FARUK BEY: Mapenzi yanavyomsumbua ndani, nje ya EverMore
Muktasari:
- Nyota huyo aliyezaliwa 1972 Ankara, Uturuki, amejijengea umaarufu mkubwa kupitia tamthilia na filamu zinazohusu mapenzi yenye majonzi, mateso na misukosuko ya maisha ya familia.
KATIKA historia ya filamu na muziki wa Kituruki, wachache wameweza kuunganisha sanaa na maisha halisi kwa namna ya kipekee kama Ozcan Deniz maarufu Faruk Bey.
Nyota huyo aliyezaliwa 1972 Ankara, Uturuki, amejijengea umaarufu mkubwa kupitia tamthilia na filamu zinazohusu mapenzi yenye majonzi, mateso na misukosuko ya maisha ya familia.
Lakini cha kushangaza simulizi hizo za kisanii zimekuwa zikiendana pia kwenye maisha yake halisi kana kwamba waongozaji wanagusa maisha anayoishi.
Katika filamu na tamthilia alizoigiza kuanzia Asmali Konak (2003) hadi EverMore (2017) kwa Kituruki A°stanbullu Gelin, Faruk amejikuta akikumbana na hekaheka kwenye mapenzi kutokana na vikwazo vya kifamilia.
Kwenye tamthiliya, watazamaji wamezoea kumuona akilia na kupigania mapenzi yasiyowezekana au kuachwa na mtu anayempenda zaidi. Uhusika anaopewa mwingi kwenye tamthilia hizo umefanya aonekane kama mwanaume anayeteswa na mapenzi.
Lakini, uhalisia huo unaakisi picha hiyo kwenye maisha yake binafsi ambayo aliwahi kuoa na kuachana na wake kadhaa kwa migogoro, mivutano na ndugu kuhusu mahusiano ya kimapenzi.
Vyote vinalingana na vinaonyesha si tu kwenye tamthilia anazoigiza, bali anapitia changamoto hizo kwenye maisha halisi.
Mwanaspoti linakuletea kwa kina Faruk Bey ni nani, kazi na maisha yake binafsi.
MAISHA BINAFSI NA KAZI
Kile unachokiona kwenye tamthilia ya EverMore, kwa asilimia kubwa anachoigiza Faruk Bey ndiyo maisha yake halisi kuanzia kwa wazazi hadi maisha ya ndoa.
Kwenye moja ya mahojiano aliyowahi kufanya, Faruk alisema katika maisha yake ya utotoni walikuwa karibu na mama kwani baba alikuwa na wanawake wengi na hawakupata muda mwingi wa kuzoeana naye.
Ndani ya tamthilia hiyo, baba yake - Boran alikuwa na mwanamke mwingine ambaye alizaa naye mtoto mmoja aliyeitwa Adem na kutokana na kutengana kwa wazazi wake kulimfanya ajae chuki moyoni na kuanza kuitesa familia ya upande wa baba.
Faruk alimuoa Sureyya Hanam, mwanamke ambaye ni mdogo kiumri, ndoa ambayo ilikuwa na mgogoro mkubwa kutokana na mama yake mzazi, Esma Hanam kutomridhia mwanamke huyo akiamini hakuwa na maadili yanayoakisi familia yao kwani Sureyya alikuwa anakesha baa akiimba.
Bila kujua, Sureyya aliingia kwenye ndoa na Faruk, mtoto wa kwanza wa familia ya Boran ambaye hapo awali alikuwa na mwanamke mwingine, Begum, na aliondoka Uturuki na kuhamia Marekani kikazi akiwa na mimba bila kujua kutokana na shinikizo la Esma ambaye naye hakuridhia mahusiano hayo.
Kiuhalisia, Faruk (53) ndoa yake ya kwanza ilikuwa 1992 nchini Ujerumani na alimuoa Handan Deniz. Ndoa hiyo haikudumu muda mrefu, mwaka 2003 wakapeana talaka na kuachana.
Akamuoa Feyza Aktan 2018 na wawili hao wakapata mtoto wa kiume aitwaye Kusey. Vyombo mbalimbali vya habari Uturuki vikaripoti kuwa supastaa huyo alikuwa na mzozo mkubwa na mkewe. Mwaka 2019 wakaachana.
