Frank Sanga: Safari yangu ya miaka 10 na Mwanaspoti

SEPTEMBA 2003, nikiwa bado kijana kabisa, nikapokea simu. Aliyenipigia akajitambulisha kuwa anaitwa Theophil Makunga, Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) wachapishaji wa Gazeti la Mwananchi na Mwanaspoti. Bado kipindi hicho hakukuwa na Gazeti la The Citizen. Nilishtuka kupigiwa simu na Mzee Makunga, kwani alikuwa gwiji wa habari aliyefahamika na waandishi wengi nchini.

Baada ya kujitambulisha na kupeana salamu na mazungumzo ya dakika mbili tatu, Mzee Makunga akanitaka nifike ofisini kwake katika ofisi za MCL zilizokuwa Jengo la CCM Mkoa, ghorofa ya nane barabaraba ya Lumumba jijini Dar es Salaam.

Kabla sijakata simu, akaniambia kuwa wanatafuta mtu ambaye anaweza kuwa mhariri wa kuliendesha Gazeti la Mwanaspoti. Ingawa nilikuwa nimepanga kwenda kumuona baada ya kauli hiyo nikasita, sikwenda kumuona kama nilivyoahidi.

Nilikuwa nina sababu kubwa moja au mbili; mimi nilikuwa mwandishi wa michezo niliyependa kuzunguka huku na kule, mara nipo Msimbazi, mara Jangwani, mara nimesafiri na timu mbalimbali, mara niko Uwanja wa Taifa na maeneo mengine yaliyohusu michezo. Hayo ndiyo maisha niliyokuwa nimeyazoea na kuyafurahia katika kazi zangu enzi hizo.

Lakini sababu kubwa ilikuwa ni kwamba sijawahi kuwa Mhariri wa Michezo, hivyo sikuwa na uzoefu. Baada ya kujifanyia tathmini hiyo nikajiona siwezi kushika nafasi hiyo kubwa, hivyo sikwenda kumuona Mzee Makunga kama alivyonitaka nifanye.

Kipindi hicho nilikuwa mwandishi wa michezo wa magazeti ya Majira na Spoti Starehe, nikiwa na damu changa nikiwa ndio kwanza nimeshinda Tuzo ya Mwandishi Bora wa Michezo Tanzania tuzo zilizoandaliwa na Taswa, mgeni rasmi akiwa Waziri wa Mambo ya Nje, Jakaya Kikwete.

Niliendelea kufanya kazi zangu, sikuwa na mpango tena wa kwenda kuonana na Mzee Makunga. Baada ya miezi mitatu yaani ilipofika Desemba nikijiandaa kwenda likizo, Mzee Makunga akanipigia simu nyingine na kuongea na mimi kwa kirefu zaidi. Safari hii nilikwenda kuzungumza naye kwa sababu sikutaka kuonekana mtovu wa nidhamu.

Kutokana na ushawishi wake, nikajikuta nakubaliana naye kusaini mkataba, nikaenda likizo ya mwezi mmoja, likizo ambayo ilikuwa haina raha sana; ilikuwa ya kujuta, kujiona msaliti na wakati mwingine huzuni.

Haikuwa rahisi kuondoka nilikokuwa nafanya kazi, ilikuwa kazi ngumu, lakini mhariri wangu mkuu wakati huo, Masoud Sanani alinipa baraka zote baada ya kusikiliza sababu zangu za kuondoka, sababu yangu ilikuwa moja tu, kukua.

Januari 5, 2004 nikaenda kuripoti kazini makazi mapya ghorofa ya nane nikapokewa na dada wa mapokezi, Rehema Nzige, aliyenipeleka chumba cha habari ambako nilitambulishwa kwa waandishi wengine wa habari. Wengi tulikuwa tunajuana, kwa hiyo sikuwa mgeni kwao.

Nikatambulishwa vijana ambao watakuwa chini yangu; kwa habari za michezo za ndani walikuwa vijana wadogo; Michael Momburi na Zena Chande.

Kuandika habari za Simba na Yanga, ilikuwa lazima ufahamiane sana na viongozi wa klabu hizo pamoja na wachezaji wote. Waandishi wangu hawa walikuwa wachanga na hawakuwa wanafahamika sana kwa viongozi wa klabu mbalimbali. Mtihani wa kwanza ulianzia hapo.

Sikuwa na tatizo katika habari za kimataifa kwani nilikuwa naweza kuwatumia Innocent Munyuku (marehemu) na Mbonile Burton, waandishi waliokuwa wanachangia kuandikia pia habari za michezo za gazeti la Mwananchi, Timu ya Mwanaspoti ilikuwa na watu wachache sana, hatukuzidi wanne.

