Rweyemamu afichua kile watu wasichokijua kuhusu Ajibu
Muktasari:
- Anasema vijana wanaotaka kufanikiwa kimaisha wawe wachezaji au wanaofanya kazi zingine, sehemu wanapoishi wasichonge kabati za kuhifadhia fedha, badala yake liwe la kutunzia vitabu vinavyotoa elimu mbalimbali ya kimaisha na ndani yake wanaweza wakatunzia pesa.
KAMA kuna kitu anakiamini meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu basi ni kufanya majukumu yake ni ukweli na unyoofu wa mambo, vitu vinavyomsaidia kurahisha kazi yake na kujenga mahusiano mazuri na wachezaji.
Anasema vijana wanaotaka kufanikiwa kimaisha wawe wachezaji au wanaofanya kazi zingine, sehemu wanapoishi wasichonge kabati za kuhifadhia fedha, badala yake liwe la kutunzia vitabu vinavyotoa elimu mbalimbali ya kimaisha na ndani yake wanaweza wakatunzia pesa.
Akifafanua kauli yake:"Ili ufanikiwe katika uongozi wa kitu chochote huwezi kukwepa elimu, mimi nimesoma na bado nasoma hilo linanisaidia kujua jinsi ya kuishi na wachezaji bila changamoto ya aina yoyote na wengi wao ukiwauliza watakwambia mimi ni mtu wa aina gani.
Anaongeza:"Siamini katika unafiki na majungu, nikikosea niambie sasa bahati mbaya katika sekta hii imeingiliwa na watu wasiyo wa kweli na mpira wa miguu unahitaji unyoofu, kwa sababu unachezwa kwa uwazi."
Katika mahojiano hayo, yaliyofanyika Uwanja wa Mo Simba Arena uliyopo Bunju aligusia mambo mbalimbali.
ANAVYOISHI NA WACHEZAJI
Rweyemamu anasema haijawa ngumu kwake kuishi na wachezaji kwa kuzingatia nidhamu, kwanza amesoma shule za wanafunzi watukutu enzi hizo:" Nafahamu niishi nao vipi pia huwezi kufanikiwa bila kusoma, mimi nasoma hadi kesho na nimetunza daftari za kuanzia chekechea hadi chuo, hivyo najua lugha ipi ya kwenda nao sawa.
Anasema zaidi ya wachezaji 290 waliyopitia Simba B bado wanacheza katika timu mbalimbali za Ligi Kuu, Championship na Ligi Daraja la Kwanza.
"Nawafuatilia wanaendelea kupambana kuonyesha vipaji vyao na wengi wao nimekaa nao nyumbani kwangu."
Miongoni mwa wachezaji waliyopita mikononi mwake akiwa na kikosi cha Simba B ni Ibrahim Ajibu, Jonas Mkude, Denis Richard, Hamad Waziri, Abdallah Seseme, Abdallah Suleiman, Adeyun Saleh, Miraj Athuman, Frank Sekule, Carlos Protas.
Wengine ni Mizar Kristom, Hija Ugando, Miraj Adam,Emily Mugeta ambaye kwa sasa yupo Marekani, Hassan Isihaka, Issa Ngoah na Ibrahim Twaha.
AJIBU YUPO HIVI
Akimzungumzia mshambuliaji Ibrahim Ajibu, tofauti na jamii ya mpira wa miguu nchini inavyomchukulia ni mvivu wa mazoezi, anasisitiza duniani wachezaji wenye vipaji vya kuzaliwa ni nadra kutoa asilimia 100 mazoezini.
"Wachezaji waliyozaliwa na vipaji, wanakuwa hawaoni sababu ya kutumia nguvu kubwa mazoezini, kwasababu hawafundishwi kila kitu, tofauti na mchezaji ambaye hana kipaji bali mpira wa kufundishwa huyo lazima afanye asilimia 100 ya mazoezi ili kujiweka sawa na kumshawishi kocha kuwapa nafasi," anasema meneja huyo na kuongeza;
"Talenti kubwa wakati wa mechi wanakupa matokeo ya asilimia 100, kuhusu Ajibu ana kipaji cha hali ya juu ndiyo maana huwezi kuona anajituma sana katika mazoezi ya kawaida ila akiingia uwanjani kiwango chake kinakuwa juu, hivyo mtazamo wangu dhidi ya Ajibu ni tofauti na jinsi watu wanavyomuongelea."
MTAZAMO WAKE KWA KAPOMBE
Kuhusiana na beki wa kulia Shomari Kapombe, anatamani katika misimu miwili au mitatu aliyo na nguvu ya kucheza uwanjani, amalizie soka lake Simba ili baadaye aanze kusogezwa katika mabenchi ya ufundi.
"Ingawa siwezi kumpangia Kapombe anachokitaka katika maisha yake, ila ninachotamani amalizie soka lake Simba ili aje kuagwa kwa heshima kubwa kama wengine ambao wameitumikia na wamesalia kwa majukumu mengine," anasema na kuongeza;
"Mfano mzuri kocha Selemani Matola, alianza kwa kuchezea Simba, akafundisha kikosi B ambacho kilikuwa na mafanikio ya hali ya juu ikiwa na wachezaji kama Said Ndemla, Jonas Mkude, Abdallah Seseme,Edward Christopher tulikuwa tunawapa kupitia michuano mbalimbali na walitengewa fungu maalumu la pesa na Simba la Friends wakati huo nilikuwa kwenye uongozi ingawa kuna muda nilikuwa nasaidiana na Matola kufundisha timu.
"Baadaye ulikuja mfumo wa kila timu inayocheza Ligi Kuu Bara iwe na kikosi B sasa sijajua kama wemeweka nguvu ya pesa kuendesha timu hiyo kwa upande wa Simba tulianza tena programu hiyo kuna kipindi mimi na Matola tulipewa tena jukumu la kusaka vipaji na programu hiyo inaendelea chini ya wengine."
Staa mwingine anayetajwa na Rweyemamu ni nahodha wa zamani wa timu hiyo, John Bocco anayeionoa Simba B kwa sasa jinsi alivyopewa heshima:"Natamani afuatie Kapombe pindi atakapoamua kustaafu, huo ni mtazamo wangu kwani mchezaji ana uhuru wake."
AMTAJA MO DEWJI
Anasema ni ngumu kumuweka nje ya mafanikio ya Simba, muwekezaji wa klabu hiyo Mohammed Dewji:"Kuwekeza pesa katika soka siyo kitu kidogo, katika hilo Mo Dewji anastahili heshima yake, kuna wakati mwingine nashangazwa na jinsi watu wanavyomfananisha na watu wengine."