Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Furahisha: Maisha yangu ni ngumi, bado sijafika ninapopataka

FURAHISHA Pict

Muktasari:

  • Huyo ni Hamadi Furahisha, mmoja wa mabondia wa Tanzania ambaye safari yake imepitia kwenye maumivu, jasho na damu.
  • Lakini nyuma ya ushindi wake ulingoni kuna simulizi ya mtoto wa Yombo Dovya aliyekuwa na ndoto ya kupanda ulingoni tangu akiwa darasa la saba, akiwa hajui kama siku moja angekuwa bondia wa kulipwa.

NDANI ya ulingo anajulikana kwa utulivu wake, lakini anapopanda ulingoni hubadilika na kuwa bondia anayependa kushambulia, asiyeogopa majina makubwa na mwenye kiu ya mafanikio.

Huyo ni Hamadi Furahisha, mmoja wa mabondia wa Tanzania ambaye safari yake imepitia kwenye maumivu, jasho na damu.

Lakini nyuma ya ushindi wake ulingoni kuna simulizi ya mtoto wa Yombo Dovya aliyekuwa na ndoto ya kupanda ulingoni tangu akiwa darasa la saba, akiwa hajui kama siku moja angekuwa bondia wa kulipwa.

Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Furahisha anasimulia maisha yake kuanzia alipoanza hadi ndoto alizonazo sasa za kutwaa mikanda mikubwa ya kimataifa.


SAFARI YAKE

Anasema safari yake ya Ndondi ilianza mwaka 2009 wakati huo akiwa mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Yombo Dovya, alianza kuvutiwa na mchezo wa ngumi baada ya kuona watu waliokuwa wakifanya mazoezi katika eneo hilo.

"Mwaka 2009 nilikuwa darasa la saba. Nilianza kufanya mazoezi Yombo Dovya. Nilikuwa napenda michezo tangu utotoni, lakini ngumi ndiyo zilinivutia zaidi," anasema Furahisha

"Bondia niliyekuwa nampenda wakati huo alikuwa Alhaji Mohamed Cholile ambaye alikuwa anapenda ngumi, baadaye nikashangaa ameacha akageukia kwenye soka na nako akaacha nilikuwa namkubali sana."

Safari yake ilianza chini ya kocha  Haji Pela, ambaye anamtaja kuwa mtu aliyemfundisha siyo tu namna ya kupigana, bali pia nidhamu ya maisha ya bondia.


"Kocha alikuwa mkali sana alitufundisha kwamba kabla hujawa bondia mzuri lazima uwe na nidhamu. Hicho ndicho kilichonisaidia mpaka leo."

Hata hivyo, mwanzo wake haukuwa mzuri Pambano lake la kwanza lilimkutanisha na bondia aliyekuwa akiheshimika wakati huo, Abdallah Kassimu.

"Nilikuwa mdogo sana. Abdallah alikuwa tayari anajulikana na maarufu. Kocha aliniambia nisiogope jina lake, nicheze kwa uwezo wangu."

Anasema raundi ya kwanza ilikuwa ngumu kuliko alivyotarajia.

"Alinisumbua sana. Raundi ya pili nilijaribu kurudi kwenye mchezo lakini sikuweza. nikapoteza pambano."

"Sikuumia kwa kupoteza, niliumia kwa kuona bado nilikuwa sijafikia kiwango nilichotaka. Kuanzia siku hiyo nilianza kufanya mazoezi kwa bidii sana."

Mwaka 2014 akakutana na mpinzani huyo kwenye mashindano ya Bingwa wa Mabingwa yaliyokuwa yakitafuta bondia mmoja wa kujiunga na timu ya taifa.

"Kabla sijafika kwake nilicheza na mabondia wawili nikawashinda. Nilipoambiwa nitakutana  na Abdallah nilijisemea huu ndiyo wakati wa kulipa deni."

Anasema safari hiyo ilikuwa tofauti.

