Hawa hapa kiboko wa Simba, Yanga

New Content Item (1)
New Content Item (1)

TAMBA pande zako, pande zetu hautambi... Hiyo ni mistari utakayoisikia mwanzo kabisa wakati ukisikiliza wimbo wa rapa Young Lunya unaoitwa ‘Freestyle Seassins 5’.

Ndio kilichotokea kwa klabu kubwa nchini kwa baadhi ya timu za Ligi Kuu Bara. Simba na Yanga zimekutana na wababe wao kwenye michezo yao ya msimu huu na mzunguko wa kwanza Wanajangwani walipata tabu kwa Ihefu FC kwa kuchapwa mabao 2-1 kabla ya mzunguko wa pili Simba nao kukutana na kichapo kutoka kwa Tanzania Prisons cha mabao 2-1. Vipigo sawa.

Huwa inashtua kidogo. Miamba hii hata mashabiki zao hawajazoea vichapo vya kushtukiza hivi. Zimekuwa zikitamba kushinda kila mechi lakini kuna miamba imekataa tambo hizo na kuzipiga bao pale walipokutana.

Ukiachana na vichapo vya msimu huu, Mwanaspoti linakuletea kumbukumbu za mechi ambazo Simba na Yanga zilitamba lakini mwishowe zikachezea vichapo kwenye mechi za ligi kutoka katika timu tofauti tangu mwaka 2019.


YANGA

Katika miaka mitano sasa, Yanga imepoteza mechi za ligi 13, ukitoa zile ilipokutana na Watani wake wa jadi Simba.


Katika mechi hizo, Azam ndiyo imeongoza kwa kutia doa tambo za Yanga ikiipa vipigo vitatu katika miaka mitano sasa, ikifuatiwa na Ihefu iiliyoshinda mara mbili huku Coastal Union, KMC, Kagera Sugar, Ruvu Shooting, Biashara United, Mtibwa Sugar, Lipuli na Stand United zikishinda mara moja dhidi yao.


STAND UNITED

Januari 19, 2019 Stand United ilizima shangwe la Yanga baada ya kuichapa bao 1-0 lililofungwa na Jacob Masawe dakika ya 88. Hiyo ilikuwa mechi ya kwanza kwa Yanga kupoteza kwa mwaka huo huku mashabiki wake wakibaki midomo wazi.


LIPULI

Machi 16, 2019 Lipuli ikiwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Samora Iringa, ilizima shangwe la Yanga iliyokuwa kileleni mwa msimamo na alama 67, baada ya kuichapa bao 1-0, lililowekwa nyavuni Haruna Shamte kwa frikiki iliyozama moja kwa moja nyavuni dakika ya 19 ya mchezo na kumwacha kipa Klaus Kindoki akishangaa.


MTIBWA SUGAR

Wakali hawa ambao kwa sasa maji yako shingoni wakihaha kutoshuka daraja, waliwahi kuizuia Yanga kutamba kwenye ligi.

Ilikuwa April 17, 2019 Mtibwa ilipoifunga Yanga bao 1-0, lililofungwa na  Riphat Hamis dakika ya 52 kwa kiki kali lililomshinda kipa Kindoki. Wakati huo Yanga ilikuwa kileleni mwa msimamo na alama 74.


BIASHARA UNITED

Wanajeshi hawa wa mpakani kipindi wapo Ligi Kuu waliichapa Yanga bao 1-0, mechi iliyopigwa Mei 10, 2019 Uwanja wa Karume, Musoma.

Bao la Biashara lilifungwa na Taqiq Seif Kiakala dakika ya nane, alipomchambua kipa Kindoki. Wakati huo Yanga ilikuwa nafasi ya pili kwenye msimamo na alama 80.


AZAM

Mei 5, 2019 Yanga ikiwa Uwanja wa Mkapa ilichapwa 2-0 na Azam, kwa mabao ya Daniel Amoah dakika ya 45 na Mudathir Yahya dakika ya 50 wakati huo Yanga ilikuwa nafasi ya pili kwenye msimamo huku Azam ikiwa nafasi ya tatu.

Januari 18, 2020 Azam ilichafua tena ubao wa Yanga baada ya kuichapa 1-0 kwa bao la kujifunga kwa aliyekuwa beki wa Yanga, Ally Mtoni ‘Sonso’ (sasa marehemu), dakika ya 26 ya mchezo. Katika mechi hiyo Sonso alipata kadi nyekundu dakika ya 79 baada ua kumkanyaga beki wa Azam, Nico Wadada.

Aprili 25, 2021 Azam ilitamba tena mbele ya Yanga kwa kuichapa bao 1-0 lililofungwa na Prince Dube aliyepiga kiki kali lililomshinda kipa Faroukh Shikhalo dakika ya 86 ya mchezo.


RUVU SHOOTING

Wakati ‘Wazee wa Mpapaso’ wakiwa Ligi Kuu waliwahi kuzima tambo za Yanga kwa kuichapa bao 1-0, Agosti 28, 2019 kwa bao la Sadat Mohamed.


KAGERA SUGAR

Januari 15, 2020 Yanga ikiwa chini ya kocha Luc Eymael ilipokea kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Kagera Sugar Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam. Mabao ya Kagera yalifungwa na Yusuph Mhilu, Ally Ramadhan na Peter Mwalyanzi.


