Gofu sheria zake zitakufurahisha

GOFU ni mchezo uliyojaa kila aina ya vitu vinavyoweza kukushangaza na kukupa hamasa ya kuupenda ili kuendelea kuongeza siku za kuishi.

Kama kawaida Mzuka wa Gofu, unafanywa na Gazeti la Mwanaspoti, linakuchambulia sheria mama za mchezo huo, zipo ambazo zitakushangaza na kukupa tabasamu la moyo, kwani zinatofautiana sana na michezo mingine.

Katika mahojiano maalumu na mchezaji wa kulipwa Aidan John Nziku ambaye pia ni msimamizi msaidizi wa viwanja vya gofu Dar Gymkhana anazifafanua baadhi ya sheria za mchezo huo.

Anasema “Sheria mama duniani kote kabla ya mchezo lazima uwe na begi ambalo limebeba fimbo zisizozidi 14, kukagua aina ya mipira kabla ya mchezo, kufika uwanjani kabla  dakika 10 ukichelewa unatolewa kwenye mashindano.”

Sheria nyingine inayozingatiwa ni mavazi kwa wachezaji wa kulipwa hawaruhisiwi kuvaa kaptura, bali suruali ndefu ya kitambaa na tisheti ya kola.

“Tofauti kidogo na wachezaji wa ridhaa ambao wanaweza wakavaa kaptula ila iwe ya kitambaa kuhusu tisheti na viatu wanapaswa kuvaa kama maproo,”anasema na kuongeza;

“Wanawake wanatakiwa kuvaa sketi iwe juu zaidi ya magoti na iwe ya kitambaa, wanaweza wakavaa blauzi ya kola ama tisheti iwe ya kola, huku hakuna kuvaa nguo za jinzi kabisa.”


SHERIA ZA ADHABU

Mchezo huo hauhitaji udanganyifu, inapotokea ukagundulika tu, unaondolewa kwenye mashindano husika,mbaya zaidi kwa Caddy Master (mbeba vifaa), akimsaidia mchezaji kudanganya basi unakuwa ndio mwisho wa kufanya kazi hiyo.

“Kwa wabeba vifaa adhabu yao ni kali zaidi, anafukuzwa kabisa kazi na inaandikwa barua kwa klabu zote za gofu nchini kuzijuza kuwa huyu ni mdanganyifu, hivyo atakuwa amejiondoa kwenye mchezo huo moja kwa moja,”anasema.

Nziku anaelezea sheria nyingine mchezaji akiwa mkorofi akatoa lugha za matusi, ama kupiga fimbo chini pia anaondolewa kwenye mashindano na adhabu atapewa na nahodha wake.

“Nahodha ana nguvu ya kumfungia mchezaji aliyekosa nidhamu, vile anavyoona anastahili kunyooshwa inaweza ikawa mwezi mmoja, miwili ama mitatu na akimuonea huruma basi wachezaji wote wa kulipwa wataamua adhabu yake, kwani tuna uongozi wa wachezaji wa kulipwa,”anasema.


SHERIA ZA MASHABIKI

Ukiambiwa mchezo huo ni wa kistarabu basi unapaswa kuuelewa sheria zake kisawasawa, huko hakuna mashabiki wa fujo kama ilivyo kwa soka, wote wanapaswa kuzingatia masharti.

Ipo hivi: “Wanatakiwa kushangilia baada ya mchezaji kupiga mpira hapo wanaweza wakapiga makofi, miruzi, sasa basi mambo ya vigoma, filimbi huko havitakiwi.

 “Mchezo huo unatumia sana akili, ndio maana mtu akipiga mpira kila mtu anatakiwa akae kimya, mashabiki wasioelewa wataeleweshwa kwa mara ya kwanza, wakirudia mara ya pili kupiga kelele wakati mchezaji anapiga mpira anatolewa nje,” anasema.

Anasema sheria nyingine kwenye mashindano lazima kila kundi lianzie wachezaji wawili hadi wanne, wasizidi idadi hiyo.