"Nilianza kwa kasi. Raundi ya kwanza nilimpiga sana mpaka akavuja damu nyingi. Nilishinda pambano na nikachaguliwa kuwa bondia bora wa mashindano," anasema

Anasema ushindi huo ulimfungulia milango ya kuitwa kwenye timu ya taifa, jambo ambalo lilikuwa ndoto yake tangu aanze kucheza ndondi.

Miongoni mwa safari ambazo hazitoki kichwani mwake ni ile ya China mwaka 2014/15 walikokwenda kuweka kambi kabla ya mashindano ya Scotland.

"China ilinifundisha mengi. Tulikuwa tunafanya mazoezi kwa nidhamu kubwa sana. Kila kitu kilikuwa kinapangwa kwa muda na hapo ndipo nilipojifunza somo la nidhamu."


REKODI ZAKE

Kwa mujibu wa rekodi za Boxrec zinaonyesha kuwa Furahisha amecheza mapambano 16, akishinda 12, sare mbili na kupoteza mapambano mawili.

Rekodi hiyo inaonyesha jinsi alivyoendelea kuweka heshima kwenye ndondi za kulipwa huku akiisaka nafasi ya kupigania mikanda mikubwa zaidi Afrika.

"Malengo yangu ni kuandika historia mpya ya kushindania mikanda mikubwa Afrika najua sio rahisi lakini kupitia uongozi wangu na juhudi zangu nitafikia malengo hayo ndani ya miaka michache ijayo," anasema Furahisha.


HILI HALISAHAU

Akiendelea kusimulia safari yake, Furahisha anasema pamoja na ushindi alioupata dhidi ya mabondia mbalimbali, kuna pambano moja ambalo bado linamuumiza moyo wake kila anapolikumbuka.

 Ni pambano la kuwania mkanda wa PST, ambalo anaamini alistahili kushinda lakini akanyimwa ushindi.

“Nilipigana raundi zote 10 na bondia mmoja hivi anaitwa Hamad simkumbuki jina la mwisho sababu ni muda kidogo.Nilifanya kila nilichoweza matokeo yalipotoka wakampa mwenzangu ushindi," anasema Furahisha na kuongeza

"Kulikuwa na fujo ukumbini, watu wengi walishangaa kuona kile kilichotokea binafsi  nililia sana kwa sababu niliamini nilikuwa nimefanya kazi yangu lakini nikadhulumiwa.”

Anasema siku hiyo ilikuwa miongoni mwa siku ngumu zaidi katika maisha yake ya ubondia.

“Bondia akipanda ulingoni anajitoa kwa asilimia mia moja. Unapopigana vizuri halafu usipewe haki yako inauma sana.”


AWAACHA MIDOMO WAZI

Mbali na pambano la PST, Furahisha anasema moja ya mapambano yaliyompa heshima kubwa ni lile dhidi ya Henock Phiri kutoka Malawi alilopigana mwaka huu.

“Watu wengi walikuwa wanaamini napigwa kwa sababu alikuwa amewapiga mabondia wengi wa Tanzania. Nilipoingia ulingoni nilijua lazima niwaonyeshe kwamba na mimi nina uwezo.”

Anasema pambano hilo lilimjenga kujiamini zaidi na kuwafanya wengi waanze kumchukulia kama bondia mwenye uwezo wa kupigania mikanda mikubwa.

“Baada ya pambano watu wakaanza kubadilisha mtazamo. Wale waliokuwa hawanipi nafasi wakaanza kunikubali, nakumbuka kocha wangu aliniambia napaswa nionyeshe uwezo wangu,"


NJE YA ULINGO

Wakati mabondia wengi huonekana wakifurahia umaarufu, Furahisha anasema maisha ya bondia Tanzania si mepesi kama watu wanavyofikiria.

“Sina kazi nyingine zaidi ya ngumi. Hizi ndizo zinazonifanya niishi. Dovya Boxing wananisimamia vizuri sana na mashabiki zangu wa Temeke nawakubali kwa sababu wananisapoti sana.”

