Fei Toto akibugi kidogo inakula kwake

Muktasari:
- Aliwahi pia kusikika, Eden Hazard katika mahojiano yake na John Obi Mikel akisema kwamba hakuwahi kupenda mazoezi ya kujituma sana, na alipojaribu kufanya hivyo ndipo ukawa mwisho wa maisha yake ya soka akiwa na Real Madrid kwani aliandamwa na majeraha ya mara kwa mara yaliyosababisha aamue kustaafu soka.
ALIWAHI kusikika mchezaji wa zamani wa Barcelona, Kevin Prince Boateng akimzungumzia Lionel Messi katika moja ya mahojiano yake akisema fundi huyo wa timu ya Inter Miami na Argentina hakuwahi kumuona akiingia gym kwa ajili ya kufanya mazoezi, na mara kadhaa alizoingia ilikuwa ni kwa ajili ya kufanyiwa masaji na kucheza mpira wa kikapu.
Boateng na Messi waliwahi kucheza pamoja Barcelona.
Aliwahi pia kusikika, Eden Hazard katika mahojiano yake na John Obi Mikel akisema kwamba hakuwahi kupenda mazoezi ya kujituma sana, na alipojaribu kufanya hivyo ndipo ukawa mwisho wa maisha yake ya soka akiwa na Real Madrid kwani aliandamwa na majeraha ya mara kwa mara yaliyosababisha aamue kustaafu soka.
Sio wachezaji wote wanapata bahati ya kucheza kwa kiwango kikubwa na kufanya makubwa bila ya kuweka juhudi za ziada. Ni wachache wanaobarikiwa.
Tanzania imebahatika kupata wachezaji wa aina hiyo, mmoja wao akiwa ni Feisal Salum 'Fei Toto' anayekipiga katika kikosi cha Azam FC.

Huwezi kupita katika ukurasa wake ukaona ameweka picha akiwa gym au anakimbia katika fukwe za bahari. Awapo uwanjani huwezi kutoa kasoro katika utimamu wake wa mwili. Atakupa asilimia 100 ya kile ambacho wengine wanakupa.
Wakati wachezaji mbalimbali wakishindwa kuendana na matakwa na makocha wapya au mifumo ya timu mpya, hilo huwezi kuliona kwa Feisal. Aliwahi kucheza kama kiungo mkabaji akiwa chini ya Mwinyi Zahera katika kikosi cha Yanga, akacheza kiungo namba nane, 10 pia akiwa na makocha wengine kama Nassredine Nabi (Yanga) na Youssouph Dabo (Azam FC).
Kwa mujibu wa tovuti za Wikipedia na Transfermarket, Feisal alizaliwa Januari 11, 1998, Zanzibar, ikiwa na maana mwaka huu tarehe kama hiyo atakuwa anatimiza miaka 27.

Tangu atue Bara 2018 hadi sasa, amekuwa mmoja kati ya wachezaji bora katika ligi. Licha ya uwepo wa mastaa kutoka nchi mbalimbali wanaocheza katika eneo analocheza bado Feisal ameonyesha kutobadilika.
Karibu kila timu ndani ya Ligi Kuu Bara ingehitaji huduma yake ikiwa inapatikana.
Kwa sasa ana mkataba na Azam hadi mwisho wa msimu ujao, lakini tayari Kaizer Chiefs na Wydad Casablanca zimekuwa zikitajwa kutaka kumsajili.
Inawezekana akawa amechelewa sana kucheza katika ligi ya ndani, lakini huu unaweza kuwa muda sahihi wa staa huyo kupata cha kusimulia dakika za mwisho za soka lake.

