EXCLUSIVE: Usajili Kassim Dewji afunguka mazito Simba

Usajili Kassim Dewji afunguka mazito Simba

KASSIM Dewji ni moja ya viongozi wenye alama kubwa ndani ya klabu ya Simba kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa akiwa katika nafasi mbalimbali.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalum na Dewji baada ya kutangazwa kuchukua mikoba ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya usajili marehemu Zacharia Hanspope aliyefariki dunia hivi karibuni.

Katika mahojiano hayo na Kassim ameweka wazi mipango yake katika majukumu hayo mapya baada ya kujiweka nje ya kabumbu kwa muda mrefu.


MASTAA WAZAWA

Kassim anasema katika maisha yake ya mpira, yeye ni muumini mkubwa wa wachezaji wazawa, hivyo hiyo ndiyo silaa kubwa wakati wa usajili atawapa kipaumbele zaidi wenye vigezo.

“Kitu ambacho mimi upande naamini katika vipaji vya wachezaji wa ndani hivyo endapo nitapata nafasi ya kusajili basi nitawatazama zaidi wao,” anasema na kuongeza kwa;

“Wazawa wanahitaji heshima kubwa kwenye soka letu sambamba na kupatiwa nafasi kwani ndio muhimili wa taifa tunaweza tusipate faida kama klabu lakini wakalisaitia taifa kwenye timu yeyu ya Taifa,” anasema.


KAGERE KAMA GABRIEL

Licha ya nyota wengi ndani ya kikosi hicho lakini Kassim anamtaja Meddie Kagere (mwenye mabao manne) anafanya vitu ambavyo vinamkumbusha mbali anajikuta anamuona nyota wa zamani wa Simba Emmanuel Gabriel.

“Gabriel alikuwa mchezaji ambaye hakati tamaa kuipambania timu yake, alitumia dakika anazopewa kwa nguvu zake zote,angalau bidii naiona kwa Kagere ingawa hawawezi kufanana kila kitu,”anasema.

“Gabriel ni mchezaji mkubwa kwa upande wa wazawa kwani kimataifa amefanya mambo makubwa sana nakumbuka kipindi tunashiriki mashindano ya Kimataifa alizifunga timu zote tulizokutana nazo,”


ULE UTAWALA WA TARIMBA YANGA

Kassim anasema wakati akiwa Katibu, Yanga ilikuwa ikiongozwa na Abbas Tarimba ni uongozi ambao ulimtia kashkash kutokana na namna ambavyo walikuwa wakibadilishana katika matokeo.

“Yaani katika uongozi wake, sikumbuki ni mwaka gani, lakini nakumbuka upinzani ulikuwa mkubwa sana, leo tunawafunga kesho wanatufunga yaani tulikuwa tukibadilishana,” anasema.

Anasema uongozi huo ndio ulimpa changamoto na kumfanya apambane kuhakikisha hawawi wanyonge ndani ya timu yao kwa kufanya usajili wa maana na wa uhakika anajivunia hilo lilifanyika kwa wakati.


VIINGILIO HADI UWEKEZAJI

Nikiwa Simba na watani wakiongozwa na Jamali Malinzi timu hizi zilikuwa zinacheza sana michezo ya kirafiki sio kujiweka fiti pekee tulikuwa na malengo ya kukusanya fedha kwaajili ya kuziendesha.

“Ilifika kipindi tulikuwa tunaonyesha mastaa wetu kwenye mazoezi kwa kiingilio yaani Simba ikiwa inafanya mazoezi mashabiki wakija kuona tunawatoza fedha hili lilisaidia pia kuziongezea klabu pesa,” anasema.

Kassim anasema sasa kumekuwa na mabadiliko makubwea kutokana na timu kuwa na udhamini sambamba na wawekezaji kujitokeza kuwekeza na ndio maana unaona wachezaji wananufaika na hawapati changamoto za kifedha.

Anasema baada ya kubaini mashabiki wanazipenda timu zao ndio walipoamua kuanzisha tamasha kubwa maalumu kwaajili ya kutambulisha nyota wao wa msimu mpya Simba Day.

“Hata Simba Day nayo tuliianzisha kwa lengo la kujipatia kipato cha kuisaidia timu maana bila ya kufanya hivyo ilikuwa ngumu sana, tulikaa tukaona inafaa sana ili kutusaidia sisi kupata chochote kitu,”anasisitiza.


