FOBA: Salim, Mshery mbona suala la muda!
Muktasari:
- Utatu huo wa makipa wa Azam FC, Foba pekee ndiye mwenye umri mdogo na hana rekodi tamu kama za wakongwe hao, lakini ameweza kupenya katikati yao akipata nafasi ya kucheza na kufanya kazi yake kwa usahihi.
ISSA Fofana, Aishi Manula na Zubeir Foba wanagawana dakika tu ndani ya Azam FC, wote wakiwa na lengo moja; kuhakikisha timu hiyo inafikia malengo iliyojiwekea.
Utatu huo wa makipa wa Azam FC, Foba pekee ndiye mwenye umri mdogo na hana rekodi tamu kama za wakongwe hao, lakini ameweza kupenya katikati yao akipata nafasi ya kucheza na kufanya kazi yake kwa usahihi.
Manula aliyerejea kikosini hapo msimu huu akitokea Simba, alipokaa takribani mwaka mzima bila kucheza, ametamba upande wa Kombe la Mapinduzi alipodaka mechi zote tano ilizocheza Azam iliyopoteza fainali kwa penalti 5-4 dhidi ya Yanga. Pia amedaka mechi za Ligi Kuu Bara.
Fofana, kipa raia wa Ivory Coast, amejiunga na timu hiyo ukiwa ni usajili wa kocha Ibenge kutokana na kufahamiana vizuri na kocha huyo. Yeye pia amedaka mechi chache za Ligi Kuu na moja Kombe la Shirikisho.
Sio Azam tu, Foba alikwenda Afcon 2025. Baada ya Yakoub kuumia, akachukua mikoba, naye akaumia, akamalizia Masalanga wakati Taifa Stars ikiishia 16 bora. Sasa amerejea kikosi na anaendelea na mapambano. Amezungumza na Mwanaspoti na kufunguka mambo mbali mbali, ikiwa ni pamoja na namna ambavyo amekuwa akiaminiwa na kupewa nafasi ya kucheza.
KUMLEA HADI KUMUAMINI
Foba ni zao la akademi ya Azam FC, kutokea mji wa Musoma mkoa wa Mara. Kipa huyo alipandishwa msimu wa 2022/23 na kuendelea kuwa chini ya makipa waandamizi akijifunza, na sasa anacheza kikosi cha kwanza huku akipata nafasi ya kuitwa timu ya taifa.
Foba ametoa uhakika kwa taifa kuwa na kipa wa kumtegemea kwa miaka mingi ijayo, kutokana na umri wake wa miaka 23. Kama ataendelea kuimarika na kupata uzoefu zaidi, anaweza kutawala nafasi yake kwenye kikosi cha timu ya taifa kwa miaka 10 ijayo.
Foba na Azam FC ni kama walizaliwa kuishi pamoja kwani tayari amejihakikishia nafasi ya kucheza. Anaweka wazi kuwa haikuwa rahisi kwake, amevumilia sana na kujipa imani kuwa anaweza, hadi sasa anapata nafasi ya kucheza.
“Nimepandishwa kutoka timu ya vijana, nimefanya kazi na makipa wengi wa kigeni na wazawa. Hii imenijenga kwani ni muumini wa kukubali kujifunza bila kukata tamaa. Nawashukuru makocha na hata makipa kwa kunifikisha hapa,” anasema Foba.
“Imani kubwa iliyojengeka kwangu sio ya bahati, ni kupambana na kuondoa hofu ili niwe imara kila ninapopata nafasi ya kucheza. Namshukuru Mungu kwa hili na bado ntaendelea kupambana zaidi na kujifunza kwa kila mtu ili niendelee kuwa bora.”
Anasema amepita chini ya makocha wengi na hawezi kuwataja mmoja mmoja, lakini anawashukuru kwa nafasi waliyompa ili aonyeshe kipaji wakiwa chachu kwake kucheza timu ya taifa.
AFCON DARASA LA UBORA
Tanzania ni mojawapo ya nchi wenyeji rasmi wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ikishirikiana na Kenya na Uganda, na tayari imeanza kufanya maandalizi kwa ajili ya kuandaa kwa ubora. Wakati hayo yakiendelea, Foba amesema anatamani kuwa sehemu ya wachezaji watakaoiwakilisha Tanzania.
“Kuwa sehemu ya nyota wanaoipambania nchi ni jambo kubwa. Kila mchezaji anatamani, ukiondoa uwakilishi wa nchi, pia ni fulsa kwa mchezaji kujiongezea uzoefu kwani ni michuano ambayo inakutanisha wachezaji wengi kutoka nchi mbalimbali shindani.
“Natamani kuwa sehemu ya kikosi kitakachoitwa. Kama nitapata nafasi ya kuitwa ni hatua moja, kuhusu kucheza ni nyingine, lakini endapo nitaitwa tu ni fulsa kwangu. Hata nisipocheza kuna mengi nitayabeba kwa kujifunza kupitia kutazama,” anasema.