KMC

Watoza ushuru hawa wa Kinondoni nao waliikanda Yanga kwenye ligi, Machi 12,2020 kwa bao 1-0 lililofungwa na Salim Aiyee dakika ya 62.


COASTAL UNION

Wagosi wa kaya, Machi 4, 2021 walizima shangwe la Yanga katika uwanja wa mkwakwani baada ya kuichapa mabao 2-1.

Mabao ya Coastal yalifungwa na Eric Msagati na Mudathir Said huku lile la Yanga likifungwa na Tuisila Kisinda.


IHEFU

Kwa msimu wa pili mfululizo sasa Ihefu inaitandika Yanga kila inapokanyaga Uwanja wa Highland Estate.

Msimu uliopita Ihefu ilishinda 2-1, mchezo ambao Yanga ilianza kupata bao dakika ya tisa kutoka kwa Yanick Bangala kabla ya Never Tigere kuisawazishia Ihefu dakika ya 38 kwa Frikiki ya moja kwa moja na Lenny Kisu akafunga bao la ushindi kwa kichwa dakika ya 61.

Msimu huu pia matokeo hayo yamejirudia, Oktoba 4, mwaka jana na Yanga ilitangulia kupata bao dakika ya tatu kupitia kwa Pacome Zouzoua lakini dakika ya 40 Lenny Kisu aliisawazishia Ihefu na Charles Ilamfya kufunga bao la ushindi dakika ya 67.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

SIMBA

Wenye nchi katika  miaka mitano sasa wamepoteza mechi za ligi 11,  ukitoa zile walipokutana na Yanga.

Katika mechi hizo, Tanzania Prisons na Kagera Sugar ndio wamekuwa wababe wa Mnyama, kila timu ikimtwanga mara tatu huku Azam, Mbeya City, Ruvu Shooting, Mbao, JKT Tanzania na Mwadui, kila moja ikishinda mechi moja.


KAGERA SUGAR

Aprili 20, 2019, iliichapa Simba mabao 2-1 yaliyofungwa na Abdalkasim Hamis dakika ya 20 na Ramadhan Kapera dakikia ya 41 huku lile la kufuta machozi kwa Simba likifungwa na Emmanuel Okwi dakika ya 64.

Wakati mchezo huo unapigwa Uwanja wa Kaitaba, Simba ilikuwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi na alama 60. Kagera iliikanda tena Simba Mei 10, 2019, bao 1-0 katika Uwanja wa Uhuru kwa bao la kujifunga la Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ dakika ya 42.

Wakati huo Simba ilikuwa ikiongoza ligi na alama 81.

Januari 26, 2022 Kagera Sugar iliharibu tena shangwe la Simba baada ya kuichapa bao 1-0, lililofungwa na Hamis Kiiza dakika ya 71.


MWADUI

Wakati wakali hawa wa Shinyanga wakiwa Ligi Kuu waliwahi kuichapa Simba bao 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga kwa bao la kichwa lililofungwa na Gerald Mdamu. Mechi hiyo ilipigwa Oktoba 30, 2019.


JKT TANZANIA

Februari 7, 2020 Simba ikiwa Uwanja wa Uhuru ilipokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa JKT Tanzania kwa bao pekee lililofungwa na Adam Adam dakika ya 25.


MBAO

Wakali hawa wa mwanza Julai 16, 2020 kipindi wapo Ligi Kuu waliichapa Simba mabao 3-2 kwenye mchezo uliopigwa Uwanja wa Mkapa.

Mabao ya Mbao yalifungwa na Rajabu Rashid, Jordan John na Wazir Junior huku yale ya Simba yakifungwa na Meddie Kagere na Miraji Athuman ‘Sheva’. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Simba kuruhusu mabao zaidi ya mawili kwa msimu huo.


TANZANIA PRISONS

0ktoba 22, 2020, Prisons 1-0, ilichapa Simba, bao 1-0 kwenye uwanja wa Nelson Mandela Sumbawanga kwa bao la Samson Mbangula alilofunga kwa kichwa dakika ya 49.

Juni 26, 2022, Prisons iliifunga tena Simba kwa bao la Benjamin Asukile lililofungwa dakika ya 53 ya mchezo na kudumu. Mechi hiyo ilichezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Simba ilikufa tena kwa Prisons msimu huu katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro baada ya kuchapwa mabao 2-0. Mabao yote ya Prisons yalifungwa na Mbangula huku lile la Simba likifungwa na Fabrice Ngoma.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

RUVU SHOOTING

Wakati Ruvu ikiwa Ligi Kuu, ilichafua ubao wa Simba Oktoba 26, 2020 kwa kuichapa 1-0. Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Uhuru bao la Ruvu lilifungwa na Fully Maganga.


MBEYA CITY

Wakali hawa wa Mbeya nao wamewahi kuipasua Simba kwenye ligi. Ilikuwa Januari 17, 2022, Uwanja wa Sokoine na Simba ilichapwa bao 1-0, bao lililofungwa na Paul Nonga.

Katika mechi hiyo, beki wa Mbeya City, Mpoki Mwakinyuke alionyeshwa kadi nyekundu na Chris Mugalu wa Simba akakosa mkwaju wa penalti.


AZAM

Matajiri hawa wa Chamazi, Oktoba 27, 2022 waliikanda Simba 1-0 kwa bao la Prince Dube lililofungwa dakika ya 35 ya mchezo.