KUTOKA LAKI HADI MILIONI

“Ni miaka 20 sasa nikiwa Katibu Mkuu, ni muda mrefu sana nakumbuka mshahara mkubwa wa mchezaji ulikuwa 120,000 lakini kwa sasa mil 5, 6 na kuendelea, hata udhamini ilikuwa mil 105 kwa mwaka leo bil 15 kwa mwaka,”anasema na kuongeza kuwa kitakwimu kwa kipato kile na matokeo ambayo walikuwa wakiyapata hayatofautiani sana kipato kimeongezeka lakini matokeo bado ni yale yale.

“Ukubwa wa fedha wanazopata wachezaji wa sasa wanahitaji kubadili matokeo kwani wenzao walikuwa wanapata fedha kidogo lakini walikuwa ni wapambanaji maana ukiangalia matokeo ya zamani na sasa hakuna mabadiliko yangekuwepo tungeona mataji ya klabu bingwa,” anasema.


MSIMU HUU MH..

Kassim anasema udhamini mkubwa uliowekwa kwenye ligi umekuwa chachu ya ushindani mkubwa ndani ya timu kwani imeleta ushindani hii inatokana na wachezaji kupata fedha zao kwa wakati.

Anasema msimu huu anaona chachu ya mafanikio makubwa ya ligi, anaiona ikiwa bora huku akiizungumzia timu yake kuwa inakikosi kizuri na cha ushindani pamoja na kuanza vibaya kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa.

“Ni lazima kujua mwalimu anahitaji nini, bado ni mgeni labda ikifikia dirisha dogo atakuja na mapendekezo ya kutuambia wanahitaji nafasi gani na sisi tutafanya, katika mashindano sio kwamba usajili ndio unachangia timu kufanya vizuri, kwani matokeo ya mpira yanachangiwa na vitu vingi sana, unaweza kusajili wachezaji wazuri sana, lakini kama mwalimu hafikii ubora unaohitajika timu inaweza isifanye vizuri,”

“Yawezekana wachezaji wakawa na mapungufu, au hawalipwi kwa wakati hapo kufanya vizuri inakuwa ni kazi kubwa, ni jukumu letu sisi katika hizi kamati kufuatilia sekretarieti kuona kama wanafanya sioni ugumu wowote kwamba hatuwezi kufanya vizuri lakini sio rahisi kwa kuwa timu za ligi msimu huu zote zinapambana,” anasema.


SIMBA ILE YA NYUMA

“Uwezo wetu wa ubora wa kiwango cha juu kabisa, kikosi cha miaka hiyo kilichoitoa Zamalek kilikuwa na mchezaji mmoja pekee wa kigeni ambaye ni Ramadhan Waso pekee, leo kikosi kilichofika robo fainali wachezaji wa kigeni 10,” anasema na kuongeza kuwa timu inawachezaji kumi wa kigeni inashindwa kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa wakati timu miaka 20 iliyopita iliweza kufanya vizuri ikiwa na mchezaji mmoja wa kigeni. “Tunahitaji kujitafakari na kufanya usajili utakaokuwa na tija kwa timu.

“Ubora umekuwa mkubwa sana,maana ndio mambo ya mabadiliko ya nyakati tu,kikosi cha sasa kipo vizuri ingawa tumeondolewa katika Ligi ya Mabingwa mapema mno tofauti na matarajio imemshtua kilamtu na tunaamini kuna vitu vimesababisha hayo tutavifanyia kazi mapema,” anasema.”


KUGOMBEA WACHEZAJI

Anasema kwa ilipofikia Simba sasa haina sababu ya kugombea mchezaji na timu yoyote ya Ligi Kuu wanachokipambania sasa ni kuhakikisha wanafanya usajili wa nguvu bila kuhusishwa na timu nyingine kwani wana pesa za kutosha ambazo zinawafanya wasajili mchezaji yeyote.

Kassim anasema, ushabiki umekuwa mkubwa sana kwa sasa, na ndio maana unakuta Simba inamuhitaji mchezaji na wengine wanaibuka kitu ambacho kimechangiwa na mitandao ya kijamii zaidi.

“Tunatakiwa tufike mahali habari za kugombea wachezaji ziishe, na sisi kama Simba hatuna muda huo wa kugombea mchezaji, lakini timu nyingine zinaposikia tumefanya hivi zinakuja kwa mchezaji husika ndio mambo ya kimpira tena hayo,”anasema na hayo yote lengo ni kuwafurahisha wanachama wao.