Anasema kuwa sehemu ya kikosi bila hata kucheza kwake ni darasa kubwa kwani anawatazama kwa ukaribu makipa bora kutoka mataifa mbalimbali na kuchukua mazuri yao ambayo atayatumia kwenye kikosi chake.
“Unajua kujifunza sio kwenye kucheza pekee, hata ukiwa nje ya timu ukizingatia unachohitaji kuwa nacho kwa usahihi inawezekana, lakini cha muhimu ni kuamini katika kukubali ubora wa mwingine na kuchukua kwa kufanyia kazi.”
MANULA, FOFANA WAALIMU
Wadau wengi waliamini kuwa mara baada ya Azam FC kufanya usajili eneo la kipa ni mwisho wa Foba kwani ameongezewa nyota bora na wazoefu, lakini mwenyewe anasema yalikuwa mawazo yao, ila upande wake imekuwa fursa kwani anawatumia makipa hao kujiweka kiushindani.
“Naheshimu ubora wa Fofana na Manula. Ni wazoefu kwangu na wana rekodi nzuri za ubora. Kujiunga pamoja na mimi imekuwa nafasi nyingine bora kwangu kwani wananichukulia kama mdogo wao. Wamekuwa wakinikosoa ninapokosea na kunielekeza nini nifanye ili niwe bora zaidi," anasema.
“Tayari wameshafanya mambo makubwa ambayo mimi bado sijayafikia, hivyo wamekuwa wakiniongoza ili niweze kuwa bora. Nafurahia uwepo wao, wananijenga. Nikikosa nafasi ya kucheza nawatazama ili kuchukua ufundi wao. Pia hata mimi nikicheza wanachukua upungufu wangu na ubora. Baada ya mechi wananiita na kuniambia nilikuwa bora wapi na nimezingua wapi.”
Foba anasema wawili hao hawapo kwa ajili ya kumpa changamoto ya kupambana tu, lakini pia wamekuwa walimu bora, hivyo anajua kuwa wote ni sehemu ya kuendelea kuwa imara na kutokuwa na hofu kwani anaamini katika muda asipocheza kuna vitu anapata, lakini pia akicheza anaendelea kuwa darasani.
KIMATAIFA WALIKWAMA HIVI
Azam FC inaiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa ikiwa katika Kombe la Shirikisho Afrika na haikuanza vizuri mechi mbili za mwanzo za makundi ikipoteza zote na kuzinduka kuanzia mechi ya tatu, na sasa tayari ina pointi tisa. Foba anasema sababu ya kuanza vibaya ni kukosa mwendelezo wa kushiriki mara kwa mara ili kupata uzoefu.
“Mechi mbili za mwanzo tulianza kwa presha na hatukuwa na uzoefu kwenye michuano, lakini sasa chini ya kocha Frolent Ibenge tumejengewa kujiamini na ndio maana tumeweza kushinda mechi mbili mfululizo,” anasema.
“Hatuna hofu na tayari tumeamini katika kujitoa ili kujiweka kwenye mazingira bora ya ushindani. Tunaitaka robo fainali na tunaamini mchezo ujao ugenini (dhidi ya Wydad leo) tutapata matokeo ambayo yatatupa nafasi ya kuandika historia nyingine baada ya kutinga makundi kwa mara ya kwanza.”
Anasema timu ina wachezaji wenye ubora na ushindani, na wapo tayari kushindana kwa lengo la kuifanya iweze kufikia malengo.
UVUMILIVU MTAJI WAKE
Kuna methali inasema, “mvumilivu hula mbivu.” Hii imeenda vyema kwa Foba kama ambavyo anabainisha kuwa amepita katika 'moto' hadi sasa amekuwa dhahabu safi kwani alianza kusugua benchi na sasa anapata namba mbele ya mastaa wakubwa wenye rekodi.
“Azam FC nimekaa muda mrefu. Nilikuwa sipati namba, nakaa benchi nikishuhudia makipa mbalimbali wakipata namba ya kucheza, wageni kwa wazawa. Sikuwahi kukata tamaa, niliamini ni suala la muda. Muda wangu ni sasa pamoja na kwamba sina namba ya kudumu, lakini nacheza.
“Fofana na Manula ni makipa bora na wakubwa kwa kila mmoja kwenye nchi walizocheza. Manula hakuna asiyefahamu rekodi zake nzuri Simba na hata Azam FC kabla ya kuondoka akiwa ameipa taji la ligi. Wote nacheza nao pamoja, wana uzoefu mkubwa, lakini kocha amekuwa akiniamini na kunipa nafasi ya kucheza,” anasema.
