Hawa kina Folz kuna wakati wanaonewa tu!
Muktasari:
- Huo ulikuwa mchezo wa kwanza kwa kocha Romain Folz ugenini katika Ligi Kuu akiwa na kikosi hicho dhidi ya timu iliyorejea katika ligi hiyo baada ya kushuka misimu miwili iliyopita.
YANGA imeangusha pointi mbili za kwanza katika Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kulazimishwa suluhu na Mbeya City, jijini Mbeya.
Huo ulikuwa mchezo wa kwanza kwa kocha Romain Folz ugenini katika Ligi Kuu akiwa na kikosi hicho dhidi ya timu iliyorejea katika ligi hiyo baada ya kushuka misimu miwili iliyopita.
Mara baada ya mechi hiyo kuna baadhi ya mashabiki walikaririwa wakiimba hawamtaki kocha Folz na kutaka aondoke Yanga. Pia katika mitandao ya kijamii kuna mijadala mingi kuhusu kocha huyo, ikielezwa kuwa timu kucheza hovyo ndiko kunakowakera mashabiki. Timu haijapoteza mechi yoyote kati ya 10 ilizocheza chini ya kocha huyo, zikiwamo tano za kimashindano na tano za kirafiki.
Hata hivyo, kuna wakati ukiwauliza wanaompinga na kumkataa Folz wanataka aondolewe Yanga kwa sababu zipi za maana? Hatakuwa na majibu kwa sababu, wengine wanaenda na upepo bila kufikiria kwa kina. Na sio mashabiki wa Yanga tu, hata wa klabu nyingine wanaposhinikiza kocha atoke huwa wanaangalia vitu gani vya maana kuushinikiza uongozi uwatimue makocha wa timu hizo?
Ngoja nitoe darasa dogo, kisha ndipo tuone kama ni kweli mashabiki hao wa Yanga na wengine ambao wamekuwa wepesi kutoa shinikizo kwa viongozi, kutimuliwa kwa makocha wana sababu za maana au wanafuata upepo kuushinikiza viongozi wa klabu kuwafukuza makocha bila kujua wakati mwingine wanazitia hasara klabu hizo na kupoteza mwenendo mzuri wa timu kwa wachezaji!
Ipo hivi. Pre-Season ndicho kipindi pekee ambacho timu hupata nafasi ya kujiandaa kulingana na malengo ya timu kwa msimu husika.
Ni kipindi ambacho kocha hukiandaa kikosi kwenye maeno matano ikiwamo; utimamu wa mwili (physical fitness), mbinu (tactical), ufundi (technique), kiakili (psychology) na kijamii (social).
Hizo nguzo tano huwa ndio msingi wa maandalizi na timu ikionekana baada ya kutoka katika maandalizi itapimwa kwenye maeneo hayo na hapo ndipo unapoweza kufanya tathmini kitaalamu kutokana na tabia za timu ndani ya kiwanja.
1. Utimamu wa mwili: Utapima ufanisi wa timu ndani ya kiwanja kwa dakika za mchezo katika matukio yanayohitaji uwajibikaji kama kukimbia, kugombea mpira juu au chini usahihi wa utekelezaji wa majukumu bila kujali mchezo uko dakika ya ngapi.
2. Mbinu: Hapa tutaitazama katika maeneo matano - timu ina mpira, timu haina mpira, timu imepoteza mpira, timu imepokonya mpira na mipira ya kutenga. Hapa tutazitazama tabia za timu kwenye kuyaendea matukio haya, tusipoziona ndio tutamgeukia mwalimu na kuhoji maandalizi yake.
3. Ufundi: Hili pia ni jukumu la kocha kuhakikisha anaboresha viwango vya wachezaji kwa kuhakikisha eneo la ufundi linakuwa bora kwa mchezaji mmoja mmoja. Na kama haviko sawa pia ni swali linarudi kwa kocha mhusika.
Kwa wapenzi au mashabiki wao humpima mwalimu au timu kulingana na utaratibu wao kiuchezaji kwa msimu uliopita au aina yao ya uchezaji (style of play).
Au philosophy ya timu na ndio huwa kipimo cha kocha mbele ya wapenzi wa timu na wapenzi wa mchezo kwa ujumla.
Nawaelewa wapenzi wa Yanga wanapohoji uwezo wa mwalimu sababu wanaipima timu yao msimu huu na ilivyokuwa msimu uliopita. Wanachokitaka ni burudani waliyokuwa wakiipata msimu uliopita na sio matokeo peke yake.
Swali la kujiuliza, je kocha aliyekabidhiwa timu anaamini katika namna ile ambayo wapenzi wanaamini? Je, viongozi wanatumia vigezo gani kumpitisha kocha?
Kwani nakumbuka baadhi ya kesi za makocha waliondolewa kwenye timu kwa kushindwa kuendana na mahitaji ya mashabiki na sio kuisaidia timu kushinda.
Simba tuliwahi kufundishwa na kocha kutoka Uganda, Moses Basena, timu ilikuwa inashinda ila watu hawafurahi sababu si aina ya uchezaji waliouzoea katika timu yao.
Na hata Jose Mourinho mbali na kushinda mataji akiwa Real Madrid bado mashabiki walikuwa hawafurahishwi na namna timu yao ilivyokuwa ikicheza kitu kilichopelekea makocha hao niliowatumia kama mfano kupoteza vibarua vyao kwa sababu hizo.
Shabiki ni mteja. Timu na wote wanaoizunguka wanamhudumia. Hivyo wanapaswa kuhakikisha anafurahia huduma ndio maana mabadiliko ya wachezaji au makocha wakati mwingine shinikizo huwa linatoka kwa wenye timu yao.
Kwa kuzingatia hilo kuna wakati unaweza kuona kama mashabiki wanapatia kutaka makocha waondolewe kwa kukosa lile soka walilolizoea bila kujali matokeo.
Hata hivyo, kuna wakati makocha wanakuwa wanaonewa kwa sababu, kwa vile kila kocha ana falsafa na mfumo wake wa kufundisha kutengeneza timu, ndio maana huwezi kukuta Mourinho na Pep Guardiola au Enzo Maresca akafanana na Arne Slot.
Huwezi kusema Nasreddine Nabi, Miguel Gamondi, Sead Ramovic na Miloudi Hamdi wanafanana kimbinu, hata kama wote wameipa Yanga mafanikio misimu minne iliyopita ndio maana kuna wakati ukipima kelele za mashabiki unaweza kuona ni kama vile makocha wanaonewa. Hata kama shabiki ni mteja na anataka burudani uwanjani, ifikie wakati watu waheshimu taaluma za watu na wenye taaluma kufanya yale yanayoleta furaha kwa mashabiki ambao ni kutaka kuona ushindi na burudani.