mbaya. Aliondoka timu ikiwa nafasi ya 16.

Mourinho alijiunga na Chelsea kwa mara ya kwanza mwaka 2004 na akadumu hadi mwaka 2008 kisha akapita Inter Milan, Real Madrid kabla ya kurejea tena Chelsea 2013.


Kenny Dalglish

Kwanza alianza kufanya makubwa akiwa akiwa mchezaji ambapo alizichezea timu mbili, Liverpool na Celtic jumla ya mechi 850 na akafunga mabao 345. Hii ilikuwa ni kuanzia mwaka 1960 hadi miaka ya mwishoni mwa sabini.

Baada ya kustaafu soka aliingia kwenye masuala ya ukocha ambapo aliajiriwa Liverpool. Akiwa kocha aliiwezesha Liver kuwa timu tishio kwenye soka la England kuanzia miaka ya 1980, aliiwezesha kushinda mataji matatu ya Ligi Kuu ambapo wakati huo ilijulikana kama Daraja la Kwanza na Kombe la FA mara mbili.

Baada ya mafanikio hayo aliondoka mwaka 1991 akapita baadhi ya timu za hapo hapo England na mwaka 2011 baada ya Roy Hodgson kufungashiwa virago jamaa ilimbidi achukue tena mikoba ya kuinoa Liverpool lakini alidumu kwa miezi 18 tu, hata hivyo aliiwezesha kutwaa Kombe la Carabao na alifanya maboresho kwenye kikosi ikiwa pamoja na kumtengeneza Luis Suarez aliyeimarika na kuchukua nafasi ya Fernando Torres.


Zinedine Zidane

Baada ya mafanikio ya kuchukua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu mitatu mfululizo jamaa aliamua kuondoka zake kwenda kupumzisha akili.

Baada ya kuondoka nafasi yake ilizibwa na makocha wawili wakubwa kwenye vipindi tofauti ambao ni Julen Lopetegui na Santiago Solari.

Lakini hali ilikuwa mbaya na Rais wa Madrid Florentino Perez aliamua kumvuta tena Machi 2019 ili aende kuokoa jahazi na aliwawezesha kushinda taji la La Liga msimu wa 2019-20. Hata hivyo. ameamua kuondoka tena baada ya msimu uliopita kuondoka mikono mitupu.


Jupp Heynckes

Heynckes aliajiriwa Bayern Munich kwa mara ya kwanza mwaka 1987 na akaiwezesha kuchukua mataji matatu katika miaka minne aliyohudumu. Baada ya hapo alijiunga na Athletic Bilbao, Tenerife na Real Madrid.

Kisha akapata nafasi ya kurejea tena Munich mwaka 2009 kama kocha wa muda na baadaye akajiunga na Bayer Leverkusen mwaka 2011. Alirejea rasmi Munich baada ya msimu wa mwaka 2010/11 kumalizika na kwenda kuchukua nafasi ya Louis van Gaal aliyekwenda kuifundisha timu ya taifa ya Uholanzi.


Harry Redknapp

Baada ya kuipandisha daraja Portsmouth aliamua kuachana nayo mwaka 2004 kwa kuwa hakuwa na maelewano mazuri na mmiliki Milan Mandaric.

Mara tu baada ya kuondoka alijiunga na Southampton aliyokuwa na kazi ya kuhakikisha inabaki Ligi Kuu, hilo halikufanikiwa kwani ilishuka daraja na yeye akaamua kuachana nayo Desemba 2005.

Baada tu ya kuondoka Southampton Mwenyekiti wa Portsmouth, Rupert Lowe alisema Redknapp amefikia makubaliano na timu hiyo kwamba yupo tayari kurejea kuifundisha. Kurejea kwake mara ya pili kulikuwa na mafanikio sana kwani aliiwezesha kushinda taji la FA mwaka 2008 kabla ya kuondoka tena kujiunga na Tottenham mwaka mmoja baadaye.

Advertisement