 “Kwanza mchezo huo mwamuzi ni wachezaji wenyewe na wanapaswa kusimamia sheria ipasavyo. Kama ni wachezaji wa ridhaa wameshindwa kumudu mchezo anatumwa mchezaji wa kulipwa kuwasimamia, kwani anakuwa anajua zaidi sheria na ndio wenye kauli ya mwisho.”

Ukiachana na hilo, anaeleza sheria ya kwanza anayotakiwa kuijua mtu anayejifunza gofu anaanza kufundishwa maana ya fimbo na namna zinavyotumika kila moja.

“Kila fimbo ina maana yake na umbali wake, ukikosea unaweza ukaharibu pichi ukipiga fimbo ambayo haitakiwi kwenye kiwanja husika,”anasema.


MCHEZO WENYEWE

Anaeleza jinsi zinavyopatikana Handcup (kiwango cha mchezaji), zipo madaraja matatu, akitaja la kwanza Division C inaanzia 19-24 hiyo ni kwa wachezaji ambao wanaanza kujifunza gofu, B ni 18-10 wachezaji hao wanakuwa wameujua mchezo na sheria zao ila kiwango chao kinakuwa bado kipo chini.

Wakati A 9-0 wachezaji wa daraja hilo wanakuwa wanaaminiwa na klabu husika na wanaweza wakawatuma popote, ila wanakuwa wanaangaliwa na jicho la taifa na pia akifanya vizuri anaweza akacheza timu ya taifa.

“Lakini kwa mchezaji wa kulipwa hapimwi kwa hayo madaraja hana A, B na C kwani tayari anakuwa amevuka viwango vyote hivyo,” anasema.


POINTI

Anasema kuna kadi ambazo zina vyumba vya kujaza kila kiwanja alichocheza mchezaji, hivyo mwisho wa mchezo zinahesabiwa na kupatikana kwa mshindi wa kwanza pengine hadi wa 10 inategemeana na idadi ya watu walioshiriki mashindano, wanaweza wakawa 150 ama zaidi.


MUDA WA MCHEZO JE!

Anasema hakuna muda kamili wa mchezo inategemeana na ushapu wa wachezaji wenyewe wapo ambao wanaweza wakatumia masaa mawili hadi manne.

“Hapo kwenye muda ni wachezaji wa kundi husika wanacheza kwa haraka kiasi gani, kama watu wanaoelewa zaidi mchezo wanatumia dakika chache zaidi,”anasema.

Mbali na hilo, viwanja vya gofu vya Dar Gymkhana kwamba cha Par3 ambacho kinatakiwa kupiga mipigo mitatu mpira kwenda shimoni kina urefu wa mita 157, par 4 kina urefu wa mita 315 na par5 kina mita 450.

“Viwanja vimetofautiana kwa Viwanja vya Dar Gymkhana ni hizo mita nilizokutajia ila vingine viko tofauti,”anasema.

Pia, ameelezea kuhusiana na makocha wa gofu “Kuna mawili, kocha anaweza akasomea bila kucheza gofu kabisa, lakini pia wapo wale ambao ni wachezaji wa kulipwa wanafundisha ndio maana hata mimi nakochi watu,” anasema na kuongeza;

“Kwa hapa Tanzania kuna nguli mwenye heshima kubwa ya mchezo huo na hana haja ya kusoma kabisa ni Salum Mwanyenza kiwango chake cha kucheza mataifa mengi duniani anastahili moja kwa moja kufundisha.

“Watu wengi wasichojua Mwanyenza amecheza na baba wa staa duniani Eldrick Tont ‘Tiger Woods’  unaweza ukaelewa ni kiasi gani tuna staa mkubwa sana, huyo hana haja ya kusomea kabisa mchezo huo.


Imeandaliwa na Olipa Assa, Nevumba Abubakar, Oliver Albert, Brown Msyani na Imani Makongoro