Prime
Freddy ‘Fungafunga’ ametuacha darasani bila jibu
Muktasari:
- Wiki mbili zilizopita alitangazwa kuachwa na Simba. Mchezaji ambaye alitua Simba dirisha la Januari tu akitokea Zambia ambako alikuwa mfungaji bora wa ligi hiyo hadi Simba walipoamua kutoa noti zao na kumtwaa. Alionekana kuwa suluhisho la matatizo ya Simba katika safu ya ushambuliaji.
NILIWAHI kuandika katika kolamu ya Jicho la Mwewe. Unaamini katika namba au unaamini unachokiona uwanjani? Freddy Michael, rafiki yangu Ahmed Ally alimpachika jina la ‘Fungafunga’ ametuachia somo jingine katika soka. Tumeachwa mdomo wazi.
Wiki mbili zilizopita alitangazwa kuachwa na Simba. Mchezaji ambaye alitua Simba dirisha la Januari tu akitokea Zambia ambako alikuwa mfungaji bora wa ligi hiyo hadi Simba walipoamua kutoa noti zao na kumtwaa. Alionekana kuwa suluhisho la matatizo ya Simba katika safu ya ushambuliaji.
Kocha mpya wa Simba, Fadlu Davids alimtazama Freddy pale Ismailia, Misri katika siku chache mazoezini akaona imetosha. Pale pale alitoa maagizo kwa viongozi wa Simba, Freddy alikuwa hatoshi katika kikosi kipya ambacho amekabidhiwa majukumu ya kukirudisha katika makali yake ya miaka mitano iliyopita.
Freddy huyu huyu ambaye kuanzia Januari alikuwa amefunga mabao ya kutosha hadi mwishoni mwa msimu. Alifunga mabao 11. Hapa ndipo dunia mpya ya soka inapotushangaza. Niliwahi kuandika hapa, kwa Freddy tutachagua kati ya tunachoona au namba zake.
Katika dunia ya sasa macho yetu yanaweza kuona kitu ambacho kompyuta haioni. Kocha Jose Mourinho aliwahi kudai wale wote ambao tunaangalia zaidi namba uwanjani basi hatufahamu soka. Tunaishi katika dunia ambayo unaweza kupiga pasi elfu moja dhidi ya ishirini za adui uwanjani halafu ukafungwa bao moja na kupoteza mechi.
Binafsi kwa Freddy sikuona maajabu katika mpira aliokuwa anaucheza katika dakika 90. Hakuwa na kasi, nguvu, wala mbinu kubwa. Hata hivyo, Freddy alikuwa anafunga. Ndio, alikuwa anafunga mabao mepesi. Hata hivyo, Mfalme wa soka duniani, Edson Arantes do Nascimento 'Pele' aliwahi kutuambia ‘mpira ni mabao’.
Hapo ndipo ambapo Freddy alikuwa anatufunga mdomo. Unaweza kudai alikuwa anafunga mabao ya kawaida, sawa, lakini alikuwa anafunga. Inawezekana alionekana amelegea uwanjani, inawezekana alikuwa anaonekana hana kasi wala nguvu lakini alikuwa anafunga.
Hadi leo hii ambapo Freddy ameachwa nadhani tumebaki midomo wazi. Kitu pekee ambacho kitaamua maamuzi haya na kitamuokoa kocha Fadlu ni pale ambapo mshambuliaji aliyeletwa atakuwa na sifa zote mbili. Kufunga mabao na kuonyesha uwezo mwingine mkubwa uwanjani.
Unaweza kuelewa kuhusu uwezo mwingine mkubwa wa uwanjani kama vile mshambuliaji kuchukua pia jukumu la kuunganisha timu, kupiga pasi za mwisho na mwengineyo yasiyohusu kufunga. Kama Lionel Ateba aliyechukuliwa kutoka USM Alger atakuwa na sifa hizo basi Fadlu na mabosi wa Simba watakuwa wamefaulu.
Kama Ateba atakuwa na sifa kubwa ya kimchezo, lakini akawa sio mfungaji mzuri basi bado kutakuwa na kesi kubwa ya kujibu katika namba zake pindi msimu utakapofika nusu tu. Nawajua Watanzania namna ambavyo wamekuwa mabingwa wa kulinganisha takwimu za wachezaji kwa siku hizi.
Tayari pale Simba kuna mchezaji kama Kibu Dennis ambaye amekuwa akifanya kazi kubwa uwanjani lakini mashabiki wamekuwa wakihoji kiasi kikubwa cha pesa kilichotumiwa na mabosi wa timu hiyo kumpa mkataba mpya wakati akiwa ameifungia timu hiyo bao moja tu.
Kifupi ni kwamba Kibu aliyecheza msimu mzima aliifungia Simba bao moja tu, wakati Freddy aliyeichezea Simba nusu msimu alikuwa amefunga mabao 11. Wakati huo huo Ateba aliyekuwa Algeria ameifungia USM bao moja tu kuanzia Januari.
Hata hivyo, katika hili la sasa ni ngumu pia kuwahukumu viongozi wa Simba kwa sababu aliyesema hamtaki mchezaji ni kocha wa Simba na sio viongozi. Huenda hili likawa jinamizi ambalo litamhukumu Fadlu kwa muda mrefu kama mabao yatatoweka Msimbazi.
Hata hivyo, kuna jicho lingine kali inabidi lianze kutumika kule ambalo wakubwa wa soka hili wamekuwa wakichukua wachezaji. Namaanisha katika ligi ambazo tumekuwa tukichukua wachezaji. Zamani tulikuwa tunachukua wachezaji kutoka katika soko la Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Malawi.
Baadae tukajiona tuna pesa zaidi za kwenda mbali na tukaanza kuchukua wachezaji kutoka katika ligi ambazo tunaamini zina wachezaji wanaojua mpira zaidi kuliko sisi. Zambia ni miongoni mwa ligi hizi. Mchezaji yeyote mwenye wasifu mkubwa kutoka Zambia tungemuona anafaa moja kwa moja katika ligi yetu.
Leo, mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Zambia ameonekana mchezaji wa kawaida katika ligi yetu. Siwezi kuwa mnafiki, hata mimi pia jicho langu la kwanza nilimuona Fredy kuwa mchezaji wa kawaida. Kwa nini alitisha Zambia? Tuhamishe soko?
Aliwahi kuja mshambuliaji kama Davis Mwape pale Yanga alikuwa ana mambo mengi mguuni. Alikuwa ametoka kuwa tishio pale Zambia na akaonyesha utishio wake. Leo Freddy ameonekana kuwa mchezaji wa kawaida tu. Hata Kennedy Musonda naye anaonekana kuwa mchezaji wa kawaida tu. Tuhamishe soko?
Kila la kheri kwake. Nasikia alikuwa mbioni kujiunga USM Alger, lakini dili limekwama na sasa yupo mitaa ya Dar es Salaam akijifua na mastaa wa Yanga. Lakini unaweza kujiuliza Freddy amebadilishana nafasi na Ateba. Na sasa utakuwa wakati mwafaka kwetu kupima nani amelamba dume na nani hajalamba dume. Inawezekana vipi USM Alger ilikuwa tayari kumuacha Ateba halafu wakamchukua Freddy. Wameona kitu gani? au mawakala wamefanya kazi yao vema? Tusubiri tuone!