Fadlu Davids Raja ilikuwa suala la muda
Muktasari:
- Baada ya kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Kawkab Marrakech, ripoti kutoka vyanzi maarufu vya habari nchini Morocco na Afrika kijumla zinasema jamaa wapo katika hatua za mwisho kumvunjia mkataba wake.
NDOA ya Kocha Fadlu Davids na Raja Casablanca ya Morocco ina dalili zote zinazoonyesha inakaribia kuvunjika.
Baada ya kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Kawkab Marrakech, ripoti kutoka vyanzi maarufu vya habari nchini Morocco na Afrika kijumla zinasema jamaa wapo katika hatua za mwisho kumvunjia mkataba wake.
Ikitokea Fadlu akatimuliwa, sisi hapa kijiweni tunaona litakuwa ni jambo la kawaida kwa vile maisha ya soka la Uarabuni yanafahamika.
Wale jamaa wana kiburi cha fedha na mara zote wanahitaji timu zao zipate matokeo mazuri kwa vile wanafanya uwekezaji mkubwa.
Ikitokea timu imeyumba kidogo tu kwa matokeo ya uwanjani, usitegemee kuona kocha akiwa katika maisha yasiyo na presha kwani wanao uwezo wa kumtimua na kumlipa fidia.
Bahati mbaya ya Fadlu Davids ameenda katika timu kubwa na inayoongoza kwa kupendwa zaidi Morocco ambayo imekuwa na kiu ya kurejesha taji la Ligi Kuu ya Morocco ambalo ililikosa msimu uliopita.
Mwanzo mzuri ambao ilikuwa nayo msimu huu ulishawapa matumaini wanaelekea kutimiza ndoto hiyo lakini hali imebadilika mwishoni.
Kupoteza kunawafanya sio tu waendelee kupoteza matumaini ya kutwaa taji bali pia yanazidi kuwashusha kwenye msimamo wa ligi.
Ni vigumu Raja Casablanca kuvumilia kukosa ubingwa wakati huohuo kukosa hata nafasi ya kucheza mashindano ya klabu Afrika. Uvumilivu huo hawana.