Timu ya Mwanaspoti ilikuwa na kompyuta moja tu tena mbovumbovu, ambayo waliitumia waandishi wote, hivyo nikawa ninawapisha waandishi wangu kuandika habari, wakimaliza ndiyo mimi ninakaa kwa ajili ya kuhariri na kufanya marekebisho mengine pamoja na kuongeza habari nyingine. Habari za Yanga na Simba nyingi nilikuwa naandika mwenyewe.

Ilikuwa kazi kubwa kwa sababu kama nilivyotambulisha mwanzo, waandishi wangu walikuwa wachanga, hawakuwa na uzoefu mkubwa kiasi kwamba habari nyingi za Yanga na Simba ilikuwa nazitafuta mwenyewe na kuziandika.

Mzigo ulipokuwa mzito, nikaanzisha utaratibu wa kuwachukua waandishi wangu kila jioni kwenda kwenye mazoezi ya Simba na Yanga. Huko nikawa ninawatambulisha kwa viongozi wa klabu hizo pamoja na wachezaji. Baada ya miezi kadhaa wakaanza kufahaminiana na wachezaji wa Simba na Yanga pamoja na viongozi. Mambo yakabadilika taratibu.

Ngoja nimalize hapahapa nisije kusahau, Momburi na Zena walipenda kazi yao na baada ya muda mfupi wakawa waandishi mahiri wa michezo, ingawa Zena aliondoka kwenda kujiunga na kampuni nyingine ya magazeti.

Hata hivyo tulikuwa na changamoto nyingi, mauzo ya gazeti yalikuwa madogo sana kiasi kwamba hata wamiliki wapya wa kampuni ya MCL yaani Nation Media Group (NMG) ya Kenya hawakuwa wakilipa uzito gazeti la Mwanaspoti, nguvu yao kubwa ilikuwa kuanzisha gazeti la Kiingereza The Citizen na kuimarisha gazeti la Mwananchi.

Changamoto zilikuwa nyingi licha ya kukosa vifaa kama kompyuta na kuwa na waandishi wachache hatukuwa na mtambo wa kuchapa magazeti, hivyo tukawa tunachapa kwa mitambo ya makampuni mengine hivyo kulazimika kuchapa saa sita mchana ili kuwahi foleni ya magazeti mengine, hiyo ilitufanya kukosa matokeo ya mechi za jioni za Ligi Kuu Bara. Ilikuwa changamoto kubwa iliyotupa akili ya kufikiri sana. Unauzaje gazeti la michezo bila matokeo ya mechi? Ilitufikirisha sana.

Kutokana na kukosa habari za matokeo ya ligi, tulilazimika kuandika habari kubwa kubwa na za kipekee.Tukaanza kuandika habari za pekee yetu (exclusives) ambazo zilikuwa hazipatikani katika magazeti mengine, tukaaminika kwa viongozi, wachezaji, tena wakawa wanatupatia habari za siri kuhusu usajili na ndio maana tukawa tunapata habari kubwa na kushtua za usajili kuliko magazeti mengine yote nchini.

Baadhi ya habari chache ambazo zilishtua wapenda michezo ni ile ambayo beki wa kushoto wa Simba, Ramadhani Wasso aliaga kwamba amepata timu Ubelgiji, hivyo Simba wakamuacha kwenye usajili wao, lakini baada ya wiki kama tatu, Mwanaspoti likaandika kuwa Wasso amesajiliwa Yanga. Ilikuwa ngumu kwa watu kuamini, kwa sababu kila mtu nchini aliamini kuwa Wasso amekwenda Ubelgiji.

Lakini habari nyingine ambayo ilitikisa sana ni ile ambayo Victor Costa alitoka Simba akaingia mkataba na Yanga. Simba wakafanikiwa kumtorosha na kumuweka nyumbani kwa mmoja wa viongozi wao kwa siri kubwa. Mwanaspoti likaandika Costa alivyotoroshwa Simba. Hakuna aliyeamini mpaka Costa alipojitokeza kwenye mazoezi ya Simba.

Tukabadilisha staili ya uandishi wa habari, ambao umedumu mpaka sasa, basi tukawa tunaandika vichwa vya habari vya aina yake, mathalani “Yanga hii tema mate chini’, “Simba acha kabisa”.

Inapofika mechi ya Simba na Yanga ilikuwa tunaandika vichwa vya habari kabla ya mechi, baada ya mechi ni kupachika tu, kila mwandishi alipewa uhuru wa kuandika kichwa cha habari, baadaye tungechagua kinachovutia zaidi, nakumbuka baadhi ya vichwa vya habari vilivyotumika zamani kama Titanic, Air Force One na B-52.