Miaka minne baadaye akamuoa mwanamitindo na mbunifu kutoka Iran, Samar Dadgar mwenye miaka 22. Ndoa hiyo imedumu hadi sasa, lakini inaelezwa mama yake Faruk hakuridhia ndoa hiyo shidi ya binti mdogo.
Hata kwenye ndoa yao, mama yake mzazi na familia ya Faruk haikuhudhuria. Kurudisha nyuma kidogo kwenye tamthilia, ndivyo ilivyokuwa, Esma hakutokea kwenye ndoa ya mwanawe na alifunga ndoa akisindikizwa na mdogo wake wa pili Osman Boran.
Tabia zinazoelezwa za msanii huyo hazina tofauti na maisha yake halisi kwani hadi sasa hana maelewano mazuri na familia yake kutokana na kumsema mkewe Samar kuwa aliolewa kufuata mali na si upendo halisi.
Pamoja na mzozo huo, lakini bado Ozcan maarufu Faruk Bey aliendelea kukumbusha kwenye mitandao ya kijamii kuwa ataendelea kuwa upande wa mkewe kama ilivyo kwenye tamthilia ambapo alikuwa mstari wa mbele kumtetea Sureyya hata pale ambapo mama yake mzazi hakumuamini.
MWANAMUZIKI
Nyota huyo ni mwanamuziki mkubwa Uturuki akiimba zaidi muziki wa pop na folk ambao ni muziki wa kitamaduni nchini humo. Kwa Tanzania ni kama taarabu au singeli.
Mbali na kuigiza na kuimba, pia ni mtunzi na muongozaji mzuri wa filamu na kipaji hicho ndicho kilianza kumleta kwenye ramani ya sanaa.
“Tangu nikiwa shule nimekuwa nikiandika mwenyewe na kuigiza mbele ya maelfu ya watu. Nimekuwa nikipata pesa huko na kusaidia familia yangu. Nikiwa na miaka 12 tu nilikuwa kama baba kwenye familia yangu,” aliwahi kusema kwenye moja ya mahojiano yake.
Faruk anasema alirithi kipaji cha kuimba kutoka kwa baba yake mdogo Shakiro Dengbej aliyekuwa maarufu nchini humo, Australia na Canada.
“Nadhani nimerithi sauti yake. Wengi waliomfahamu walisema nafanana naye sauti, nimekuwa nikisikiliza kanda za nyimbo zake tangu nikiwa mdogo,” anasema.
Kama wasemavyo Wabongo, ‘mubaba’ huyo amejaliwa vipaji vingi ikiwamo kuimba, kuigiza na kuongoza filamu ingawa kwa sasa hafanyi kwa ukubwa kama ilivyo kuigiza na kuimba.
Baadhi ya ngoma zake ni pamoja na Her Sey DegiÅŸir aliyoitoa 2009, Merakimdan (2012), Ask (2019), Allah Buyuk (2020), Ben Yine Kendimle (2020) na AyrA±ntA±larda Gizli (2020). Mara ya mwisho msanii huyo kutoa albamu ni mwaka 2012 iitwayo Bi Dusun. Tangu hapo amekuwa akishirikishwa kwenye nyimbo za wasanii wengine.
Albamu nyingine ni Yine AglattA±n Beni (1992), Hadi Hadi Melegim (1993), Beyaz Kelebegim (1994), Yalan Mi? (1997), Coban YA±ld-A±zA± (1998), Aslan Gibi (2000), Leyla (2002), Ses ve Ayrilik (2004), Hediye (2007) na Sevdazede (2009).
FILAMU ALIZOIGIZA
Ukiitoa EverMore ambayo ilimpa umaarufu mkubwa duniani aliwahi kuigiza filamu kama Yalan (1997) akiigiza kama Hassan. Nyingine ni Askin Daglarda Gezer (1999) aliigiza kama Zal, AsmalA± Konak (2002/2003), Haziran Gecesi (2004), Kader (2006), Ask Yakar (2008), Samanyolu (2010) na nyinginezo. Kwenye orodha ya wasanii wenye utajiri mkubwa nchini humo, Faruk anakadiriwa kuwa na utajiri wa Dola 40 milioni 40.