Prime
GOAL MACHINES: Kwa mastraika hawa, Sowah wenzake kazi wanayo!
Muktasari:
- Achana na makipa, mabeki au viungo waliosajiliwa kutoka nje ya nchi, hapa nazungumzia washambuliaji kadhaa wenye majina waliotua katika klabu hizo wakibeba matumaini ya mashabiki.
MSIMU mpya wa mashindano wa 2025-26 umeanza kunoga, huku mashabiki wakiwa na hamu ya kutaka kuona nyota wapya waliosajiliwa na klabu za Ligi Kuu Bara watafanya maajabu gani.
Achana na makipa, mabeki au viungo waliosajiliwa kutoka nje ya nchi, hapa nazungumzia washambuliaji kadhaa wenye majina waliotua katika klabu hizo wakibeba matumaini ya mashabiki.
Kuna Japhte Kitambala wa Azam FC, Andy Boyeli na Celestin Ecua kwa Yanga, Jonathan Sowah wa Simba na Horso Mwaku Malanga wa Singida BS wote wanasubiriwa kuona watafanya nini.
Hadi sasa katika mechi za kimataifa na zile za katika Ligi Kuu Bara, bado hawajafanya maajabu yoyote, japo wana muda wa kuweka mambo sawa, kadri michuano inavyozidi kusonga mbele.
Hata hivyo, wakati tunawasubiri kina Mwaku, Boyeli na Kitambala kufanya maajabu katika Ligi Kuu Bara, hapa chini kuna washambuliaji wa kigeni waliowahi kukinukisha na kuacha alama kubwa nchini kupitia Ligi Kuu Bara.
Bila kujali walitumika kwa muda gani na klabu hizo za Tanzania, lakini kile walichokifanya kinaweza kuwa ni mtego wa aina yake kwa kina Sowah na wenzake.
Ebu soma dondoo za washambuliaji hao, kisha utaamua mwenyewe nani anastahili kuwa mshambuliaji wa muda wote wa kigeni aliyewahi kukiwasha Bara, bila kujali alichofanya kupitia michuano ya kimataifa na kitaifa.
KIPRE TCHETCHE
Mshambuliaji huyo raia wa Ivory Coast, aliitumikia Azam FC kwa miaka mitano kuanzia 2011 alipotua na pacha wake kiungo mkabaji, Kipre Balou wakitokea JC Abidjan ya kwao hadi 2015, na alikuwa moto kweli kweli.
Nyota huyo aliiwezesha Azam kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2013-2014, likiwa ndio taji lao pekee la ligi tangu klabu hiyo imeanzishwa hadi sasa pamoja na kuipa Kombe la Mapinduzi 2012, 2013 na Kombe la Kagame 2015.
Akiwa na Azam, Kipre aliibuka Mfungaji Bora wa msimu wa 2012-2013 akifunga mabao 17, kisha kuwa Mchezaji Bora wa msimu wa 2013-2014.
Rekodi zinaonyesha kuwa hadi anaondoka nchini mwaka 2015, alikuwa ndiye mchezaji wa kigeni aliyefunga idadi kubwa zaidi ya mabao akiwa na 57 katika Ligi Kuu. Kipre alikuwa ni mchezaji anayekupa kila kitu, kwani alikuwa na uwezo wa kufunga na kuasisti mabao mbali na kuamua mechi kubwa.
Kipre alimudu kucheza kama mshambuliaji wa kati, akitumika pia kama winga ya kushoto na kulia kwa ubora ule ule.
Pia alikuwa ni kati ya wachezaji waliojaaliwa nguvu, kasi, maarifa na mbinu za kuwatoka mabeki, lakini kubwa ni kupiga mashuti kwa kutumia miguu yote kwa ubora ule ule wa kunyanyasa makipa huku akiwapa furaha mashabiki wa timu yake.
MEDDIE KAGERE
Ndiye mshambuliaji wa kigeni anayeshikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 77.
Straika huyo raia wa Rwanda mwenye asili ya Uganda, pia ndiye anayeshikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa misimu miwili mfululizo akifanya hivyo 2018-2019 na 2019-2020.
Alianza kwa kufunga mabao 23 ikiwa pia ni rekodi kwa nyota wa kigeni na alipigiwa debe abebe tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu, lakini hafla ya tuzo za TFF hazikufanyika na alitetea tuzo hiyo ya mfungaji bora kwa msimu uliofuata kwa kufunga mabao 22. Misimu minne akiwa Simba alifunga mabao 65 huku mengine 12 aliyafunga katika misimu mitatu kupitia Singida Fountain Gate na Namungo aliyoachana mwishoni mwa msimu uliopita.
Kagere alisifika kwa kuwa na akili ya kuwatoka mabeki na kufunga kwa kutumia miguu yote na kichwa.
Hakuwa na chenga kama Kipre Tchetche au Emmanuel Okwi, lakini alikuwa mjanja kujipanga katika eneo sahihi la kuwatungua makipa. Kwa misimu saba aliyokipiga nchini akianzia na Simba, Singida Big Stars iliyofahamika baadaye kama Singida Fountain Gate (sasa Fountain Gate) na Namungo, 'Bull Striker' MK14 aliacha alama ikiwamo kuibeba Simba katika michuano ya CAF kwa kucheza mara kadhaa hatua ya robo fainali.
FISTON MAYELE
Straika wa kiwango cha hali ya juu aliyeitumikia Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili tu akiwa na Yanga na kufanya mambo makubwa anayoyaendeleza kwa sasa kule Pyramids ya Misri.
Rekodi zinaonyesha Mayele alitumika katika mechi 56 za Ligi Kuu na kuhusika katika mabao 41 akifunga mabao 33 na asisti manane.