Kama nikiamua kutaja habari zote ambazo zilikuwa zinaandikwa na Mwanaspoti tu, itachukua mwaka mzima kuandika. Lakini kwa kifupi tu ni kwamba safari ya Mwanaspoti iliyokuwa na mabonde, ikabadilika na kuanza kupaa kwa kasi.

Baada ya miaka miwili, niliondoka kwa ruhusa maalumu ya kwenda masomoni Uganda, baada ya mwaka mmoja nikarejea na kuendeleza makali yaleyale, safari hii tukaongeza nguvu kwa kuwaleta waandishi wengine kwa vipindi tofauti wakaja Saleh Ally, Doris Maliyaga, Oliver Albert, Mohammed Abdul, Ndaya Kassongo na Said Pendeza, Khatimu Naheka na wengineo.

Meneja wa Usambazaji wa MCL, Hussein Bashe, ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Kilimo alifanya kazi kubwa kupandisha mauzo ya Mwanaspoti, hakuogopa kuchapisha nakala nyingi.

Bashe alikuwa ananifuata mara kwa mara kila siku tunayofanya uzalishaji akiniuliza tuchape nakala ngapi? Kuna kipindi mimi na yeye tukapanga tusiwe tunachapa chini ya nakala 50,000.

Hapo tayari kampuni ilikuwa na mtambo wake, hivyo mambo yakawa mazuri,nakala zikaongezeka kila siku tukafika mpaka nakala 120,000 baadhi ya siku na hasa Jumamosi.

Kutokana na mafanikio hayo, mtazamo wa wamiliki ulibadilika kabisa, Mwanaspoti likapewa sapoti kubwa sana, kila mwandishi akawa na kompyuta yake, waandishi wakaongezwa kama nilivyowataja hapo juu. Kila tulichokijaribu kikaenda vizuri, kila mpango ukakubali. Nzuri zaidi waandishi walipendana na kuishi kama familia.

Lakini jambo jingine ambalo lilisaidia sana Mwanaspoti kupanda kwa kasi ni kwamba tulituma waandishi kwenye kila tukio kubwa la michezo, hasa safari za nje ya nchi ambazo zilihusu Yanga, Simba au Taifa Stars.

Simba na Yanga zilikuwa na mtindo wa kwenda kupiga kambi ya wiki mbili au mwezi Uturuki, Omani au Afrika Kusini. Kote huko tulikuwa tunatuma mwandishi na kuripoti matukio kama yalivyo. Kumbuka wakati huo hakukuwa na mitandao ya kijamii.

Mwanaspoti likawa gazeti pekee kupeleka mwandishi Afrika Kusini kuripoti fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 kwa siku zote 30.

Kipindi fulani kulitokea malalamiko ya wasomaji kwamba tunaandika habari nzuri, ila wakataka tuimarishe na habari za uchambuzi.

Nakumbuka nilizungumza na Edo Kumwembe tukiwa Uwanja wa Taifa, na baada ya siku chache akajiunga nasi kwa ajili ya kuandika uchambuzi na habari za kimataifa. Tukaanzisha kolamu mbalimbali za uchambuzi kama Ninachokiamini ya Frank Sanga, Kurunzi ya Angetile Osiah, Mzee wa Kutibua ya Michael Momburi huku Edo Kumwembe tukimpa jukumu la kuandika chambuzi mbalimbali kama Hoja Yangu na nyinginezo.

Kwa mara ya kwanza, tukawa tunamleta mtaalamu kutoka Nairobi aliyekuwa anafanya mabadiliko ya muonekao wa gazeti na kuyatofautisha na mengine. Gazeti likawa linabadilishwa muonekano kila baada ya miaka mitatu au mitano.

Kutokana na ubora wa Mwanaspoti ilifika mahali watu wakawa wanawatuma watoto wao kwenda kununua gazeti bila kujua lina habari gani, maeneo mengine liliuzwa kwa bei ya juu(na mavenda) kutokana na watu kuligombea.

Mafanikio hayo, yakafanya kampuni ianzishe gazeti la Mwanaspoti Kenya, likiwa na habari za Kenya tu na linauzwa huko.

Safari yangu na Mwanaspoti ilikuwa ya miaka 10, iligota Februari 2014 nilipohamishiwa kuwa Mhariri Mtendaji wa Mwananchi kabla ya miaka michache baadaye kujiunga na Azam Media Limited (AML)

Jambo pekee ambalo linanifurahisha ni wale vijana wawili; Momburi na Zena . Miaka 17 baadaye Momburi amekuwa Mhariri Mtendaji wa Mwanaspoti na Zena ni Mhariri wa Michezo wa Habari Leo.

Maisha ni Safari.


Imeandikwa na FRANK SANGA