Hadithi ya wizi wa tiketi mwisho wake ni lini?

Muktasari:
Hali hiyo ilikuja mara baada ya kutangazwa rasmi kuanza kutumika kwa mfumo wa tiketi hizo na hivyo imani iliyojengeka ni kwamba wale wote waliokuwa wakiendesha maisha yao kwa kuhujumu mapato ya mechi mwisho wao ulikuwa umefikia.
IMANI kwamba mfumo wa tiketi za elektroniki ni kikwazo kwa wezi wa mapato ya mechi za soka hasa zile za mahasimu Yanga na Simba ilizungumzwa na wadau wengi wa soka.
Hali hiyo ilikuja mara baada ya kutangazwa rasmi kuanza kutumika kwa mfumo wa tiketi hizo na hivyo imani iliyojengeka ni kwamba wale wote waliokuwa wakiendesha maisha yao kwa kuhujumu mapato ya mechi mwisho wao ulikuwa umefikia.
Kilichoaminika mbele ya wengi ni kwamba zile habari za watu kukamatwa na tiketi feki au fedha kubebwa kwenye viroba ilikuwa imefika mwisho.
Kinyume na matarajio hayo, mfumo wa tiketi za elektroniki haukuweza kudumu, kama ilivyo ada mwanzo wa jambo lolote huandamana na changamoto za hapa na pale.
Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa tiketi za elektroniki ambazo pamoja na nia njema iliyokusudiwa wakati mfumo huu ukianzishwa changamoto zimekuwa nyingi kiasi cha kuamua kuusimamisha kwa nia njema.
Tumewahi kuuzungumzia uamuzi huu na kusisitiza kwamba changamoto zilizopo zifanyiwe kazi ili mfumo huu ambao bado tunaamini ni mwiba kwa wezi wa mapato na ndio mfumo wa kisasa urudi kwa mara nyingine changamoto hizo zikiwa zimefanyiwa kazi kikamilifu.
Kama tulivyowahi kusema awali kwamba kusimamishwa kwa mfumo huu sababu yake ni changamoto za kiutendaji na tukaonya kwamba isiwe fursa ya wezi wa mapato kuanza kazi yao ya kuhujumu mapato ya mechi za soka.
Kauli yote hiyo ni kama ilipuuzwa kwani katika mechi ya mahasimu Yanga na Simba iliyochezwa Machi 8 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam haukutumika mfumo wa tiketi za elektroniki.
Kilichotokea ni hadithi ya watu kukamatwa na tiketi feki za mechi hiyo wakiwa tayari wameshauza tiketi nyingi na kujipatia fedha kwa njia isiyo halali.
Hadithi hii ya kukamatwa kwa wezi wa tiketi si mara ya kwanza kuisikia, ni hadithi ambayo imekuwa ikisikika mara kwa mara kabla mfumo wa tiketi za elektroniki haujaanza.
Hata hivyo kinachosikitisha na kutatiza ni ile hali ya tatizo kujirudia mara kwa mara na watu kuendelea kukamatwa lakini baada ya kukamatwa kumekuwa na ukimya unaojitokeza.
Hatuoni wahusika kuchukuliwa hatua ambazo zitatoa funzo kwa wengine kutokuwa tayari kufanya biashara hiyo ya uuzaji wa tiketi haramu zinazohujumu mapato ya klabu, TFF pamoja na serikali.
Kwa upande wetu tunaamini wahusika wa hujuma za mapato ya mechi wana mtandao mpana, si hawa ambao tumesikia wanakamatwa bali kuna watu nyuma yao, watu ambao tunaamini wanatoka TFF na wengine katika klabu.
Wanaokamatwa ni dagaa, mapapa wenyewe wapo TFF na wengine katika klabu, ni wazi kwamba ukweli huu ndio unaofanya vita ya wezi wa tiketi na wenye kuhujumu mapato ya mechi iwe kubwa na ngumu.
Ni vyema juhudi za makusudi zikafanyika ili kuuvunja huu mtandao ambao huenda ndio uliofanya kazi kubwa ya kuhujumu matumizi ya tiketi za elektroniki jambo ambalo wamelifanikisha.
Bila ya kufanya hivyo ni wazi kwamba hadithi hii inayochosha ya mapato ya mechi za soka kuhujumiwa itaendelea kusikika kila kukicha kwa watu kukamatwa mara kwa mara.