Anasema wakati mwingine anaweza kukaa muda mrefu bila pambano lakini kutokana anaishi vizuri na watu inakuwa rahisi wao kumsaidia.

“Unaweza ukakosa kabisa pambano halafu baadaye ukapata pambano moja. Ndani ya mwaka mara nyingi napanda ulingoni mara tatu au mara nne, lakini mtaani kwangu wananisapoti sana kwa sababu naishi maisha halisi, shabiki anaweza kutoka alikotoka anakupa pesa."


MAPAMBANO YA NJE

Anasema kupitia ngumi ametembea nchi mbalimbali ikiwemo Scotland China Congo Brazzaville na nyinginezo ambazo kama isingekuwa ngumi basi asingefika.

Kati ya nchi hizo Ghana ndiyo iliyompa moja ya malipo makubwa zaidi katika maisha yake ya ubondia.

“Nilienda kuwania mkanda wa BWPF dhidi ya Dogo Beto. Alikuwa bondia mwenye nguvu sana na anajua kweli timing. Nakumbuka nilipata dola 5,000, hiyo ilikuwa fedha kubwa kwangu," anasema Furahisha.

Anasema fedha hizo zilimpa nguvu ya kuendelea kuamini kwamba ndondi zinaweza kubadilisha maisha ya bondia.


ANACHOFELI MWAKINYO

Furahisha anasema anamkubali sana Hassan Mwakinyo kwa mafanikio aliyoyapata ndani na nje ya Tanzania lakini kuna kitu anafeli.

“Namkubali sana Mwakinyo. Ila kuna kitu kimoja anafeli shabiki mwache abaki kuwa shabiki. Sio kila anayesema jambo lazima umjibu baadhi ya majibu wajibu kupitia ulingo," anaongeza Furahisha.

Anasema Mwakinyo tayari ni bondia mkubwa na anapaswa kuendelea kuonyesha ukubwa wake kupitia mapambano na si kumjibu kila anayemsema.

Mbali na Mwakinyo, Furahisha anawataja mabondia wengine anaowakubali na wenye uwezo mkubwa, Hassan Mwakinyo, Ibrahim Class, Juma Choki na wengineo.


SEMUNYU ANASTAHILI

Furahisha anamtaja Selemani Semunyu kama mmoja wa mapromota wanaofanya kazi kubwa kwenye tasnia ya ngumi na wanastahili pongezi kubwa.


"Kusema ukweli Semunyu anastahili kupongezwa kwa sababu ni miongoni mwa mapromota wanaofanya kazi yake kwa weledi mkubwa bila ya kubagua mabondia na kiukweli anaifanya tasnia ya ngumi izidi kulia," anasema Furahisha


HAYA YAKIFANYIKA

Kwa mtazamo wake, tasnia ya ndondi nchini bado ina nafasi kubwa ya kukua ikiwa viongozi na wadau wataweka maslahi ya mabondia mbele.

“Mapromota wanapaswa kushirikiana zaidi. Wapo wanaofanya kazi nzuri kama Semunyu, lakini bado tasnia inahitaji umoja wa wadau ili izidi kukua."

Pia anatamani viongozi wa Chama cha Ngumi wawe na msimamo mmoja badala ya migawanyiko inayoweza kuathiri maendeleo ya mchezo.

“Sisi mabondia kazi yetu ni kupigana. Tukipata viongozi wenye umoja na mapromota wanaoshirikiana, hata kiwango cha mabondia kitapanda.”


MIAKA MITANO IJAYO

Anapoulizwa anajiona wapi baada ya miaka mitano, Furahisha anajibu:

“Kila siku najiona nabadilika. Malengo yangu ni kuwa bondia bora zaidi, kushinda mikanda mikubwa na kuitangaza Tanzania kimataifa naamini ndani ya kipindi hicho nitakuwa bora zaidi."

Kauli hiyo inaonyesha wazi kwamba licha ya kupitia, maumivu, kudhulumiwa na changamoto za maisha Furahisha bado anaamini safari yake bado ndefu.