Msimu wa kwanza alifunga mabao 16 na kumaliza katika nafasi ya pili ya wafungaji nyuma ya George Mpole aliyekuwa Geita Gold aliyetupia 17 na msimu uliofuata alibeba tuzo ya Mfungaji Bora sambamba na Saido Ntibazonkiza aliyeanza na Geita na kumalizia Simba msimu huo wa 2022-2023 kila mmoja akifunga mabao 17, lakini akiiwezesha Yanga kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kufunga jumla ya mabao 14, yakiwamo saba yaliyompa tuzo ya mfungaji bora wa CAF.
Pia alibeba mataji mawili ya Ligi Kuu, mawili mengine ya Kombe la Shirikisho (FA) na Ngao ya Jamii akiitungua Simba misimu mwili mfululizo.
Mayele raia wa DR Congo amejaaliwa uwezo wa kusepa na kijiji kutokana na kipaji cha kukaa na mpira, kasi, nguvu na akili ya kutoka mabeki.
Mabao 33 ya Ligi aliyatupia kwa kutumia miguu yote miwili pamoja na kichwa na alikuwa akiwatesa mabeki kwa nguvu na ujanja aliokuwa nao, japo ni kati ya washambuliaji waliokuwa wanapoteza nafasi nyingi za kufunga, lakini amewaliza sana makipa kwa umahiri wake akijitoa kwa kila hali uwanjani kuibeba timu.
AMISSI TAMBWE
Huyu ndiye aliyekuwa anashikilia rekodi ya nyota wa kigeni aliyefunga mabao mengi katika msimu mmoja wa Ligi Kuu, lakini aliyekuwa kinara wa mabao kwa wageni baada ya kumpiku Kipre na kuja kupitwa na Kagere.
Hadi alipostaafu Tambwe alikuwa amefunga jumla ya mabao 75 katika misimu saba kupitia klabu za Simba, Yanga na Singida Fountain Gate. Straika huyo raia wa Burundi, pia ni nyota pekee wa kigeni aliyewahi kutwaa tuzo ya mfungaji bora akiwa na klabu mbili tofauti za Simba na Yanga, na pia kinara wa hat trick akizifunga sita.
Tambwe alisajiliwa na Simba 2013 akitokea Vital'O ya Burundi na kuitumikia kwa msimu mmoja na nusu akitwaa tuzo ya mfungaji bora 2013-2014 kabla ya kuibukia Yanga baada ya kutemwa kitatanishi kutoka Msimbazi katika dirisha dogo la 2014-2015 na kuwa mfungaji bora wa Ligi 2015-2016 kisha kugeuka shujaa wa Jangwani hadi anaondoka kwenda Oman na baadae Djibouti kabla ya kurejea kujiunga na Singida Big Stars (Singida Fountain Gate, sasa Fountain Gate).
Tambwe alisifika kwa umaliziaji mzuri na tabia yake ya kujipanga katika maeneo muhimu zaidi kuliko kutengeneza mashambulizi, kwani hakuwa mkali wa kupiga chenga.
Mabao yake mengi aliyafunga kwa kutumia kichwa na mguu wa kulia pia ulikuwa mahiri kutupia, japo alifunga vilevile kwa mguu wa kushoto. Kwa sasa ni meneja wa Singida Black Stars (zamani Ihefu).
EMMANUEL OKWI
Nyota huyo raia wa Uganda ni miongoni mwa nyota wa kigeni waliopapatikiwa kwa kipaji kikubwa cha soka alichokuwa nacho uwanjani.
Okwi amecheza kwa mafanikio makubwa katika klabu ya Simba, japo aliitumikia Yanga kwa muda mchache msimu wa 2013-2014 kabla ya kuweka mgomo kudai fedha zake za usajili na kujikuta wakiachana juu kwa juu kabla ya kurejea Msimbazi akitokea Denmark.
Okwi ndiye mchezaji aliyeingia na kutoka katika Ligi Kuu Bara kuliko yeyote akiitumikia zaidi Simba iliyowahi kumfanya awe Mfungaji Bora msimu wa 2017-2018 akifunga 20, lakini rekodi za ujumla zinaonyesha Okwi ameitumikia Simba katika mechi zaidi ya 100 na kuifungia karibu mabao 80 yakijumuisha ya Ligi Kuu, Kombe la FA na ile ya kimataifa.
Kipaji cha kusakata soka akipiga chenga, kukimbia kwa kasi na kutoogopa mabeki, ilimfanya nyota huyo aliyekuja kwa mara ya kwanza nchini akiwa na umri wa miaka 17 mwaka 2010, kuwa nyota kuwa hatari.
Alifunga mabao kutumia miguu yote miwili pamoja na kichwa na kutengeneza nafasi kwa wenzake na alikuwa fundi wa mipira iliyokufa kama ya penalti na frii-kiki na alijaaliwa mashuti makali. Anakumbukwa zaidi na Yanga alipowanyamazissha katika dabi ya 2015 kwa bao pekee la mbali na kuwa mmoja ya nyota walioiua kwa mabao 5-0 Mei 6, 2012.
WENGINE
Orodha hii haina maana hakuna washambuliaji wengine wakali waliowahi kutamba nchini. Hapana. Kuna Didier Kavumbagu, Prince Dube, Laudit Mavugo, Obrey Chirwa, Donald Ngoma, waliowahi kutamba katika timu za Simba, Yanga na Azam, lakini hao waliopo hapo juu walikuwa na balaa zaidi na baadhi wameondoka wakiendelea kukumbukwa na sasa kina Boyeli na wenzao wajipange vilivyo. Kazi kwao!