Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuanza kwa Fainali za Kombe la Dunia 2026 ndiyo maandalizi ya fainali zingine

Muktasari:

  • Ongezeko hili limeleta ushindani mpya, matumaini mapya na fursa kubwa zaidi kwa mataifa mengi duniani, hususan yale yaliyokuwa yakipambana kwa miaka mingi kupata nafasi ya kushiriki jukwaa hilo kubwa zaidi la soka.

JUNI 11, 2026, dunia ya soka imehamia Amerika Kaskazini ambako fainali za Kombe la Dunia zimeanza rasmi nchini Marekani, Mexico na Canada. Hili ni toleo la kwanza la michuano hiyo kushirikisha mataifa 48, kutoka idadi ya awali ya timu 32 iliyodumu kwa muda mrefu.

Ongezeko hili limeleta ushindani mpya, matumaini mapya na fursa kubwa zaidi kwa mataifa mengi duniani, hususan yale yaliyokuwa yakipambana kwa miaka mingi kupata nafasi ya kushiriki jukwaa hilo kubwa zaidi la soka.

Kwa upande wetu Tanzania, tunapaswa kuitazama michuano hii kwa jicho la mbali zaidi ya kufurahia burudani, mbinu na ubora wa wachezaji wanaoshiriki. Tunapaswa kuanza sasa maandalizi ya kushiriki fainali zijazo, hasa Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2034 zitakazofanyika Saudi Arabia. Miaka minane inaweza kuonekana ni mingi, lakini katika ulimwengu wa maendeleo ya soka ni kipindi kifupi sana. Mafanikio ya kweli katika mchezo huu hujengwa kwa mipango ya muda mrefu, uwekezaji wa kimkakati na maandalizi endelevu.

Tanzania tayari imeonyesha maendeleo makubwa katika miaka ya hivi karibuni. Tukitazama michuano ya Afrika, tumekuwa washiriki wa mara kwa mara katika ngazi mbalimbali kuanzia timu za vijana, wanawake hadi timu ya taifa ya wakubwa wanaume. Hii ni tofauti kubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo taifa lilisubiri zaidi ya miongo mitatu kurejea kwenye fainali za AFCON kutoka 1980 hadi 2019.

Leo hii, kufuzu AFCON si jambo linaloshangaza tena; badala yake swali limekuwa kama taifa litakosekana vipi katika mashindano hayo.

Mafanikio hayo yamechangiwa pia na ongezeko la idadi ya timu katika AFCON kutoka 16 hadi 24. Ongezeko hilo limefungua milango kwa mataifa mengi yaliyokuwa nje ya ramani ya soka la Afrika.

Vivyo hivyo, FIFA imeongeza idadi ya washiriki wa Kombe la Dunia kutoka 32 hadi 48. Kwa bara la Afrika, hii ni habari njema kwani nafasi za moja kwa moja zimeongezeka kutoka tano hadi tisa, huku nafasi ya 10 ikipatikana kupitia mfumo wa mtoano dhidi ya mabara mengine.

Hali hii inapaswa kutupa matumaini ndoto ya Tanzania kucheza Kombe la Dunia si jambo la kufikirika tena. Kwa sasa, nafasi za Afrika zimeongezeka kwa kiasi kikubwa na ushindani umefunguka zaidi. Mataifa ambayo hapo awali yalionekana kuwa mbali na kiwango cha Kombe la Dunia sasa yana nafasi halisi ya kufuzu.

Tumeona mfano wa mataifa kama DR Congo na Madagascar yakizidi kujijengea uwezo wa kushindana katika kiwango cha juu. Katika eneo la Amerika Kaskazini na Karibiani, mataifa kama Curaçao na Haiti nayo yanaanza kuota ndoto kubwa kutokana na fursa zilizoongezeka.

Kwa Tanzania, hatua inayofuata inapaswa kuwa kujenga mradi maalumu wa miaka minane wenye lengo la kufuzu Kombe la Dunia la 2034. Mradi huo unapaswa kuhusisha maendeleo ya soka la vijana, kuboresha miundombinu, kuimarisha ligi za ndani, kuwekeza katika makocha wa kisasa na kuhakikisha vipaji vinatambuliwa mapema na kuendelezwa kwa viwango vya kimataifa.

Muhimu zaidi, tunapaswa kuachana na tabia ya kusubiri muda wa mashindano ukaribie ndipo tuanze kampeni za hamasa. Mafanikio makubwa hayajengwi kwa hisia za muda mfupi wala kwa kutegemea bahati. Mafanikio hujengwa kupitia mchakato wa muda mrefu wenye malengo yanayopimika na uwajibikaji wa kila mdau wa mchezo.

Tunapoangalia Kombe la Dunia la 2026 likianza, tusione tu tamasha la soka. Tulione kama darasa na chanzo cha msukumo wa kuanza safari yetu ya kwenda Kombe la Dunia la 2034. Ikiwa tutaanza sasa, tukaamini katika maandalizi, uwekezaji na mchakato wa muda mrefu, basi hakuna sababu ya Tanzania kushindwa kuwa moja ya mataifa yatakayoliwakilisha Afrika nchini Saudi Arabia. Ndoto hiyo inawezekana, lakini lazima tuanze kuijenga leo.