ATAJA SIRI SIMBA KUFANYA VIZURI

Anasema uongozi imara na usimamizi bora wa timu ndio siri ya mafanikio hasa kwenye soka hili la kisasa.

“Huwezi kuiona Simba mwaka huu imefika robo fainali ukasema miaka miwili ijayo itacheza fainali, huwezi kufanya hivyo kwenye mpira, tunaweza kucheza robo fainali na tunaweza kutolewa makundi, tunaweza kutoka kwenye makundi tukacheza fainali inategemea wakati huo maandalizi yetu ni ya namna gani na uongozi mipango na malengo yao ni nini?,”anasema.


KASHKASHI NA MATAWI

Katika uongozi wake Kassim alikuwa akicharurana na matawi ya Simba haswa lile korofi wakati huo la Simba Talebani na kukiri kuwepo na sintofahamu ambayo waliitengeneza wao.

“Unajua walikuwa watu wangu ambao wameasi, Talebanui halikuwa tawi linalonipinga sema walikuwa watu wangu katika uongozi wafuasi wangu, lakini nilipobadilisha namna ya uendeshaji ambao ulianza kuwanyima maslahi waliamua kunikimbia.

“Waliona waniasi, walinigeuka, wakaamua kujiita Talebani ila ni marafiki zangu sana, japokuwa walikataa kwenda na mimi nilipokuwa nahitaji Simba iende lakini wapo ambao walisimama na mimi na wao waliendelea kuwa wapinzani.

“Lakini ikumbukwe muda mwingine upinzani ni muhimu na ni kitu kizuri sana, unapokuwa na upinzani inakufanya kuongeza jitihada katika ufanisi wa kazi ni vitu vya kawaida kwenye mpira,” anasema.


AMKUMBUKA AVEVA/MWAIKIMBA

Anasema alipokuwa Katibu Mkuu Simba, Evance Aveva alikuwa Mwenyekiti kamati ya usajili, hawakuwahi kumshindwa kupata mchezaji.

“Tulikuwa tukiamua huyu tunamsajili lazima tumpate, labda tuamue wenyewe kughairi, labda tupange tu mchezaji fulani hatumtaki ila kwa sababu wenzangu wanamtaka nakuwepo kwenye soka tu ili kumsaidia kwenda timu nyingine,” anasema na kuongeza kuwa;

“Mfano Gaudence Mwaikimba, hatukuwa na mpango naye baada ya kugundua Yanga wanamuhitaji tulimuongezea thamani kwa kumtaja kumuhitaji kumbe si mchezaji wa mipango yetu hivyo wenzetu wakawa wanahaha kumchukua na ilikuwa mipango tu,” anasema.


LUIS, CHAMA

“Mifumo ya kisasa lazima, uuze na kununua wachezaji, mfano mchezaji unayemchukua kwenye timu fulani kama na wao wangekuwa hawauzi ingekuwaje kila mtu abakie na wa kwake si ingekuwa kazi, hapa changamoto ya skauti ni namna gani ya kuuza mmoja na kuwapata watatu ambao wataziba nafasi ya yule mmoja.’


AMCHANA MKUDE, FEI TOTO

“Yaani maisha mazuri na raha zilizopo Tanzania ndio zinazowafanya walewe sifa na kuamini wanapata kila kitu na kusahau kwenda kujaribu maisha nje ya nchi ili kujiingizia kipato kikubwa zaidi.

“Wazawa wamekuwa wakitoka na kurudi sababu kubwa ni maisha mazuri ya nchini kwetu kutoka kwao na kurudi kwa sababu hawana malengo zaidi ya kucheza Simba na Yanga, Tanzania maisha ni mazuri sana, ndio maana mtu anaweza kumuomba mwenzake hata 20,000 akampa lakini nchi nyingine hakuna kabisa,”anasema akisisitiza wachezaji wajitume na kubadilisha fikra zao, ili kutoka zaidi kuliko ilivyo sasa. Anasema ; “Nchi hii imetawaliwa na upendo ndio shida kubwa inapoanzia na ndio maana ni ngumu mtu kufa kwa njaa, mchezaji akipata millioni zake sita akawa na sehemu ya kuishi anaona maisha kayapatia.”