Foba anasema haikuwa rahisi kwake kufika alipo kwa sababu alilazimika kuvumilia mengi na kuwa na imani kuwa kuna muda atapata nafasi na atafanya vizuri. Ndicho kinachotokea sasa huku akitoa wito kwa wachezaji kuwa wanatakiwa kuamini katika vipaji vyao, mpira ni mchezo wa wazi watu wanaona.
MSHERY, SALIM SUALA LA MUDA
Licha ya wazawa wengi kufanya vizuri Ligi Kuu Bara, Foba anawataja Ally Salim ambaye sasa anakipiga Dodoma Jiji na Aboutwalib Mshery kuwa ni makipa bora licha ya kupitia nyakati ngumu kutokana na kuletewa changamoto vikosini.
“Makipa wa kigeni licha ya kuziba nafasi za baadhi ya makipa mfano Yanga, Djigui Diarra, amekuwa kikwazo kwa Mshery, lakini haijawahi kumshusha ubora na uimara. Apatapo nafasi amekuwa akifanya vizuri. Naamini ni kipa ambaye anaamini katika kujifunza kupitia mshindani na kujitunza,” anasema.
“Hivyo hivyo ilikuwa kwa Salim akiwa Simba. Makipa wengi wa kigeni waliopita Simba akiwemo mzawa Manula walikuwa wakimweka benchi, lakini akipewa nafasi alikuwa anacheza kwa ubora. Hivyo ndivyo inatakiwa ili kujiweka katika daraja bora la ushindani.”
Foba anasema hivi sasa Salim amekuwa bora nje ya Simba akisimama mwenyewe Dodoma Jiji. Uzoefu na kukubali changamoto kumemjenga, hivyo ameweka wazi kuwa hiyo ndio moja ya siri ya kuwa bora ni kuamini katika kipaji.
FAIDA, HASARA MAKIPA WA KIGENI
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), msimu huu limepitisha kanuni ya timu kusajili kipa mmoja wa kigeni na hilo limepokewa vizuri na Foba anayedai kuwa kipa mmoja wa kigeni ni sawa licha ya kuwa na faida na hasara.
“Faida ni namna ambavyo makipa wa kigeni wanavyoongeza ushindani na kutupa vitu bora ambavyo hatuna. Tumekuwa tukivichukua na kuviongeza katika ukuaji, na kuongeza ubora ili ushindani uendane na ushindani tunaoupata," anasema mchezaji huyo.
“Hatuwezi kuzuia makipa hao wasisajiliwe, japo kuna wengine wanakuja tunakuwa na uwezo sawa na wao, lakini wanabebwa na kigezo cha ugeni kupata nafasi ya kucheza. Hilo haliondoi sisi kupambana zaidi ili tupate nafasi ya kucheza.”
Foba anasema amepata nafasi ya kucheza na makipa wengi bora wa kigeni, akitumia nafasi hiyo kuchukua vitu vizuri kutoka kwao ili kujiongezea ubora, hivyo anajivunia na ndiyo faida aliyoipata sambamba na kuongezewa ushindani wa namba.
KUMTAZAMA HADI KUCHEZA PAMOJA
Kila mchezaji ana mtu ambaye amekuwa akimtazama kwa lengo la kujifunza kutoka kwake na kuwa sehemu ya mafanikio hadi kupata nafasi ya kucheza soka, kama anavyodai Foba.
“Hadi nimefika hapa nafikiri ni ubora wa Manula ndiye aliyenifanya nipende mpira na nimeanza kumtazama muda mrefu sana hadi sasa nimepata nafasi ya kucheza naye,” anasema na kuongeza:
“Manula ndiye 'role model' wangu. Nilianza kukaa langoni nikivaa jezi namba 28 ni kwa sababu ya Manula. Nilitamani kila kitu nifuate kutoka kwake. Nafurahi kwa kiasi nimefanikiwa na naendelea kuwa mwanafunzi chini yake.
“Hata siku nilipoambiwa Manula anakuja kucheza Azam FC niliongea na meneja wa timu kuwa kwa heshima naomba kumpatia Manula namba yake 28 kwa sababu nafahamu namba zina maana. Tangu nimeanza kumuona anaivaa huenda ina bahati kwake.”
Anasema baada ya kumkabidhi alichagua kuvaa namba 32 ambayo anaivaa hadi sasa, huku akidai kuwa kwake ni ya bahati kwani ndiyo alikuwa akivaa akiwa timu ya vijana ya Azam FC hadi siku alipopandishwa timu ya wakubwa.
“Kwangu jezi namba naangalia bahati na siyo kama wengine wamekuwa wakitumia tarehe zao au miezi ya kuzaliwa. Mimi nilianza na 28 mara baada ya kupandishwa, kwa ajili ya Manula, kwani ndiye kipa ambaye nilikuwa nikimtazama kwa kujifunza vitu, na 32 ni namba ya bahati kwangu baada ya kuivaa ilinipandisha hadi timu ya wakubwa ambayo anacheza hadi sasa.”