Kiwango chake kinahitaji kupaa zaidi ya pale alipo kwa kucheza katika mataifa mengine ndani ya Afrika na ikiwezekana nje ya bara hili.
Wakati Neymar anajiunga na Barcelona 2013 haikuwa kwa sababu ya pesa pekee, bali ilikuwa ni kwa ajili ya heshima kwa sababu alishaanza kutajirika kabla hata ya kutoka nje ya Brazil, ikizingatiwa kwamba mwaka 2010 alishanunua boti ya kifahari.
Huenda Neymar asingefikia umaarufu pale alipo ikiwa angeendelea kubaki Santos ya Brazil na hilo Wabrazili waliliona na moja ya kampeni yao ilikuwa kumuona akiondoka kwenda Ulaya wakiamini huko ataboresha zaidi wasifu wake zaidi ya pale alipokuwa na kupata heshima zaidi. Feisal pia anahitaji heshima hii.

Achana na Neymar, rudi England. Nahodha wa timu ya taifa hilo, Harry Kane alikuwa hatarini kwenda kumaliza safari yake ya soka bila kushinda taji lolote akiwa na klabu. Hiyo ingekuwa dhambi katika mpira wa miguu. Waingereza waliliona hilo.
Kane hakwenda kujiunga na Bayern Munich akitokea Tottenham Hotspur kwa sababu alihitaji pesa, hapana. Spurs ilikuwa na uwezo wa kumlipa sawa na kile ambacho anakipokea kwa sasa akiwa na Bayern Munich, lakini Kane alihitaji heshima.
Hapa nchini kuna kizazi ambacho kilikuwa bora enzi zake, lakini mwisho haukuwa wa kuvutia na mafanikio makubwa.
Hakuna mtu ambaye angebisha juu ya uwezo mkubwa wa kufunga wa Kane, lakini tuzo za viatu vya dhahabu alizoziweka kabatini kwake zisingekuwa na maana ikiwa asingeshinda kombe lolote.
Hii ni sawa tu na ilivyo kwa Feisal. Hakuna mwanadamu katika ardhi hii anayeweza kupinga juu ya kipaji na uwezo wake, lakini historia yake itakuwa rahisi sana kusahaulika ikiwa hana alama kubwa atakayoiacha.

Kuna wazee wanaotoa hadithi nyingi kuhusu wachezaji wa zamani, wakiwasifia sana. Lakini hadithi zao zimekuwa sio zenye kuimbwa kwa sababu hawakuwa na mafanikio makubwa nje ya mipaka ya nchi.
Leo hii, jina la Samatta limeandikwa kila kona ya hadhithi za mpira wa Tanzania, lakini angeendelea kubaki hapa nchini stori yake ingekuwa ya kawaida kama zilivyo nyingine.
Wakati fulani aliwahi kutokea Ibrahim Ajib hakuna aliyekuwa na maswali juu ya kipaji chake, lakini hivi sasa anaichezea Dodoma Jiji ambako pia kuna muda huanzia benchi.
Vilevile aliwahi kuwepo mmoja kati ya makipa bora, Juma Kaseja. Heshima aliyonayo katika soka la Afrika ni tofauti na ilivyo kwa kipa wa Uganda, Denis Onyango aliyepata mafanikio makubwa akiwa na Mamelod Sundown aliyoitumikia tangu 2011.
Waliwahi pia kuwepo mastaa kama Kelvin Yondani na Juma Nyosso ambao walipata mafanikio makubwa wakisimama kama mabeki bora, lakini stori zao hazizungumzwi sana kwa sababu waliishia hapahapa. Hawana hatua kubwa ya kimpira waliyoipita.
Leo ni rahisi kusikia jina la Sunday Manara 'Kompyuta' si kwa sababu alikuwa bora peke yake, hapana. Bali alithibitisha ubora wake nje ya nchi. Huenda alikuwa na wenzake wengi waliokuwa bora zaidi yake, lakini hadithi inayoendelea kushi katika vichwa vya habari ni ya kwake.
Kucheza Uholanzi na Austria zimekuwa moja kati ya alama zinazomtambulisha Sunday licha ya kwamba aliwahi pia kupita Yanga.